Sunday, March 5, 2017

KIGOGO WA DAWA ZA KULEVYA NCHINI ATIWA MKONONI.

Kamishna wa kupambana na Dawa za  kulevya  nchini, Rogers  William  Sianga alipokuwa Bagamoyo leo jumamosi 04 March 2017.
................................

Hatimae kigogo wa dawa za kulevya nchini anaswa pamoja na wengine watano ambao nao ni vigogo wa kusambaza dawa za kulevya.


Hayo yamebainishwa mjini Bagamoyo na  Kamishna wa kupambana na Dawa za  kulevya  nchini, Rogers  William  Sianga,  alipokuwa akizungumza katika hafla fupi iliyoandaliwa na Group la MABEST kwa kushirikiana na  Shirikisho  la Mpira wa Miguu Tanzania TFF,  iliyofanyika leo tarehe 04, Machi 2017,  katika Kituo cha  Life and Hope kilichopo Ukuni wilayani Bagamoyo.

 Sianga  alisema  kigogo huyo  ambae hakumtaja  jina  ni miongoni mwa wasambazi wakubwa wa dawa za kulevya hapa nchini na kwamba  kukamatwa kwake kunaleta  matumaini katika vita ya  kupambana na Dawa za kulevya.

Alisema mpaka sasa zaidi ya watu 11,000 wamekamatwa nchini ambao kati yao wapo watu watano ni vigogo wa biashara  ya dawa za kulevya na juhudi zinaendelea za kuwasaka wote  wanaohusika na  biashara  hiyo inayoangamiza nguvu  kazi yaTaifa.

Aliongeza kwa kusema  kuwa vita dhidi ya Dawa za  kulevya  ni  ngumu hivyo  inahitajika ushirikiano  kutoka kwa  wananchi  ili kuweza kufanikisha  vita hiyo.

Kamishna  Sianga, alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa  ili kila anaehusika achukuliwe hatua kali za kisheria na hatimae nchi ibaki salama bila ya Dawa za kulevya.

Hafla hiyo ambayo Kamishna wa Kupambana na Dawa za kulevya nchini, Rogers w. Sianga alikuwa mgeni rasmi imehudhuriwa na Viongozi wa wilaya ya Bagamoyo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini, Jamali Malinzi  pamoja na timu  ya vijana wenye umri wa  chini yamiaka  17  (Serengeti Boys),  Baraza  la viongozi wa dini nchini  pamoja na  wadau mbalimbali wakupambana na Dawa za  kulevya  wa ndani na nje ya nchi.

HALI YA DAWA ZA KULEVYA WILAYANI  BAGAMOYO.
 Katibu Tawala wilaya ya Bagamoyo, Erica Yegela akizungumza kwenye  hafla hiyo.

Akielezea hali ya Dawa za kulevya Wilayani Bagamoyo, Katibu Tawala wilaya ya Bagamoyo, Erica Yegela alisema mpaka sasa jumla ya watu  17  wanashikiliwa na  polisi katika Halmashauri ya  Bagamoyo na Chalinze ambapo Bagamoyo ni saba na  kati yao mmoja  amekutwa na kete  82  za Dawa za kulevya  na mwingine  amekutwa  na Purling  136 kete 164 za  Bangi, kete 9 za Dawa za kulevya  aina ya Heroin na Pombe ya Gongo.

Aidha, katika Halmashauri ya Chalinze ambayo  ni Wilaya ya Kipolisi wamekamatwa wauzaji  10  wa Dawa za kulevya na wanne ni watumiaji na kuongeza kuwa Dawa za  kulevya  zilizokamatwa ni mirungi  gram 500, Bangi Gram 497,  na  Heroin Gram  0.5 na kwamba  watuhumiwa wote  wamefikishwa Mahakamani na  kesi  zao  zinaendelea.

Katibu Tawala huyo aliongeza  kuwa mikakati  iliyojiwekea  wilaya ni kufanya  doria  za mara  kwa mara ili  kubaini  uingizwaji wa dawa za kulevya kutoka nje ya Bagamoyo.

Hata hivyo alisema  changamoto iliyopo ni  uwepo wa Bandari  bubu ambazo  pia hutumika  kuingiza Dawa za kulevya  na kusema kuwa Bagamoyo ina jumla ya  Bandari bubu  17.

MKURUGENZI WA LIFE  AND HOPE,  SOBA - BAGAMOYO,  AZUNGUMZA
 Mkurugenzi wa Life and Hope, SOBA- BAGAMOYO. Al-Karim Sadrudin Bhanji, akizungumza katika hafla hiyo.

Akizungumza mbele ya  mgeni  rasmi, Mkurugenzi  wa  kituo cha  Life And Hope Soba House Bagamoyo, Alkarim  Banji alisema kituo hicho kimeanzishwa kwa lengo la  kusaidia vijana  walioathirika na matumizi  ya  Dawaza za kulevya   ili  kuokoa nguvukazi ya Taifa.

Aliongeza kuwa  kituo hicho  kinakabiliwa na  changamoto kadhaa,  ikiwemo  eneo la majengo kwani eneo  lililopo sasa ni  la kukodi  jambo  ambalo  linaleta  ugumu  katika uendeshaji.

Alisema kutokana na  kukosa  eneo na  majengo ya kutosha  wanashindwa kupokea  waathirika wajinsia  ya  kike kutokana na ufinyu  wa nafasi.
Alitumia nafasi hiyo  kuiomba serikali kuwapa ushirikiano ili kupanua kituo hicho ambacho ni msaada mkubwa  kwa  vijana walioathirika na Dawa za kulevya.

RAIS WA TFF ASEMA NENO.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu hapa nchini, Jamali Malinzi alisema  wamefikia uamuzi  wa kuipeleka timu ya Serengeti Boys  katika kituo cha SOBA HOUSE Bagamoyo ili waweze kujifunza madhara yatokanayo na Dawa za kulevya ili nao wasiingie kwenye janga hilo ambalo ilina athiri nguvu kazi ya Taifa.

Alisema asilimia kubwa ya vijana  wapo kwenye hatari ya kutumia Dawa  za  kulevya kutokana na vishawishi mbalimbali wanavyopata katika jamii kutoka  katika makundi rika tofauti.

Aliongeza kwa kusema  kuwa katika mpira  wa miguu kwenye kanuni za mashindano kanuni  ya 36 (7)  kwenye  kanuni za Ligi  kuu ya Vodacom, inakataza Rushwa, matumizi ya Dawa za  kuongeza  Nguvu, matumizi ya Madawa ya kulevya, ubaguzi wa aina yoyote, fujo,  na michezo  ya  kamali.

Alisema Taifa la Tanzania  linajivunia kuwa na vijana wa Serengeti Boys ambao  wanaipeperusha vyema Bendera ya  Taifa na  kuweza  kushiriki fainali  za Afrika  za vijana chiniya miaka 17 zitakazofanyika nchini Gabon.
Alisema  ili kuweza kulinda nguvu kazi ya taifa ni vyema jamii ikajikita katika  kuwaenzi na kuwalinda vijana wasiweze kuingia katika  matumizi ya  Dawa za kulevya.

Malinzi alisema katika  kuonyesha upendo kwa SOBA HOUSE Bagamoyo, TFF imekabidhi Jezi 60 za michezo kwa vijana waliopo SOBA HOUSE Bagamoyo,  Mipira 3, pamoja na pesa taslimu shilingi milioni  mbili na  laki mbili, 2,200,000/=.

VIONGOZI  WA DINI  WAIUNGA  MKONO SERIKALI.
Kwa upande wao  viongozi wa dini  waliofika katika  hafla hiyo walisema dini  zote zinakataza aina zote za ulevi ikiwemo matumiziya dawa za kulevya na  kwamba  viongozi wa dini watashirikiana  na Serikali  katika kupiga  vita uuzaji na matumizi ya Dawa za kulevya hapa  nchini  ili Taifa  libaki na  wananchi wenye afya bora  na nguvu ya  kulitumikia Taifa.

Walisema madhara ya Dawa za kulevya  katika jamii yanamgusa kila mtu bila kujali cheo chake, dini yake  wala uwezo  wake kwani vijana wanaoathirika  ni wote hata  kama  angekuwa mtoto  wa  sheikh, Mchungaji  au  Padri  makundi ya vishawishi yakimuingia  anaweza  kutumbukia  kwenye  janga hilo. 

VIJANA WA LIFE  AND HOPE,  SOBA-BAGAMOYO.
Kwa upande wao waathirika  wa matumizi  ya  Dawa za  kulevya  wa SOBA HOUSE  Bagamoyo  walisema wanampongeza  Mkurugenzi wakituo hicho kwa kuanzisha  kituo ambacho  kimewasaidia kuondokana na matumizi  ya Dawa  za kulevya  na hatimae kurudi  katika hali ya kawaida na  kwamba  baadhi yao  wana  uwezo wa kufanya  kazi ya  kulitumikia  Taifa.

Meneja wa kituo hicho,  Godwin  Msilo  ambae  awali  alikua  mtumiaji wa Dawa za  kulevya alisema  kwa sasa  yuko vizuri na kwamba  ana  uwezo mzuri wa kufanya  kazi  na  kuwasimamia  wengine  ili  waweze kufanikiwa kama  yeye.

Aidha,  aliwasihi vijana  kuacha tabia za  kuiga  kila kitu katika jamii  na kuepuka makundi ya maovu kwani hayo  ndio  chanzo cha  matumizi ya Dawa za kulevya.
Hafla hiyo fupi  iliyofanyika  katika  kituo  cha  Life And  Hope Rehabilitation Organization (SOBA-BAGAMOYO) imeandaliwa na Kikundi cha MABEST kwakushirikiana na Shirikisho  lampira wa miguu  nchini  (TFF)  lengo  likiwa ni kuwafariji wale  waliofanya  maamuzi ya kuacha  kutumia  Dawa  za  kulevya  pamoja na  kuunga  mkono  juhudi  za  Serikali  za  kupiga vita Biashara na matumizi ya  Dawa za kulevya  hapa nchini.
Kocha mkuu wa timu ya Serengeti Boys Kim Poulsen,  akiwa na vijana wake wa Serengeti Boys ndani  SOBA -BAGAMOYO katika hafla hiyo iliyofanyika leo Tarehe 04 Machi 2017.

Vijana kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni  Bagamoyo (TaSUBa) wakionyesha  igizo  la madhara ya kutumia Madawa ya  kulevya.

Mkurugenzi wa Life and Hpo, SOBA- BAGAMOYO, Al Karim Bhanji. akikabidhiwa vifaa vya michezo na  Kocha  Mkuu  wa  timu ya Serengrti Boys Kim  Poulsen, vilivyotolewa na TFF, wanaoshuhudia ni  Kamishna wa kupambana na Dawa za kulevya nchini, Rogers Sianga na Rais waTFF Jamali  Malinzi.

No comments:

Post a Comment