Friday, May 12, 2017

MAADHIMISHO YA WIKI YA ELIMU MKOA WA PWANI

unnamed
Baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye maandamano katika siku ya kilele cha wiki ya elimu mkoani Pwani,yaliyofanyika wilayani Mkuranga.
 A

Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,akizungumza katika kilele cha wiki ya elimu kimkoa iliyofanyika Mkuranga.
............................


Na Mwamvua Mwinyi,
Pwani

IDARA ya elimu mkoani Pwani,imeweka wazi kwamba mkoa huo unakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa 3,973 hali inayosababisha baadhi ya shule ,wanafunzi kulundikana hadi 200 kwenye darasa moja.

Aidha kutokana na uhaba huo baadhi ya shule zimekuwa zikifundisha wanafunzi wake wakiwa chini ya miti .

Hayo yalielezwa na afisa elimu mkoani Pwani, Germana Sendoka ambae pia ni katibu tawala msaidizi elimu mkoani hapo,wakati akitoa taarifa ya hali ya kitaaluma na changamoto zinazowakabili kimkoa,katika kilele cha wiki ya elimu yaliyofanyika wilaya ya Mkuranga.

Alisema mkoa huo una jumla ya vyumba vya madarasa 3,003 huku mahitaji ya vyumba hivyo ikiwa ni  6,976 ili kuweza kukidhi mahitaji.

Germana alifafanua kuwa upungufu wa nyumba za walimu ni 4,811 mahitaji nyumba 6,609 zilizopo ni 1,798 pekee.

Alieleza ,upungufu wa nyumba za walimu unapunguza molari ya kazi ya kufundisha hasa shule za vijijini ambapo hakuna nyumba za kupanga.

Akizungumzia tatizo la matunda ya vyoo alisema,mahitaji ya matundu hayo kwa ajili ya wanafunzi wasichana ni 6,969 , yaliyopo 3,026 na upungufu matundu 3,943 kwa wavulana mahitaji ni 7,024 wakati yaliyopo  ni 2,810 kijumla upungufu ni matundu ya vyoo 4,214.

Changamoto nyingine ni kuwepo kwa mlundikano wa wanafunzi kwenye chumba kimoja cha darasa na baadhi yao kusomea chini ya miti.

“Shule kuwa mbali wanafunzi hutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule jambo ambalo linasababisha utoro na upungufu wa walimu waliopata mafunzo ya ufundishaji wa KKK”alisema Germana.

Germana alizitaka halmashauri zitenge fedha kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na jamii ihimizwe kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Nae mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo alisema pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuongeza miundombinu ya shule lakini bado miundombinu hairidhishi.

Alielezea wanahitaji mkoa na halmashauri zake ,wazazi na walezi,wadau ujipange kupunguza ama kuondoa changamoto hizo kila moja katika eneo lake.

Mhandisi Ndikilo alikemea,uwepo wa tafsiri potofu ya dhana ya elimu bila malipo kwani ni miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma ufanisi wa kiutendaji katika sekta ya elimu kimkoa.

Alieleza kutokana na tafsiri hiyo wazazi na wanajamii walio wengi wanaona hawana wajibu wa kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu mashuleni wakiamini ni jukumu la serikali pekee.

Alisema tafsiri hiyo sio sahihi na ni kikwazo cha kutekeleza dhamira ya elimu bila malipo kwenye maeneo mbalimbali.

“Waraka wa elimu bila malipo namba.6 wa mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa elimu bila malipo umebainisha wazi majukumu ya kila mdau wa elimu akiwemo mdau ,mzazi,walimu,kamani/bodi za shule na jamii namna ya kushiriki kutekeleza hilo”alisema.

Mhandisi Ndikilo alibainisha,baadhi ya majukumu ambayo wazazi na jamii inapaswa kutekeleza katika wakara huo ni kuhamasisha kuwaandikisha watoto wao shule.

Pia,kushiriki katika shughuli zote za kuleta maendeleo ya kielimu na kuendelea kujitolea nguvu na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko kwenye jamii husika.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa rai kwa walimu ambao hawatekelezi majukumu yao ipasavyo kwa kushindwa kufundisha  ipasavyo kwasababu za utoro na kuchelewa kazini kuacha tabia hizo mara moja.

Kwa mujibu wa mhandisi Ndikilo,ukiukwaji wa maadili ya taaluma ya ualimu ni changamoto nyingine ambayo inasababisha baadhi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kumaliza wakiwa hawajui kusoma,kuandika wala kuhesabu(KKK).

Mkoa wa Pwani ulianza maadhimisho ya juma la elima may 4 mwaka huu katika halmashauri ya mji wa Kibaha na kilele kimkoa kimefanyika wilayani mkuranga.
 A 2

Afisa elimu mkoani Pwani,Germana Sendoka akitoa taarifa fupi ya taaluma kimkoa katika kilele cha wiki ya elimu mkoani humo yaliyofanyika wilayani Mkuranga.(picha na Mwamvua Mwinyi) .
 A 1

Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akionyesha tuzo aliyopatiwa na idara ya elimu mkoanu humo ya kumpongeza kwa ushirikiano wake na idara hiyo na kupambana na adui ujinga mkoani humo.

No comments:

Post a Comment