Saturday, March 18, 2017

UJENZI WA BARABARA ZA JUU UBUNGO, JPM KUWEKA JIWE LA MSINGI.

UBU1
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na  Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim wanatarajiwa kuweka   jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za juu (Ubungo interchange)  eneo la  Ubungo jijini Dar es Salaam Machi 20 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inasema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo yatagharimu  takribani shilingi bilioni 188.71 ambapo una  lengo kupunguza msongamano wa magari katika barabara za Morogoro, Nelson Mandela na Sam Nujoma.

“Mradi huo ni sehemu ya uboreshaji usafiri Jijini Dar es Salaam yaani (Dar es salaam Urban Transport Improvement Project), utakaogharimiwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia na mchango wa Serikali ya Tanzania” .

Aidha, taarifa hiyo ilisema kuwa, mradi huo utahusisha pia awamu ya tatu na ya nne ya ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (Bus Rapid Transit- BRT), katika barabara ya Nyerere kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam hadi Gongo la mboto na barabara ya Bagamoyo kutoka katikati ya jiji hadi Tegeta.


No comments:

Post a Comment