TAARIFA
YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO MHE. UMMY ALLY
MWALIMU (MB) KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE
DUNIANI YA MACHI 8, MWAKA 2017
Nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa
itaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake kitakuwa tarehe 8
Machi, 2017 na kwa mwaka huu itafanyika katika ngazi ya mkoa kwa kuzingatia
amzingira ya mkoa husika.
Aidha Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka 2017 ni “TANZANIA YA VIWANDA:
WANAWAKE NI MSINGI WA MABADILIKO YA KIUCHUMI”. Kaulimbiu hii imetoholewa
kutokana na Kaulimbiu ya Kipaumbele ya Umoja wa Mataifa mwaka huu katika
Mkutano wa 61 wa Hali ya Wanawake Duniani (CSW) inayosema “Women Economic Empowerment in the Changing World of Work” ambayo tafsiri yake kwa lugha ya kiswahili
ni “Uwezeshaji Wanawake: Kiuchumi Katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi”.
Kaulimbiu hii ya “Tanzania ya Viwanda: Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko
ya Kiuchumi” inalenga kuhamasisha jamii, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi,
Taasisi za Serikali, Vyama vya Siasa, Wabia wa Maendeleo, mtu mmoja mmoja na
wadau wengine hapa nchini Tanzania kuongeza wigo wa fursa za kiuchumi kwa
wanawake ili kuwawezesha kushiriki na kunufaika na hatua za maendeleo katika
kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati na wa viwanda.
Chimbuko la kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa miaka
ya 1900 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini
Marekani kupinga mazingira duni ya kazi. Waandamaji hao, walilalamikia ukosefu
wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira ikiwemo
wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa ukilinganisha na wanaume.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Umoja wa Mataifa baada kuanzishwa mwaka 1945
uliridhia kuwa tarehe 8 Machi kila mwaka iwe ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake
Duniani. Uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuanzisha Siku ya Wanawake Duniani
ulitokana na ukweli kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake
yalihitaji msukumo maalumu na wa kipekee.
Lengo kuu la kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kutoa fursa kwa
jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali
za Kimataifa, kikanda na kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya
jinsia na uwezeshaji wanawake. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa haki za
wanawake kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa zinapatikana na zinalindwa.
Kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu
wa kutambua na kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta
maendeleo pamoja na kuelezea jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na
wadau mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili waweze
kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo yao, familia zao, jamii na
Taifa kwa ujumla.
Aidha wanawake ni kundi kubwa na muhimu katika jamii (asilimia 51 ya
Watanzania Wote) na kwamba hakuna maendeleo yeyote yanayoweza kufikiwa ikiwa
kundi hili litaachwa nyuma.
Kwa mantiki hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikichukua
hatua mbalimbali katika kuhakikisha wanawake wanashiriki na kunufaika na uchumi
hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu imejipanga kuelekea katika uchumi wa
viwanda na kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Taarifa ya Jukwaa la Uchumi Duniani kuhusu ‘Pengo la Jinsia ya Mwaka
2016’ inaonesha kuwa kutokana na jitihada zilizofanyika nchi yetu inashika
nafasi ya 53 kati ya nchi 144 zinazofanya vizuri katika masuala ya jinsia
Duniani.
Katika jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi Serikali
imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambao unatoa mikopo yenye masharti
nafuu kwa ajili ya kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogo kuanzisha na
kuendeleza biashara, viwanda vidogo, kilimo pamoja na shughuli nyingine za
kiuchumi.
Aidha kupitia Mfuko huo, Halmashauri zimehamasishwa kuchangia asilimia
tano ya mapato yao ya ndani ambapo katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2016
kiasi cha shs. 4,102,808,513 kilitolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana
katika Halmashauri 101 kupitia utaratibu huu.
Benki ya Wanawake Tanzania pia ilitoa mikopo yenye thamani ya Shs 9,323,240,000/-
kwa wajasiriamali 6,267 kati ya hao wanawake walikuwa 4,596. Hivyo, kiasi cha
mikopo iliyotolewa imeongezeka kutoka Tshs. 112,473,600,000/- mwaka 2015 hadi
kufikia Shs 121,796,840,000/- mwaka 2016.
Aidha, idadi ya wajasiriamali waliopata na kunufaika na mikopo
inayotolewa na Benki ya Wanawake Tanzania iliongezeka kutoka wajasiriamali
79,983 mwaka 2015 hadi kufikia wajasiriamali 86,250 mwaka 2016 ambapo asilimia
73 ya wanufaika wa mikopo hiyo ni wanawake.
Kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika fursa mbalimbali za
kiuchumi, Serikali imeratibu na kuzindua majukwaa ya uwezeshaji wanawake
kiuchumi. Majukwaa haya yatatumika kama sehemu muhimu kwa wanawake
wajasiriamali kukutana na kujadili fursa za kiuchumi pamoja na changamoto
mbalimbali zinazowakabili na namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo.
Aidha, sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002, (ilivyofanyiwa
marekebisho mwaka 2007) imetoa fursa sawa za ajira kati ya wanawake na wanaume.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, pale inapotokea mwanaume na mwanamke wanapata alama
sawa wakati wa usaili, mwanamke anapewa kipaumbele kupata nafasi hiyo.
Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini (2004) imetoa fursa sawa kati ya
wanawake na wanaume kuhusu haki zao za ajira, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa
likizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume.
Kwa kutambua elimu na mafunzo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha
wanawake na wanaume wanashiriki na kunufaika ipasavyo na uchumi wa viwanda,
Serikali imeendelea kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu kama haki ya
msingi.
Katika kuhakikisha kuwa mtoto wa kike na wa kiume wanapata haki ya elimu,
Serikali inatekeleza sera ya Elimu bila malipo ambayo inatoa fursa ya Elimu ya
Msingi na ya Sekondari na kuwahakikishia watoto elimu hiyo bila kujali tofauti
za kiuchumi.
Sera hii imeleta mafanikio makubwa katika eneo hili ambapo takwimu
zinaonesha kuwapo ongezeko la udahili kwa watoto wa kike na kiume
Pamoja na masuala yote yaliyotajwa hapo juu Kumekuwepo na ongezeko la
ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
Marekebisho ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1995 na ya mwaka 2005 yalifanywa na
kuongeza idadi ya viti maalum kwa wanawake vilivyoongezwa hadi kufikia asilimia
30.
Katika kuhakikisha kuwa wanawake wanajengewa uwezo wa kisheria na kupata
haki zao, sheria kadhaa zimetungwa na nyingine kufanyiwa marekebisho ikiwemo
Sheria ya Makosa ya Kujamiiana yaani (SOSPA) ya mwaka 1998, ambayo
imefanyiwa marekebisho na kuhuishwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu.
Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo imetoa
fursa sawa katika ajira na likizo ya Uzazi pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka
2009; Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999, ambapo sheria
hii inampa mwanamke haki ya kumiliki na kurithi ardhà sawa wanaume.
Pia, katika mwaka 2016/17 Bunge la Jamhuria ya Muungano limepitisha
Sheria ya Msaada wa Sheria ya mwaka 2016 ambayo itasawadia wanawake hasa wenye
kipato cha chini kupata haki zao za msingi.
Serikali inatambua kuwa ukatili dhidi ya wanawake bado ni tatizo kubwa
ambalo linaathiri ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Katika kukabiliana na tatizo
hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Mpango Kazi wa
Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22) ambao
ulizinduliwa tarehe 13 Disemba, 2016.
IMETOLEWA NA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO
No comments:
Post a Comment