Viwanja
vya Nyerere Square mjini Dodoma mahali ambapo kutafanyika sherehe za kuwapokea
viongozi mbalimbali wa serikali baada ya kuhamia Dodoma.
..........................
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika
hafla maalumu ya kuwakaribisha viongozi wa Serikali itakayofanyika Machi 5
mwaka huu mkoani Dodoma.
Hafla hiyo imeandaliwa na Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma na
itafanyika mkoani humo katika viwanja vya Nyerere (Nyerere Square) kuanzia saa
8 kamili mchana.
Afisa Habari wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Jeremia Mwakyoma ameyasema
hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
maandalizi ya ujio wa viongozi hao katika Mkoa huo.
Mwakyoma amesema viongozi wa Serikali kuhamia katika Makao Makuu ya Nchi
ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano hivyo Mkoa
utawakaribisha rasmi Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu
Wakuu wa Wizara waliohamia kutoka Jijini Dar es Salaam.
“Tukio la viongozi wa Wizara kuhamia Makao Makuu Dodoma ni la kihistoria
ndio maana uongozi wa Serikali ya Mkoa umeona ni vema kuweka utaratibu rasmi wa
kuwakaribisha viongozi hao,”alisema Mwakyoma.
Afisa Habari Mwakyoma amewakaribisha wananchi wote wa Mkoa huo pamoja na
Mikoa ya jirani kuhudhuria kwa wingi kwenye hafla hiyo.
Mnamo Julai 25 mwaka 2016 katika maadhimisho ya siku ya mashujaa
yalioadhimishwa mkoani Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt,
John Pombe Magufuli alitangaza rasmi Serikali kuanza mchakato wa kuhamia Dodoma
ambapo ndipo yalipo Makao Makuu ya Nchi.
No comments:
Post a Comment