Monday, May 15, 2017

TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA

PICHA-RPC-MBEYA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.

KUINGIA NCHINI BILA KIBALI [WAHAMIAJI HARAMU]

Mnamo tarehe 13.05.2017 majira ya saa 21:30 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko katika Kijiji cha Itope kilichopo Kata ya Kyela kati, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye amefahamika kwa jina la BROWN ENOS [25] Dereva na Mkazi wa Ilomba Jijini Mbeya akiwa anaendesha gari yenye namba za usajili T.196 CTO Toyota Coater akisafirisha wanamiaji haramu 47 wote raia wa Nchini Somalia.

Mtuhumiwa amekamatwa na mara baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani. Aidha taratibu za kuwakabidhi wahamiaji hao idara ya uhamiaji kwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea.

KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI [GONGO]
Mnamo tarehe 13.05.2017 majira ya saa 16:00 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko katika Kijiji cha Mahenge kilichopo Kata ya Makwale, Tarafa ya Ntebela, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye amefahamika kwa jina la THOMAS MWAKANYAMALE [40] Mkazi wa Mahenge akiwa na Pombe Moshi ujazo wa lita 50.

Mtuhumiwa alikamatwa akiwa na Pombe hiyo baada ya kufanya upekuzi katika kibanda chake ambacho hufanyia biashara ya kuuza mafuta ya Petrol na ndipo yalikutwa madumu mawili na nusu yakiwa na pombe hiyo haramu. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

KUPATIKANA NA NOTI BANDIA [DOLA ZA MAREKANI]

Mnamo tarehe 13.05.2017 majira ya saa 10:00 Asubuhi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako katika Kitongoji cha Mapelele kilichopo Kata ya Mtengule Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya. Na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 03 ambao ni:-
1.   NOBAT MUSHI [23]
2.   TAKESHI NUNDO [27]
3.   HEMED MSANGI [26] Wote wakazi wa Forest

Watuhumiwa kwa pamoja walikamatwa wakiwa na dola bandia noti 390 kila moja ikiwa na thamani ya dola 100, kama dola hizo zingekuwa halali zingelikuwa na thamani ya dola 39,000. Watuhumiwa walikamatwa na fedha hizo ambazo walikuwa wamezihifadhi kwenye mkoba na kuziweka ndani ya gari yenye namba za usajili T.715 aina ya Altezza.

Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo Kumekuwa na tukio 01 la mauaji kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 13.05.2017 majira ya saa 15:19 Alasiri huko Kijiji cha Ihahi, kilichopo Kata na Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la MICHAEL WILLIAM @ MPONZI [35] Mkazi wa Ihahi aliuawa kwa kuchomwa kitu chenye ncha kali upande wa kulia wa tumbo na kusababisha utumbo kutoka nje na mtu/watu wasiofahamika.

Chanzo cha mauaji hayo bado akijafahamika. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi. Upelelezi zaidi unaendelea ikiwa ni pamoja na msako wa kuwabaini waliohusika katika tukio hili.

WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuacha kutumia Pombe haramu ya Moshi kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya ya mtumiaji. Pia anatoa wito kwa wananchi kuachana na biashara haramu ya noti bandia au usafirishaji haramu wa binadamu. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za mtu/watu waliohusika katika tukio la mauaji huko Wilaya ya Mbarali ili watuhumiwa wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Imetolewa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA

No comments:

Post a Comment