Mkutano mkuu wa mwaka wa Shirikisho la wakuu wa Polisi kwa nchi za
Kusini mwa Afrika (SARPCCO) unatarajia kufanyika Mei 24, 2017 mkoani Arusha
chini ya mwenyekiti wa Shirikisho hilo kipindi hiki ambaye ni Mkuu wa Jeshi la
Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu.
Mkutano huo utatanguliwa na mikutano ya kamati tendaji za SARPCCO kabla
ya kufunguliwa rasmi Mei 24, 2017 na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba ambapo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo
jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya Operesheni za
pamoja katika kubaini na kukabiliana na makosa mbalimbali yakiwemo
dawa za kulevya, wizi wa magari, usafirishaji haramu wa binadamu na ugaidi.
Vilevile, mkutano huo utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na
Wakuu wa Upelelezi wa SARPCCO pamoja na kamati tendaji za sheria, Mafunzo na
kamati tendaji ya Jinsia na watoto katika mkutano wao uliofanyika mwezi Machi
mjini Bagamoyo.
Aidha suala la michezo baina ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama nalo
linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo.
SARPCCO iliundwa mwaka 1995 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa
Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika katika kukabiliana na vitendo
vya uhalifu.
Shirikisho hilo linaundwa na Nchi kumi na tano ambazo ni Tanzania,
Angola, Botswana, Malawi, Lesoto, Mauritius, DRC, Msumbiji, Namibia, Afrika
Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland, Madagascar na Syshelis.
Imetolewa na:-
Advera Bulimba-ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
No comments:
Post a Comment