Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison George
Mwakyembe na aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape
Moses Nnauye wakikabidhiana hati za makabidhiano rasmi ya
Ofisi yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mjini Dodoma.
.........................
Aliyekuwa Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye leo amekabidhi rasmi ofisi kwa Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo.
Katika makabidhiano hayo yaliyohudhuriwa na
watendaji wakuu wa Wizara, Mhe. Mwakyembe ameahidi kuwa licha ya kukabidhiwa
ofisi, anaamini kuwa Mhe. Nnauye bado ni mdau mkubwa wa sekta za Wizara
na kuwa anategemea kuendelea kupata ushirikiano kutoka kwake.
Aidha Waziri Mwakyembe ameahidi kuendeleza
yote mazuri yaliyo anzishwa na Mhe. Nnauye katika kuimarisha ufanisi wa Wizara
na kuhakikisha inakuwa ni moja ya Wizara za mifano nchini. Amesisitiza kuwa
katika kipindi kifupi alichokaa Wizarani, Mhe. Nnauye alianzisha mabadiliko
makubwa na watu wameanza kuifahamu vizuri Wizara.
Kwa upande wake Mhe. Nnauye amemshukuru Rais
John Pombe Magufuli kwa kumuamini na kumpa dhamana kubwa ya kusimamia Wizara
kwa kipindi cha miezi 15 huku akiwa ndio kwanza amekuwa mbunge katika awamu
yake ya kwanza.Aidha Mhe. Nnauye ameahidi kuendela kushirikiana na Wizara kwa
ukaribu kwani ni kweli yeye ni mdau mkubwa wa sekta za wizara hii.
“Heshima aliyonipa Mhe. Rais ni kubwa mno na
nitaendelea kumuunga mkono katika dhamira yake njema ya kuleta mageuzi nchini,”
alisema Mhe. Nnauye. Aidha alisisitiza kuwa, tofauti na maneno ya mitandaoni,
yeye atabaki kuwa mtiifu kwa Rais, Serikali na chama chake.
Pia amewashukuru watendaji wote wa Wizara kwa
kumpa ushirikiano wa kutosha kwa kipindi chote alichofanya nao kazi na kuwaomba
kutoa ushirikiano huo huo kwa Waziri wa sasa Mhe. Mwakyembe.
No comments:
Post a Comment