Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki, akizungumza na Vyombo vya Habari
jijini Dar es Salaam, kuhusu Kaya zilizoondolewa kwenye Mpango wa kunusuru Kaya
Masikini, unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), Awamu ya Tatu kwa kukosa sifa. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu,
Ikulu, Bw. Peter Ilomo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Susan Mlawi.
......................................
Serikali imeondoa kaya 55,692 katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, unaotekelezwa
na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), Awamu ya tatu kutokana na
sababu mbalimbali.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Waziri Kairuki, alizitaja Sababu
za kuondolewa kwa kaya hizo ni pamoja kifo, kuhama kijiji/mtaa ambapo mpango
haujaanza kutekelezwa, kutojitokeza mara tatu mfulululizo kupokea ruzuku,
mnufaika kuwa mjumbe wa kamati mbalimbali za mpango, wastaafu, na viongozi wa
watumishi wa Umma.
Alisema hayo yamebainika baada ya uhakiki ambao aliagiza ufanyike mwezi
Februari 2016.
Waziri Kairuki alisema katika uhakiki huo kaya zilizokuwa na mwanakaya
aliyefariki au wote kufariki zilikuwa 13, 898, kaya zilizohama vijiji/mitaa
ambapo mpango haujaanza kutekelezwa 6,228.
Aliongeza kaya ambazo hazikujitokeza mara tatu mfululizo kupokea ruzuku
zilikuwa 17,746, zilizothibitishwa kuwa sio masikini zilikuwa 13,468 na kaya
zilizogundulika kuwa na baadhi ya wanakaya wajumbe wa kamati za usimamizi za
Jamii, Halmashauri za Vijiji/Kamati za Mitaa, Viongozi na watendaji zilikuwa
4,352.
Mhe. Kairuki aliainisha kuwa kufuatia agizo lake alilotoa mwanzoni mwa
mwaka huu hadi Septemba 2016 kiasi cha shilingi Bilioni 6,427,110,309 kimeokolewa kwa kaya
42, 035 zilizoondolewa kwa kipindi hicho, na kusisitiza kiasi hicho
kitaongezeka kwasababu zoezi hilo linaendelea.
Waziri Kairuki alifafanua kuwa ameshauriana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais-TAMISEMI kuwasimamisha waratibu wa TASAF Wilaya na uchunguzi kufanyika wa
jinsi walivyojihusisha kuvuruga utekelezaji wa mpango kwa kuandikisha kaya
zisizo na sifa.
Kufuatia hilo, Waziri Kairuki alimwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF
kuwasimamisha kazi mara moja na kuendelea na hatua za kinidhamu kwa Maafisa Washauri
na Ufuatiliaji 106 walioko kwenye Halmashauri walioshindwa kufuatilia na
kusimamia mpango hivyo kusababisha kaya zisizostahili kuingizwa kwenye Mpango
na kuendelea kulipwa isivyostahili.
Wengine alioelekeza kusimamishwa ni Maafisa watano wa TASAF Makao Makuu
wanaosimamia mpango, pamoja na Mameneja Uratibu na Mkurugenzi wa Uratibu ambao
ndio wasimamizi wakuu.
Aidha, Waziri Kairuki ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina kwa
kipindi kisichozidi mwezi mmoja ili kubaini ushiriki wa Maafisa hao na kuchukua
hatua stahiki kwa wale watakaothibitika kuhusika katika kuvuruga utaratibu wa
utekelezaji wa mpango au kuwepo udhaifu katika usimamizi, ufuatiliaji na
uwajibikaji.
Waziri Kairuki alielekeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi
wa Halmashauri, Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya wahakikishe kuwa fedha zote
zilizotolewa kwa kaya zisizokuwa na sifa zinarejeshwa ili ziwanufaishe
walengwa.
Waziri Kairuki alitoa rai kwa wananchi na wadau wote wa Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF)
kutoa taarifa za watu wote ambao wananufaika lakini hawastahili kuwa kwenye
Mpango ili malipo yasifanyike kwa wote wasiostahili.
Awamu ya Tatu ya TASAF ilianza mwaka 2012 ambapo Serikali inatekeleza
Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini.
Kaya zilizoandikishwa idadi yake ni Milioni moja laki moja na kumi mia
sita thelasini na tano, 1,110,635, na kaya hizo huandikishwa baada ya hatua ya
utambuzi ambayo jamii husika hushirikishwa katika mikutano ya pamoja kwa kuweka
vigezo vya umasikini na baadaye kaya hizo hufanyiwa uhakiki kwa kutumia takwimu
na viashiria vya umasikini.
Takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania
takribani asilimia 28.2 bado ni masikini sana, na serikali hadi sasa
imeshatumia shilingi bilioni 391,835,484,755 zilizolipwa katika mikupuo nane
kwa kaya milioni moja laki moja na kumi
mia sita thelasini na tano, 1,110,635.
No comments:
Post a Comment