Serikali imeshauriwa kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari ili
waandishi waweze kupata nafasi ya kufichua matatizo yanayoikabili jamii
na kupatiwa ufumbuzi.
Hayo yamesemwa leo huko Park Hyyat Hotel na mwandishi wa habari kutoka
ubalozi wa Marekani nchini Tanzania Kenneth Cooper wakati alipokuwa
akitoa mafunzo kwa wandishi wa habari wa vyombo mbalimbali hapa nchini.
Amesema kuvitisha vyombo vya habari na kuvibinya katika kutekeleza
majukumu yake ni kuvipotezea ufanisi na kupelekea kufanya kazi zake kwa woga na
kushindwa kufichua maovu.
“Serikali ikubali na iheshimu uwepo vyombo vya habari, kwani kuvibinya
nikusababisha matatizo nchini,” alisisitiza Kenneth Cooper.
Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa kwa jamii kwani vinaweza
kuibua matatizo yanayoikabili hivyo kupitia vyombo hivyo yanaweza kufika kwa
wahusika.
Akizungumzia njia bora kwa waandishi kutafuta na kuripoti habari,
Cooper alisema mwandishi anatakiwa kuwa makini na mdadisi katika utafutaji wa
habari.
Amewaeleza washiriki wa mafunzo kuwa wanapaswa kujenga uhusiano
mzuri na vyanzo vya habari ili waweze kupata habari kwa urahisi
pamoja na kufuatilia mtiririko wa matukio mbalimbali.
Aidha amewahimiza waandishi kufanya utafiti na kutotosheka na chanzo
kimoja cha habari na kuweka umuhimu wa kutoa nafasi sawa kwa watu
watakaohusika katika habari ili kuepuka matatizo.
Hata hivyo amesisitiza waandishi kufanya tathmini na kujua thamani
ya maisha yao ili kuweza kujali usalama wa maisha, kuweka matarajio ya kazi zao
pamoja na kuwa na mashirikiano na waandishi wengine katika kutekeleza majukumu
yao.
Nae Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) Abdalla
Abdulrahman Mfaume ameushukuru Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa
kuwapatia mafunzo hayo jambo ambalo litawajengea uwezo na ameushauri ubalozi
huo kuendelea kushirikiana na waandishi wa Zanzibar kwa mafunzo zaidi.
No comments:
Post a Comment