Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi
akisalimiana na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Umoja wa
Falme za kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan,Abu Dhabi,Umoja wa Falme
za Kiarabu. June 30,2019.
Tanzania na Nchi ya Falme za Kiarabu
zimekubaliana kuendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi ikiwa
ni pamoja na kushirikiana katika masuala ya usalama wa eneo la Ghuba na bahari
ya Hindi pia kusaidia kuimarisha hali ya usalama katika nchi za Somalia na
Sudan.
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi
akiwa katika mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya
Umoja wa Falme za kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan,Abu Dhabi,Umoja
wa Falme za Kiarabu. June 30,2019.
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John
Kabudi,akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Wizara ya Mambo
ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abu Dhabi. June 30,2019.
........................................
Tanzania na Nchi ya Falme za Kiarabu zimekubaliana
kuendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi ikiwa ni pamoja na
kushirikiana katika masuala ya usalama wa eneo la Ghuba na bahari ya Hindi pia
kusaidia kuimarisha hali ya usalama katika nchi za Somalia na Sudan.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Waziri wa mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi
alipomtembelea na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Umoja
wa Falme za kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan.
Katika Mazungumzo hayo wawili hao wamekubaliana
kuendelea kuimarisha udugu wa muda mrefu baina ya mataifa hayo mawili ikiwa ni
pamoja na kufufua mazungumzo ya Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPC)
ambayo kwa mara ya mwisho yalifanyika katika Mji wa Abu Dhabikatika Umoja wa
Falme za Kiarabu ili kufufua na kutekeleza makubaliano ikiwa ni pamoja na
kuangalia fursa za kiuchumi kwa faida ya pande zote mbili.
Akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo Waziri
Palamgamba John Kabudi amesema pamoja na masuala mbalimbali waliyokubaliana pia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Umoja wa Falme za kiarabu Sheikh Abdullah
bin Zayed Al Nahyan ameahidi kufanya mazungumzo na Ubalozi wa Falme za Kiarabu
uliopo Nchini Tanzania ili kuharakisha matayarisho ya Ubalozi huo kuhamia
Dodoma baada ya serikali ya Tanzania kuupatia ubalozi huo eneo la kujenga
ubalozi wa Nchi hiyo mjini Dodoma bure.
Waziri Kabudi ameongeza kuwa mazungumzo hayo
yamekuwa ya manufaa kwa pande zote mbili na kwamba yataendelea kuimarisha
mahusiano baina ya Nchi hizo mbili ikiwa ni pamoja na kufungua fursa za
kibiashara kwa ajili ya maendeleo ya mataifa hayo.
Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi akizungumza wakati
akihitimisha ziara yake Nchini China,amesema ziara hiyo imekuwa ya manufaa
kiuchumi kwa Tanzania ambapo tayari wawekezaji takribani 150 wanatarajiwa
kuwasili nchini Tanzania kwa nia ya kuangalia maeneo mbalimbali ya uwekezaji
mapema mwezi septemba wakitanguliwa na ujumbe wa watu 10 mwezi Julai 2019,hii
ikiwa ni kipindi kifupi sana mara baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhudhuria mkutano wa kwanza wa maonesho ya
uchumi na biashara kati ya China na Afrika uliofanyika katika mji wa Chanshang
katika jimbo la Hunan,Nchini China.
Aidha ametanabaisha kuwa tayari wamepatikana
wawekezaji wanaotaka kujenga nyumba ya kulala wageni yenye vyumba mia tatu
katika mji wa Karatu ulioko mkoani Manyara kwa nia ya kuhamasisha watalii
hususani kutoka China ambao wanatarajiwa kuongezeka maradufu kufuatia hatua ya
Tanzania kuweka msisitizo katika kutangaza vivutio vyake vya Utalii.
Pia Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Beijing
kimekubali ombi la Waziri Kabudi la kutaka kuongeza idadi ya wanafunzi
watakaokwenda kusoma chuoni hapo kutoka 20 hadi kufikia idadi 40 nafasi
zitakazotolewa kwa ufadhili wa chuo hicho kila mwaka ili kuandaa nguvu kazi ya
kutosha wakati Tanzania ikijiandaa kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025.