Sunday, May 7, 2017

RC. PWANI AHIMIZA ZAO LA KOROSHO KISARAWE.

KOR2
MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, ameitaka wilaya ya Kisarawe kufufua zao la biashara kama ilivyokuwa miaka ya 1995 ambapo wilaya hiyo ilikuwa ikisifika kwa kulima zao hilo.

Aidha amepiga marufuku kang’omba kwani inasababisha hasara kwa wakulima wa korosho badala yake utumike mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mhandisi Ndikilo,pia ameonya wizi unaofanywa na baadhi ya vyama vya ushirika vya msingi vya korosho,(AMCOS) kwa wanunuzi .

“Ambapo katika msimu uliopita sh. mil. 385 zilipotea katika wilaya ya Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Bagamoyo na kati ya fedha hiyo mil. 4.633 ziliibiwa na AMCOS za Kisarawe”alibainisha .

Aliyasema hayo baada ya kutembelea shamba la korosho na mihogo la mzee George Haule huko Sungwi.

Mhandisi Ndikilo, alieleza kwamba, zao la korosho liwe ni azimio la baraza la madiwani wilayani humo.

Alisema kwa kulima korosho kwa wingi kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuwaondolea umaskini.

Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa,endapo mkulima akipanda miche 100 kwa miaka mitatu anapata tani 4 sawa na mil. 16 .

“Ndani ya miaka mitatu ni lazima utajirike, tuibue Kilimo hiki kwani kinatija kwa wilaya na mtu mmoja mmoja “alisema mhandisi Ndikilo.

Akizungumzia ubadhilifu unaofanywa na baadhi ya AMCOS  alisema kati ya mil. 385 wilaya ya Kisarawe ni mil. 4.633 na kati ya hizo Amcos ya Maneromango ni mil. 3.72 na ya Mzenga ni laki 4.64 .

Aliwaasa kuacha tabia ya wizi kwa wanunuzi na kuhujumu zao hilo la biashara.

Mhandisi Ndikilo,alisema vyama vilivyojihusisha kutapeli wanunuzi vitoe sababu za msingi kwa wakuu wa wilaya kueleza ubadhilifu huo na wakibainika kufanya wizi vyombo vya sheria vifanyekazi yake.

Katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji, Shangwe Twamala alisema, wataalamu kutoka bodi ya korosho ndio wana hakiki ubora wa korosho katika vyama vyote vya msingi vilivyokusanya korosho kwa kushirikiana na CORECU na kisha kuandaa muongozo kwa wanunuzi.

Alisema muongozo wa mauzo namba 1 wa mwaka 2015,kifungu namba 4.4 wa bodi ya korosho Tanzania  kinasema mnunuzi ataruhusiwa kuhakiki ubora wa korosho zilizopo kwenye ghala baada ya kufanya utaratibu wa kulipa korosho .

Twamala alisema sababu zinazotolewa na vyama hivyo kuwa ni unyaufu na sio upotevu alisema ni visingizio. 

Nae mtaalamu wa zao la mikoroshi wilayani Kisarawe, Ayubu Isele, alisema kwasasa wanayo miche 35,000 ambayo inasambazwa bure kwa wakulima wilaya nzima.

Alisema zao la Korosho miaka ya 1995-1996 katika wilaya hiyo lilishamiri na wakulima kunufaika.

Mkulima wa zao la korosho mzee Haule, alisema alianza Kilimo hicho mwaka 2005 ,na miche 662 na sasa ameongeza miche 342 .
Alisema zao hilo ndio ajira yake na linamuingizia kipato kwa kiasi kikubwa.

No comments:

Post a Comment