Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa
serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro uliopo
kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo iliyopo Wasso Desemba 15,
2016. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
.................................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw.
Rashid Taka na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Raphael Siumbo kufanya
uchunguzi na kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kuhusika katika
uuzwaji wa kiwanja cha shule ya msingi Waso.
Ametoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Desemba 15, 2016) wakati
akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Waso
Wilaya ya Ngorongoro akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Waziri Mkuu alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona watendaji wachache
wasiokuwa waadilifu wanamega kiwanja cha shule na kukiuza kwa maslahi
yao, hivyo aliwataka viongozi hao kufuatilia na kumpa taarifa ya hatua za
kisheria walizochukua kwa wahusika.
“Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi hapa kuna malalamiko ya viwanja fuatilieni
viwanja hivyo vinavyolalamikiwa na wananchi ni viwanja gani je hiyo ya kwamba
mmeuza viwanja vya shule ameuziwa nani,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu amemtaka Bw. Taka ahakikishe Mkuu wa Idara ya Ardhi,
Maliasili na Mzingira, Bw. Switbeth Byorushengo anatekeleza majukumu yake
ipasavyo. Ametoa agizo hilo baada ya wananchi kudai Ofisa huyo ameshindwa
kufanya kazi na kumuomba Waziri Mkuu aondoke naye.
Alisema Bw. Byorushengo anatakiwa kuhakikisha halmashauri hiyo inapima
viwanja vya kutosha na kutoa hati kwa wananchi ili waweze kupata maeneo ya
kujenga makazi na shughuli zingine za kijamii.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa halmashauri
hiyo Bw. Byorushengo kuhakikisha halmashauri hiyo inaanza ujenzi wa hospitali
ya wilaya na ifikapo Aprili, 2017 awe amepewa taarifa za ulipofikia ujenzi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi huyo alisema tayari wapo katika mchakato wa
ujenzi wa hospitali ya wilaya ambapo wametenga sh. milioni 800 za kuanzia.
Akizungumzia kuhusu mgogoro wa ardhi kati ya vijiji vya Tarafa ya
Loliondo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Waziri Mkuu alitoa muda wa siku 30
kwa uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) wawe wamekamilisha
uhakiki wa mpaka huo.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye ni Mbunge wa
Ngorongoro Mheshimiwa William Ole Nasha alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia
kutatua mgogoro huo wa ardhi kwa kuwa ni wa muda mrefu na unakwamisha shughuli
za maendeleo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema Wilaya ya
Ngorongoro inachangamoto nyingi ikiwemo ya ardhi na sasa kuna mgogoro kati ya
Kampuni ya Thomson Safari na wananchi ambao wanadai kuwa ardhi hiyo
ilichukuliwa kinyemela na mwekezaji huyo bila ya wao kushirikishwa.
Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kumalizika mkoani hapa atarudi
wilayani Ngorongoro kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo ya ardhi na
matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na wawekezaji ambazo matumizi yake
hayajulikani.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, DESEMBA 16, 2016.
No comments:
Post a Comment