Friday, March 17, 2017

RIDHIWANI KIKWETE AFURAHI BAADA YA KUHOJIWA NA MAMLAKA YA KUPAMBANA NA KUZUIA DAWA ZA KULEVYA.

Ridhiwani-Kikwete
Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ameeleza kufurahishwa kwake baada ya kuhojiwa na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya nchini.

Mbunge huyo amezungumza hayo jana jijini Dar es salaam baada ya kuhojiwa na Mamlaka hiyo, ambapo alisema roho yake imesuuzika kwani jamii imeamini kwamba hahusiki kwa namna yoyote ile na biashara hiyo haramu.

“nashukuru kwa kuhojiwa huku nimepata nafasi ya kueleza ukweli juu ya jambo hili ambalo lilishaanza kuleta taharuki katika jamii, sasa umma umejua kuwa siuzi wala sihusiki na dawa za kulevya roho yangu imesuuzika “alisema Ridhiwani.

Alisema vita ya dawa ya kulevya ni kubwa na inapaswa kupigwa na kila mmoja ili kuokoa kundi kubwa la vijana ambao wanaathirika kutokana na suala hilo na kwamba kuhojiwa kwake kumemfanya awe na amani.

“naunga mkono vita hii ya dawa za kulevya nchini kwani itasaidia kurudisha nguvu kazi inayopotea kutokana na matumizi ya dawa hizo za kulevya kwa mzazi ambaye mtoto wake ameathirika na matumizi ya dawa hizo anajua uchungu wake na hasara zake”alisema Ridhiwani.

Aidha aliongeza kuwa jamii inapaswa kusimama kwa kauli moja ili kuliokoa Taifa na nguvu kazi inayopotea ili Taifa liwe na vijana wanaojitambua na kutimiza wajibu wao katika kulitumikia taifa.

“Tunapoteza vijana wengi mno, Serikali imeamua kupambana nami kama Mbunge napiga vita uuzaji, utumiaji na usambazaji na kwa kuwa umma ushajua sihusiki na chochote basi naweza kuwa balozi mzuri wa kupiga Vita suala hili .”alisema Ridhiwani.

Akizungumzia suala la marafiki zake kuhusishwa na biashara hiyo haramu alisema kuwa sio marafiki zake bali ni watu anaokutana nao katika maeneo anayotembelea.

“kamishina ameaniambia walioonekana kufanya biashara hiyo sio marafiki zangu bali ni watu ninaokutana nao katika maeneo ninayotembelea wanakuja kunisalimia na kutaka kunizoea kwa ajili kuna watu wanaopenda kutumia watu kama sisi ili kujificha kutokana na maovu wanayofanya”alisema ridhiwani.

Ridhiwani alisema kuwa mchakato huo wa kupambana na dawa za kulenya nchini umekuwa ukiwachanganya wananchi kwani haieleweki ni nani anayehusika na kushugulikia suala hilo.

“huu mchakato umekua ukichanganya kuna watu wanaitwa kwa Kamanda Sirro na wengine wanaitwa kwa Kamishina Sian’ga mfano Msanii Vanessa Mdee ambaye ameitwa kwa Kamanda Sirro badala ya kwa Kamishina Sianga”alisema Ridhiwani.

Alisema kuwa watu wanahoji kwa nini wengine watangazwe hadharani na wengine kuitwa  kimya kimya na ameongeza kuwa ni vyema mamlaka zikajipanga ili kufanikisha vita hii na kufikia malengo yake ya kumaliza tatizo la dawa za kulevya nchini.

No comments:

Post a Comment