Mkuu
wa Mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, akiwa ametembelea shamba la mfano la
zao la biashara la korosho lililopo Ruvu JKT, wilayani Kibaha. (picha na
Mwamvua Mwinyi) .
....................................
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist
Ndikilo,amemaliza ziara yake ya kutembelea wilaya sita kimkoa,ambapo amehimiza
mambo makuu manne ikiwemo ulinzi na usalama,uwekezaji,kilimo cha matunda na
korosho.
Aidha amekemea migogoro ya wakulima na wafugaji
ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watu na wengine kujeruhiwa pasipo sababu za
msingi.
Akimaliza ziara yake wilayani Kibaha,mhandisi
Ndikilo,alieleza mkoa wa Pwani una viwanda vitatu vikubwa vya kusindika matunda
kwa sasa ambavyo endapo wakulima watavitumia watanufaika kwa kiasi kikubwa.
Alisema,kiwanda cha Bakhresa ambacho kipo Mwandege
-Mkuranga kimeshaanza kazi na kile cha Elven Agri co.ltd kilichopo kata ya
Mapinga -Bagamoyo huku cha Sayona kinachojengwa kata ya Mboga kikiwa
kwenye hatua za mwisho za ujenzi.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kiwanda cha kusindika
matunda cha Bakhresa kina uwezo wa kusindika tani 350 za matunda kwa siku na
uwekezaji wake umegharimu sh.bil.261.
Mhandisi Ndikilo alisema uwekezaji wa viwanda hivyo
ni mkubwa na utawatengenezea kipato na soko wakulima wa matunda .
“Niwasihi wakulima wa mkoa wa Pwani na mikoa mingine
kulima kwa bidii maembe,nyanya,mananasi,mapeasi,pilipili “
“Sio tu mlime kwa kilimo chetu tulichokizoea ,hapana
kwasasa inabidi twende na mabadiliko ya teknolojia ya kisasa kwa kutumia
mbegu,pembejeo bora na mpalilie na kutumia madawa ili kupata
matunda yatakayouzika”alifafanua.
Hata hivyo mhandisi Ndikilo aliwaomba wawekezaji wa
ndani na nje ya nchi kukimbilia kuwekeza mkoani Pwani kwani unaelekea kuwa
ukanda wa viwanda na uwekezaji.
Alisema kwasasa viwanda vilivyopo ni 200 ambavyo
vipo vikubwa,vidogo na vya kati na mabavyo vimeanza kazi,vinavyoendelea na
mchakato na vingine hatua za mwisho za ujenzi .
Akizungumzia masuala ya ulinzi na usalama ,aliwataka
wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na kuacha kuamini wageni wanaoingia
katika maeneo yao.
“Ukiona kuna mtu yupo kijijini ama kwenye mtaa wako
humjui na unamtilia shaka basi toeni taarifa kwenye vyombo vya dola ili viweze
kumfuatilia”
Hakusita kukemea migogoro ya wakulima na wafugaji
ambayo imekuwa ikigharimu maisha ya watu kwa kujeruhiwa ma kupoteza maisha.
Kwa mujibu wa mhandisi Ndikilo,migogoro hiyo haina
tija miongoni mwao na kusisitiza umoja,upendo na amani katika pande hizo mbili
.
Alisema wamejipanga kuongea na mhimili husika ili
kuuomba kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kutoa hukumu badala ya
kupiga faini.
Mhandisi Ndikilo alisema wafugaji wakitozwa faini
wamekuwa na kiburi na dharau kutokana na kuwa na uwezo wa kulipa hivyo kuanzia
sasa wapigwe kifungo ili kukomesha jeuri yao.
Katika hatua nyingine amewataka wazazi na walezi
kusomesha watoto wao wa kike na wakiume pasipo kuwabagua kwani elimu ni ufunguo
wa maendeleo ya maisha yao ya baadae.
Nae katibu tawala msaidizi uchumi na uzalishaji
mkoani Pwani,Shangwe Twamala alisema ziara hiyo ililenga kutembelea maeneo
yenye uzalishaji wa mazao ya kilimo cha biashara kama kwenye maghala ya korosho
na viwanda vya matunda.
Pia kutembelea mashamba ya wakulima wa mihogo na
kuhimiza kilimo kinachostahimili ukame ikiwa ni pamoja na mhogo,mtama,mikunde
na viazi vitamu.
Twamala alisema wananchi wanapaswa kujiwekea
utaratibu wa kucheza na misimu ya mvua kwa kulima mazao yanayotakiwa ili
kukabiliana na uhaba wa njaa.
Katika ziara hiyo mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi
Ndikilo alitembelea maeneo ya Mji wa
Rufiji,Mkuranga,Kibiti,Bagamoyo,Chalinze,Kisarawe na Kibaha.
No comments:
Post a Comment