Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
ametoa mwezi mmoja kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari kuwasilisha
taarifa za wanafunzi waliopata mimba pamoja na kuolewa wakiwa bado wanasoma.
Maelekezo hayo yametolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri Ummy
Mwalimu alipokuwa akizindua Ripoti ya Utafiti wa Visababishi na Madhara ya Ndoa
za Utotoni nchini Tanzania uliofanywa kwa ushirikiano wa Wizara hiyo na
Mashirika yasiyo ya Kiserikali yakiwemo ya Plan International, Children’s
Dignity Forum, UNFPA, FORWARD pamoja na REPOA.
Alisema, wakati Sheria ya Ndoa inafanyiwa marekebisho, wizara yake
inatumia marekebisho ya Sheria ya Elimu yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mnamo June 2016 ambayo yanakataza mtu yoyote kumuoa mtoto
wa shule ya Msingi au Sekondari kwani ni kosa la jinai lenye adhabu ya miaka 30
jela.
“Sheria hii inamtaka Mwalimu Mkuu kuandaa taarifa ya kila robo mwaka
kuhusu jumla ya watoto waliopata ujauzito na kuolewa wakiwa bado wanasoma na
taarifa hiyo kupelekwa kwa Kamishna wa Elimu, lakini tangu sheria hiyo ianze
kutumika hakuna Mwalimu Mkuu aliyetii sheria hiyo hivyo natoa maelekezo kwa
walimu hao kukusanya taarifa hizo ndani ya mwezi mmoja,”alisema Waziri Ummy.
Ameongeza kuwa bila kuwapeleka wazazi na wahusika wa matukio hayo
mahakamani na kufungwa tatizo hilo haliwezi kuisha nchini.
Aidha, Waziri Ummy amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kila
Halmashauri kupita nyumba kwa nyumba kuwaibua wazazi wanaofanya vitendo hivyo
na kuwasilisha taarifa hizo sehemu husika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa
sheria hiyo.
Ametoa rai kwa Wadau wote wa Maendeleo nchini kwenda zaidi Vijijini kuwasaidia
wanawake na wasichana waliopo huko kwani ndio maeneo yenye waathirika wengi wa
matatizo ya ndoa pamoja na mimba za utotoni.
Nae, Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka Shirika la Plan
International – Tanzania, Jane Mrema amesema, mnamo mwaka 2016 ripoti ya
wasichana ilionyesha nafasi ya watoto wa kike ulimwenguni haionekani kwa sababu
takwimu zinazowahusu ziko nyuma ya wakati, hazijakamilika na muda mwingine
tafiti zake hazifanyiwi utekelezaji.
“Nchini Tanzania hatuna takwimu sahihi zinazoonyesha uhalisia wa
changamoto anazozipata mtoto wa kike kutokana na ndoa za utotoni na hiyo ndio
sababu kubwa iliyopelekea shirika letu kuungana na Serikali pamoja na mashirika
mengine kufanya utafiti huu ambao tumeuzindua rasmi leo,”alisema Bi. Jane.
Amefafanua kuwa shirika hilo pamoja na Serikali ya Canada wamejitolea
fedha kwa ajili ya kuandaa vitabu vinavyoonyesha tafiti hizo katika lugha ya
Kiswahili na kiingereza ambavyo watavigawa mashuleni na mitaani ili kuweza
kuwasaidia watoto kupata uelewa na maarifa juu ya athari za ndoa hizo.
Shirika hilo linaendelea na harakati za kupigania kumaliza tatizo hilo
nchini ambapo kwa sasa wamezindua Mpango Kazi wa miaka 5 unaoanza mwaka 2017-
2022 ukiwa na lengo la kuwasaidia wasichana zaidi ya 1,000,000 ulimwenguni kote
ambao utawawezesha wasichana kujitambua, kujisimamia na kuhakikisha hakuna
anayeachwa nyuma katika suala zima la maendeleo.
No comments:
Post a Comment