Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma akifungua Kongamano la
maazimisho ya siku ya Kifua kikuu Duniani katika ukumbi wa sanaa Rahaleo
(kulia) mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Ghirman na (kushoto) Mkurugenzi
Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jamala Taib.
Baadhi
ya wanafunzi wa vyuo vikuu walioshiriki Kongamano la maazimisho ya siku ya
Kifua kikuu Duniani katika Ukumbi wa sanaa Rahaleo wakimsikiliza Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Amali alipokuwa akifungua Kongamano hilo.
Mratibu
kitengo cha ufuatiliaji na tathmini mwenendo wa maradhi ya Ukimwi, Kifua Kikuu
na Ukoma Zanzibar Asha Ussi Khamis akitoa mada yake ya matokeo ya utafiti juu
ya uelewa, tabia na matendo juu ya kifua kikuu Zanzibar katika ukumbi wa sanaa
Rahaleo Mjini Zanzibar.
Mmoja
wawashiriki wa kongamano la kuazimisha siku ya Kifua kikuu Duniani kutoka Skuli
ya Afya na Sayansi ya Tiba (SUZA) Mariam Ali Mansour akichangia moja ya
mada zilizowasilishwa.
..........................
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma amewataka vijana
wasomi kujikita katika kufanya tafiti mbali mbali ili kupata majibu sahihi ya
matatizo yanyoikabili nchi ikiwemo maradhi.
Amesema yapo matatizo mengi yanayoikabili jamii ya Zanzibar na yanahitaji
majibu ya kisayansi ili kusaidia kupiga hatua katika kufikia maendeleo.
Waziri Riziki alieleza hayo alipokuwa akifungua kongamano la maadhimisho
ya siku ya Kifua Kikuu Duniani lililowashirikisha wanafunzi wa Vyuo vikuu
Zanzibar katika Ukumbi wa Wasanii Rahaleo.
Alisema maradhi ya kifua kikuu ni miongoni mwa maradhi hatari duniani na
kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya (WHO) mwaka 2015 watu milioni 10.4
waliugua ambapo milioni 1.8 walifariki.
Aliitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi 30 Duniani zinazoongoza kwa
maradhi ya kifua kikuu hivyo juhudi zaidi zinahitajika katika kukabiliana na
maradhi hayo.
Waziri Riziki ambae pia ni Kaimu Waziri wa Afya alisema hali sio nzuri
pia kwa Zanzibar na watu 700 hadi 800 wanaugua kifua kikuu kila mwaka na baadhi
yao hupoteza maisha.
Alizitaja dalili za maradhi ya Kifua kikuu kuwa ni kukohoa kwa kipindi
kirefu, kutoa makohozi yenye damu, homa za mara kwa mara hasa wakati wa jioni,
kutokwa na jasho jingi wakati wa usiku, kukosa hamu ya kula na hatimae kupungua
uzito.
Aliwashauri wananchi wasisite kufika katika vituo vya afya wanapoona
dalili hizo ili kupata matibabu katika hatua za awali kwani maradhi hayo
yanatibika kwa urahisi na dawa zake zinapatikana bila malipo.
Alisema miongoni mwa sababu zinazopelekea kupata maradhi hayo ni
msongamano wa watu hasa sehemu za mijini ujenzi holela wa nyumba za kuishi kwa
vile maradhi hayo yanaambukizwa kwa njia ya hewa.
Akitoa salamu za Shirika la Afya Duniani (WHO), Mwakilishi wa Shirika
hilo Zanzibar Dkt. Ghirman Andermichael alisema kifua kikuu ni janga la Dunia
hivyo kila mmoja anawajibu wa kushiriki katika kuhakikisha maradhi hayo
yanapungua kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2025.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki Kongamano hilo waliishauri Wizara ya
Afya kuandaa wataalamu na vifaa vya kutosha vya kuchunguza maradhi hayo katika
Hospitali na vituo vikubwa vya Afya.
Dunia huadhimisha siku ya Kifua kikuu kila ifikapo Machi 24 na
kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni Kifua kikuu ni janga la Taifa.
Tuungane kutokomeza Kifua
kikuu.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment