Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Muombwa, akimkaribisha
Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii, Bw. Eliabi Chodota
kutoa mada kwenye semina ya mtangamano inayoendelea Kisiwani Pemba. Ushiriki na
mwitikio katika semina hiyo umekuwa mkubwa kwa washiriki ambapo wameonekana
kuvutiwa sana na semina hii pia wamekuwa wadadisi wazuri wa kutaka kujua zaidi
fursa zinazo patikana kwenye mtangamano huo.
Bw. Chodota akitoa
mada kwenye semina ya mtangamano inayoendelea Pemba.
Sehemu ya washiriki
wakisikiliza kwa makini mada iliyokuwa ikitolewa na Bw. Chodota (hayupo
pichani).
Bw. Chodota akiendelea
kutoa mada yake.
Mmoja wa washiriki Bi.
Kauthari akiuliza swali mara baada ya mada kumalizika kutolewa na Bw. Chodota
hayupo pichani.
Washiriki wakisikiliza
kwa makini mada na maswali yaliyo kuwa yakiulizwa na washiriki wengine.
Mhe. Mbarouk Salim Ali
Mbunge wa Jimbo la Wete akiuliza swali kwenye semina. Pembeni yake ni Mbunge wa
Jimbo la Konga, Mhe. Mbarouk Ali akisikiliza kwa makini.
Meneja wa TRA kwa
upande wa Kisiwani Pemba Bw. Habibu Saleh naye akiuliza swali kwa mtoa mada,
Bw. Suleimani (hayupo pichani).
TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Zanzibar haibaguliwi katika EAC,
Serikali ya Zanzibar inashiriki moja kwa moja bila ukomo katika masuala
yote ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hivyo Wazanzibari
wamehimizwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye Jumuiya hiyo na kuondokana na
dhana kuwa eti, Serikali yao inabaguliwa.
Akiwasilisha mada leo kuhusu ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwenye semina ya masuala ya mtangamano wa EAC inayofanyika
Pemba, Afisa wa Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Bw. Suleima Haji alitoa ufafanuzi wa kina kuonesha namna
Zanzibar inavyoshiriki katika EAC.
Bw. Haji alieleza kuwa licha ya Zanzibar kuwa sehemu ya muungano
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ushiriki wake umedhihirika katika mgawanyo
wa miradi ya maendeleo ya EAC, hususan miradi ya Miundombinu. Alisema
Zanzibar iliwasilisha mapendekezo ya miradi 10 kwenye Sekretarieti ya EAC na
kutokana na vipaumbe vilivyowekwa miradi 3 imekubaliwa na mchakato wa
kuitekeleza unaendelea. Miradi hiyo ni ujenzi wa Bandari ya Marhubi
kisiwani Pemba, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na ununuzi wa meli kubwa
zitakazosafirisha abiria na mizigo kwenye nchi wanachama wa EAC.
Aidha, kwenye miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Zanzibar haijasahaulika. Zanzibar inanufaika na
miradi inayofadhiliwa na taasisi inayojihusisha na masuala ya kukuza biashara
na kupunguza umasikini katika nchi za EAC inayoitwa "East Africa
Trademark" (TMEA). TMEA ambayo ni mdau mkubwa wa EAC inafadhili
mradi ambao unawawezesha Wazanzibari kufanya maombi kwa njia ya mtandao ili
kupata cheti cha uasili wa bidhaa. Cheti hicho ni muhimu kwa wafanyabiashara
kwani kinatambulisha bidhaa yako ilipotengenezwa na kupata msamaha wa kodi ya
forodha inapoingia nchi nyingine za EAC.
Mradi mwingine unaofadhiliwa na TMEA huko Zanzibar ni ule wa kuwasilisha
malamiko kwa njia ya mtandao au ujumbe mfupi wa simu pale inapotokea
mfanyabiashara amekumbana na vikwazo visivyo vya forodha katika kusafirisha
bidhaa zake ndani ya Jumuiya. Ujumbe huo utakapopokelewa, kikwazo
kilicholalamikiwa kitafanyiwa kazi na taasisi husika mara moja.
Benki ya dunia pia inaendesha mradi wa kutathmini utekelezaji wa Soko la
Pamoja kwa upande wa Zanzibar. Kama inavyotambulika soko la pamoja lina
vipengele vingi vikiwemo; usafirishaji huru wa bidhaa, huduma, mtaji na watu.
Hivyo kuna umuhimu wa kupima namna nchi wanachama zinavyotekeleza vipengele
hivyo.
Ushiriki wa Zanzibar unapatikana pia kwenye uenyeji wa taasisi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Zanzibar imebahatika kuwa mwenyeji wa Kamisheni ya
Kiswahili ya EAC. Kuwa mwenyeji wa taasisi kuna faida kubwa zikiwemo
kujitangaza na ajira. Kwa upande wa ajira, Bw. Haji alisema sio tu Wazanzibari
wanafaidikia na ajira za Kamisheni ya Kiswahili, bali wanapata ajira hata
katika Sekretarieti ya EAC na kutolea mfano kuwa Mhasibu Mkuu wa kwanza wa
Sekretarieti hiyo alikuwa Mzanzibari.
Vile vile, Zanzibar imekuwa mwenyeji wa vikao mbalimbali vya taasisi za
Jumuiya. Mwaka 2010 Mahakama ya Afrika Mashariki ilifanya kikao chake Zanzibar,
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) lilifanya kikao chake Zanzibar
mwaka 2016 na mwezi Agosti mwaka huu utafanyika mkutano mkubwa wa masuala ya
Kiswahili mjini Zanzibar. Aliendelea kusema kuwa katika Bunge la EALA la
kipindi hiki, Zanzibar ina wabunge watatu, wawili wakitokea CCM na mmoja
CUF.
Alihitimisha mada yake kwa kuwasihi Wazanzibari waache fikra potofu za
kujihisi kubaguliwa badala yake waunganishe nguvu kuchangamkia fursa lukuki za
kibiashara zilizopo kwenye mtangamano wa EAC. Alisema Serikali ya Zanzibar
inashiriki katika kila jambo ikiwemo kushiriki mikutano ya Marais. Mawaziri na
Wataalamu ili kutetea maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam,
18
Mei, 2017
No comments:
Post a Comment