Serikali inamkakati wa kuhakikisha inajenga Magereza katika
maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa kilimo ambayo pia yana ukubwa wa kutosha ili
kazi ya kuwarekebisha wafungwa iwe rahisi kufanyika huku shughuli za uzalishaji
zikiwa zinaendelea.
Hayo yamesemwa leo Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya
nchi Mhe. Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu swali la Mhe Devotha Minja Mbunge
wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro.
“Magereza hayo yatajengwa katika maeneo yenye Kilimo na
yatakuwa ni kwa ajili ya watu waliokwisha hukumiwa huku yale Magereza ya
mijini yawe kwa ajili ya mahabusu tu ili wawe karibu na Mahakama,”alisema
Mwigulu.
Aliongeza kuwa mkakati huo wa Serikali ni wa muda mrefu na
wanahitaji kufanya hivyo ili kurahisisha shughuli za maendeleo zinazofanywa na
wafungwa na pia kupunguza msongamano wa wafungwa katika Magereza.
Hili pia
linatokana na tamko la Mh.Rais Dkt John Pombe Magufuli alilowahi kulitoa hivi
karibuni kuwa wafungwa wako katika kutumikia adhabu hivyo wanatakiwa kufanya
kazi hasa za kilimo ili kwanza kujipatia chakula na sio kukaa tu bure na
kusubiri kila kitu wafanyiwe na serikali.
Aliongeza kuwa Serikali ina mkakati wa kutumia bajeti inayotengwa na
nguvu kazi wanayoipata kutoka kwa wataaalam walionao kwa upande wa askari
Magereza na wafungwa ili kukarabati Magereza chakavu na kujenga nyumba za
askari.
Aidha alibainisha kuwa suala la kukatwa kwa umeme katika Magereza, nyumba
za askari,pamoja na maeneo na maeneo mengine ya kambi za Jeshi la Polisi
na Magereza limeshafanyiwa kazi na serikali kwa kupitia hazina
imekwishatoa fedha kwa ajili ya kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Waziri aliliambia Bunge kuwa sheria zimeainisha baadhi ya haki
za mfungwa zikiwemo huduma za afya kwa wakati,kupewa chakula, uhuru wa
kutembelewa na ndugu zake na kupata mawasiliano kwa kusoma magazeti,kusikiliza
taarifa za habari na kuandikiwa barua na ndugu zao,haki ya kukata rufaa ikiwa
hakuridhika na hukumu yake, malazi safi na yakutosha pamoja na kushiriki
michezo mabalimbali.
No comments:
Post a Comment