Mwenyekiti
wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Nemes Temba (katikati)
akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea
maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelewa juu ya ualbino mapema hii leo jijini
Dar es Salaam, kulia ni Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Dar es Salaam
Bw.Gabriel Aluga na kushoto ni Afisa Mawasiliano na Habari wa chama hicho Bw.
Josephat Torner.
Afisa
Mawasiliano na Habari wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) Bw.
Josephat Torner (katikati) akifafanua jambokwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) wakati akielezea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelewa juu ya
ualbino mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwenyekiti wa chama hicho
Taifa Bw. Nemes Temba na kushoto Mwekahazina wa chama hicho Bw. Abdulah Omar.
Baadhi
ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye
Ualbino Tanzania (TAS) Bw. Nemes Temba (mwenye koto jeusi) wakati akielezea
maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu wa ngozi mapema hii leo jijini Dar es
Salaam.
........................
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim
Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya kimataifa
ya uelewa juu ya ualbino yatakayofanyika Juni 13 mwaka huu katika uwanja
wa Jamhuri mjini Dodoma.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chama cha
watu wenye Ualbino Tanzania Nemes Colman Temba alipokutana na waandishi wa
habari.
Temba alisema maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuibua mijadala na
tafakuri kwa wadau juu ya ukusanyaji endelevu wa takwimu,uchambuzi na
upatikanaji wa watu wenye Ualbino kwa wakati ili Serikali iweze
kuwasajili, kuwahudumia na kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi
wanakuwa salama.
“Bila ya utaratibu mzuri wa upatikanaji wa Takwimu Serikali haitaweza
kupanga vyema juu ya ustawi wa watu wenye ualbino, hivyo maadhimisho ya mwaka
huu yataibua mjadala wa umuhimu wa upatikanaji wa takwimu sahihi kutoka ofisi
ya Taifa ya takwimu kwaajili ya kusaidia katika mipango ya maendeleo ya watu
wenye ualbino”,alisema Temba.
Aidha alisema Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika sensa ya watu na
makazi ya mwaka 2012 iliyojumuisha takwimu za watu wenye ualbino ilisaidia
kubaini idadi ya watu hao ambapo walikuwa 16,376 wakiwemo Wanaume 7,620 na
Wanawake 8,756.
Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Mh.Dkt.
John Pombe Magufuli kwa kusikiliza na kutekeleza ombi la masuala ya
watu wenye ulemavu kuhamishiwa ofisi ya Waziri Mkuu kwani lilikuwa ombi la muda
mrefu kwaajili ya ustawi wa watu wenye ualbino na wenye ulemavu kwa ujumla.
Kwa upande wake afisa habari na uhusiano wa wa chama hicho, Josephat Torner
alisema kuwa, mauaji dhidi ya watu wenye ualbino yamepungua kwa kiasi kikbwa
kulingana na hapo awali na mapambano dhidi ya vitendo hivyo bado
yanaendelea licha ya ukimya uliokuwepo kwa sasa.
Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu Takwimu na Tafiti kwa Ustawi wa Watu Wenye Ualbino yatahudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo
wadau toka Sweden, Uholanzi, Marekani, Canada, Uingereza, Kenya na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo na Mataifa mengine.
Siku hiyo ya kimataifa ya uelewa juu ya Ualbino itatanguliwa na shughuli
mbalimbali ikiwemo hamasa kupitia vyombo vya habari,uendeshaji wa kliniki za
ngozi kwa maalbino pamoja na utoaji wa msaada wa kisheria,midahalo na
makongamano na ukusanyaji wa takwimu za watu wenye ualbino.
No comments:
Post a Comment