KIINGILIO TAIFA STARAS NA BOTSWANA 3,000.
Taifa Stars – timu ya Tanzania ya mpira wa miguu kwa mwaka 2017 inaingia
uwanjani kucheza na Botswana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi
ya kirafiki ya kimataifa katika wiki ya kalenda ya FIFA.
Kwa umuhimu wa mchezo huo na hamasa ambayo uongozi wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania umeona hivyo TFF imeatangaza kushusha bei ya kiingilio kwa
watu watakaokaa mzunguko kutoka Sh 5,000 hadi Sh. 3,000.
“Wavutieni Watanzania wakaishangilie timu yao, wekeni viingilio vya bei
ya chini ambayo Mtanzania itamweka katika mazingira ya kuchangia gharama kidogo
kwa timu. Toeni hiyo Sh 5,000 yenu. Wekeni angalau Sh. 3,000,” ameagiza Rais wa
TFF, Jamal Malinzi.
Pamoja na punguzo hilo kwa mashabiki wa mpira wa miguu watakaoketi
Majukwaa Maalumu – VIP “A” watalipia Sh 15,000 na wale watakaoketi VIP “B” na
“C” watalipia Sh 10,000.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga kwa upande wake aliwathibitishia
Waandishi wa Habari kwamba kikosi chake kiko imara kwa ajili ya mchezo huo
utakaofanyika kuanzia saa 10.00 jioni.
“Tuna morali wa hali ya juu,” alisema Mayanga ambaye aliteuliwa kuinoa
timu hiyo mapema mwaka huu.
Kwa upande wa Peter Buffler – Kocha Mkuu wa Botswana, alisema kwamba
anatarajiwa mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa sababu amegundua kuwa kikosi cha
Taifa Stars kina vijana wengi ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Mbali ya mchezo huo wa kesho, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mchezo
mwingine dhidi ya Burundi Jumanne ijayo, Machi 28, mwaka huu. Mchezo ambao pia
ni wa kirafiki wa kimataifa unatarajiwa kuanza saa 10.00 jioni.
No comments:
Post a Comment