Kamanda
wa polisi mkoani Pwani,kamishna msaidizi mwandamizi (SACP) Onesmo Lyanga, wa
kushoto,akizungumza na waandishi wa Habari.
.......................
HALI ya sintofahamu bado inaendelea kutanda wilayani Kibiti ,mkoani Pwani
,baada ya kutokea mauaji mengine ya kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi ,ndani ya
siku sita.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Kibiti ,Juma Njwayo ,alieleza kwamba,mwenyekiti wa
(CCM) tawi la Njia nne ,kijiji cha Muyuyu ,ambae pia ni mjumbe wa kamati ya
siasa kata ya Mtunda ,Iddi Kilungi ,ameuawa kwa kupigwa risasi.
Aidha alisema , mtoto wa marehemu Nurdin Iddi Kilungi ,amenusurika kifo
baada ya kupigwa risasi ya tumbo na kutokea mgongoni.
Njwayo ,alieleza ,majeruhi alikimbizwa hospital ya mission ya Mchukwi
kwa ajili ya matibabu.
Alisema ,tukio hilo limetokea may 17 majira ya saa 1.40 usiku wakati
marehemu akiwa amejipumzisha kimazungumzo nyumbani kwake .
Kaimu huyo ambae pia ni mkuu wa wilaya ya Rufiji, Njwayo,
alibainisha, watu wawili wanaodaiwa kuwa ni wauaji walifika eneo la nyumbani kwa
Kilungi na kumpiga risasi na baadae kumpiga mwanae kisha kutokomea
kusikojulikana.
Alisema watu hao waliegesha pikipiki mbali ya nyumba na baada ya tukio
walitokomea nayo .
Kwa mujibu wa Njwayo, amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Kibiti
kumhamisha majeruhi (Nurdin Kilungi)kwenda hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa
matibabu zaidi .
Alipoulizwa matukio hayo kuhusiana na masuala ya kisiasa alisema hawezi
kulisemea moja kwa moja jambo hilo kwasasa.
“Siwezi kujua kama ndio chanzo ,mambo haya yanaendelea kuchunguzwa na
vyombo vyetu vya kiusalama ,endapo itabainika basi umma utatangaziwa lolote
lililopo lakini sio kuhisi”alisema Njwayo.
Kuhusiana na madai ya askari doria na kikosi maalum kilichopo
Rufiji,Kibiti kutoingia maeneo ya vijijini ambako ndio kuna athari kubwa
,Njwayo,alieleza ,anachojua yeye ni kwamba kuna askari wanaovaa sare na
wasiovaa sare ambao wanafika mijini na vijijini.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Onesmo Lyanga ,alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kudai ni siku sita tangu kutokea kwa mauaji mnamo may 13 mwaka
huu,ambapo katibu wa CCM kata ya Bungu ,Halife Mtulia ,aliuawa kwa kupigwa
risasi na watu wasiojulikana.
Alisema chanzo cha mauaji hayo bado hakijajulikana kwani vyombo vya dola
bado vinafanya upelelezi ili kubaini kiini halisi cha matukio hayo ya mauaji .
Kamanda huyo alisema wanaendelea kuwasaka wahusika wa matukio hayo
yanayoonekana kuhusisha viongozi mbalimbali na askari polisi.
Kamanda Lyanga ,aliwataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa
kufichua wahalifu ambao wapo miongoni mwao pasipo kuogopa .
“Ni wazi kwamba wahalifu wanaofanya mauaji haya wana wenyeji
wanaowakumbatia kwa kuwaficha hivyo yeyote atakaebainika kushirikiana na
makundi ya uhalifu huo atachukuliwa hatua kali za kisheria”alisisitiza kamanda
Lyanga.
No comments:
Post a Comment