MAAFISA Habari na Mawasiliano Serikalini wametakiwa kutoa taarifa kwa
haraka zaidi kwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano ikiwemo tovuti na
mitandao ya kijamii ili kusaidia kutangaza Mafanikio ya Serikali katika maeneo
yao ya kazi.
Hayo yamesemwa jana Mkoani Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Habari
(MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, alipokuwa akizungumza
na maafisa habari na TEHAMA katika mafunzo elekezi ya uwekaji wa taarifa katika
tovuti yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kusimamiwa
na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (EGA).
Dkt. Abbas alisema kuwa mara baada ya tovuti kuzinduliwa rasmi, Maafisa
Habari wana wajibu wa kuweka taarifa mpya zinazozingatia muda na wakati kwa
kuwa malengo ya tovuti hizo ni kumsaidia mwananchi kuweza kupata taarifa
mbalimbali za Serikali.
“Tukifungua tovuti hizi tunapaswa kuona taarifa mpya, kwa sasa suala la
upashanaji wa habari na taarifa za miradi ya Serikali isisubiri tena
michakato, isipokuwa kama kutatokea suala kubwa ambalo litahitaji ufafanuzi
kutoka katika ngazi za juu katika maeneo yenu ya kazi” alisema Dkt. Abbasi
Aliongeza kuwa, taaluma ya habari katika zama za sasa inahitaji ubunifu
mkubwa katika kuisemea Serikali kwa kutafuta njia mbalimbali za kubaharisha
umma badala ya kutumia njia za kawaida na za kila siku.
“Katika maeneo yetu ya kazi tuna vituo vya redio na televisheni ambazo
zinawahitaji Viongozi wetu kufanya nao mahojiano maalum kuhusu masuala
mbalimbali ya Serikali, ni wajibu wetu kutumia fursa hizo kuhakikisha
tunaisemea Serikali” alisema Dkt. Abbasi.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema Serikali itaweka utaratibu maalum wa
kupima utendaji kazi wa kila Afisa Habari katika Wizara, Idara, Taasisi, Wakala
na Mamlaka za Mikoa na Wilaya na Mikoa ili kuona ni namna gani ameweza kutoa
taarifa za Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali.
“Katika kipindi hiki Serikali ya Awamu ya tano imetekeleza na inatekeleza
miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miradi ya umeme vijijini (REA), na ujenzi
wa miundombinu mingine kwa kutumia fedha nyingi katika kutekeleza miradi hiyo,
hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kueleza wananchi utekelezaji wa miradi hiyo”
alisema Dkt. Abbasi.
Alisema kuwa ili taarifa hizo za utekelezaji wa mafanikio hayo ya
Serikali ziweze kuwafikia wananchi, ni wajibu wa Maafisa Habari na Mawasiliano
kujenga na kuimarisha mtandao wa mawasiliano baina yao pamoja na
watendaji wengine katika maeneo yao ya kazi.
Aliongeza kuwa ubunifu ni siri nyingine ya mafanikio katika suala la
upashanaji wa taarifa za Serikali, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuwa
mbunifu badala ya kulalamika kutokana na changamoto mbalimbali zinazomkabili
katika maeneo yao ya kazi ikiwemo ufinyu wa bajeti na changamoto ya ukosefu wa
vitendea kazi.
Mafunzo hayo ya wiki moja yalishirikisha mikoa na Halmashauri za Mikoa ya
Arusha, Manyara, Singida, Dar es salaam, Pwani na Dodoma.
No comments:
Post a Comment