Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani akitoa
elimu ya mpiga kura kupitia redio A FM ya mkoani Dodoma leo Mei 9 mwaka huu
huku akifuatiliwa kwa makini na watangazaji wa redio hiyo.
...................................
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa wito kwa wananchi walioko kwenye
halmashauri mbalimbali nchini, kuitumia vyema fursa ya utoaji wa elimu ya mpiga
kura kupitia redio za kijamii kwenye halmashauri zao ili kuondoa manung’uniko
kwenye chaguzi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. Kailima
Ramadhani wakati akizungumzia mpango wa kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima
ulioanza kutekelezwa Mei 8 mwaka huu hii katika mikoa kumi nchini.
Alisema kupitia mpango huo wananchi wanaosikiliza redio za kijamii kwenye
halmashauri nchini, watapata fursa ya kujifunza elimu ya mpiga kura na kuelewa
masuala yote muhimu yanayohusu mfumo mzima wa kupiga kura.
“Tumepanga mpango, Tume itasambaa nchi nzima kuzungumzia elimu ya mpiga
kura kwenye redio za kijamii zilizoko kwenye halmashauri zote za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.” alisema Bw. Kailima.
Alisisitiza kwa kutoa wito kwa wananchi walioko maeneo ambayo Tume
itakwenda kutoa elimu ya mpiga kura, wasikilize na kuuliza maswali ili waweze
kuelewa.
“Hii ni fursa kwa wananchi ambayo muda mrefu hawajawahi kuipata,
hivyo nawaomba wafuatilie ili waweze kuelimika zaidi ili yale manung’uniko ya
kura yatakuwa yamekwisha na tutakuwa na uchaguzi mzuri zaidi ya ile ambayo
tumeifanya.” Alifafanua Bw. Kailima.
Utekelezaji wa mpango huo umegawanyika katika makundi matatu ambapo kundi
la kwanza limeanza kutoa elimu hiyo elimu hiyo kwenye mikoa ya Kagera,Mwanza,
Kilimanjaro, Morogoro, Mbeya na Dodoma.
Mikoa mingine itakayojumuishwa kwenye kundi hilo ni Ruvuma, Mara, Pwani
na Mtwara ambapo elimu hiyo itatolewa kuanzia tarehe 8 Mei hadi tarehe 20 Mei
mwaka 2017.
Kundi la pili linatarajiwa kutoa elimu hiyo kuanzia tarehe 24 Mei hadi
tarehe 7 Juni mwaka huu katika mikoa ya Geita, Tanga, Singida, Shinyanga,
Lindi, Arusha, Tabora, Kigoma, Iringa, Manyara, Rukwa, Katavi, Songwe, Njombe
na Simiyu.
Bw. Kailima alisema kuwa utoaji wa elimu hiyo utajikita kwenye mada kuu
ya Elimu ya Mpiga Kura iliyogawanywa kwenye vipindi vitano, itakaytoolewa
kwenye redio hizo kulingana mada husika na wananchi kuuliza maswali na kujibiwa
na wawasilishaji wa mada hizo kutoka Tume.
“Ni mada ambayo imejumuisha masuala yote muhumu yatakayofanya mpiga kura
yeyote au mdau yeyote wa uchaguzi kuisoma au kuisikiliza na akaelewa mfumo
mzima wa masuala ya kupiga kura” alisema.
Mbali na kutoa elimu ya mpiga kura kupitia vituo vya redio za kijamii
katika halmashauri nchi nzima, Tume pia inatoa elimu hiyo kwa njia ya magazeti
na vyombo vingine vya habari na mitandao ya kijamii, kushiriki kwenye
mikutano na maonesho mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment