Serikali imetangaza kuendesha operesheni ya kuteketeza mashamba ya
mirungi kote nchini ikiwa ni mkakati wa kupambana na dawa za kulevya.
Hatua hiyo inafuata baada ya kuteketeza mashamba ya bangi zaidi ya 150
yenye ukubwa wa ekari 165 katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers Sianga wakati akizungumza kwenye
kipindi maalum kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV.
“Dawa za kulevya zinaathiri sana nguvu kazi ya Taifa na tangu Mamlaka hii
imeanza tumefanikiwa kudhibiti uingizaji wa Heroine, Cocaine na dawa nyingine
za kulevya na tumewakamata wafanyabiashara wakubwa ambao walikuwa wanatafutwa
na mataifa makubwa na hiyo ni hatua kubwa kwa nchi yetu katika mapambano haya”
Alisisitiza Sianga.
Akifafanua Sianga alisema kuwa Serikali imepanga kuongeza vituo vya
kuhudumia waathirika wa dawa za kulevya katika Mikoa ya Mbeya, Dodoma na Mwanza
kwa awamu ya kwanza kutokana na mafanikio yaliyofikiwa katika kudhibiti
uingizwaji wa dawa za kulevya na matumizi yake.
Mikoa mingine itakayofuata katika mpango wa kuanzishwa kwa vituo hivyo ni
Pwani, Morogoro, Kilimanjaro na Arusha.
“Tumejipanga kudhibiti maeneo yote yanayotumika kupitisha dawa za kulevya
katika hili tunaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ili
dhamira ya Serikali ya kuondoa tatizo la dawa za kulevya hapa nchini
litimie.”Alisisitiza Sianga.
Akizungumzia ushirikiano na wananchi Sianga alisema kuwa kila siku
wananchi 5 hadi 10 wanafika katika Mamlaka hiyo kutoa taarifa hali inayoonyesha
mwamko kwa wananchi katika kupambana na dawa za kulevya katika maeneo yao na
katika Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Sianga alibainisha kuwa wameanza kufuatilia
Kemikali Bashirifu zinazoingizwa hapa nchini kwa kuwa zinaweza kutumika vibaya
na watu wenye nia mbaya kuzalisha dawa za kulevya.
“Kemikali Bashirifu zinaweza kutumika vibaya kuzalisha dawa za kulevya
hivyo lazima tuzifuatilie na kudhibiti uingizwaji wake ili uzingatie sheria na
taratibu na zitumike kwa makusudi chanya tu na si vinginevyo.” Alieleza Sianga.
Hivi karibuni Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya
nchini,kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka
ya Chakula na Dawa TFDA,walifanikiwa kukamata shehena kubwa ya kemikali
Bashirifu zinazoweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya katika eneo la Mwenge
Jijini Dar es Salaam.
Aidha katika msako huo pia mfanyabiashara Benedict Assey mmiliki wa
shehena hiyo alibainika kumiliki kiasi kikubwa cha kemikali hizo katika Miji ya
Bagamoyo,na Moshi mkoani Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment