Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kushoto
akipokea vifaa mbalimbali vya matibabu ya mabadiliko ya awali ya Saratani ya
mlango wa kizazi vyenye thamani takribani milioni 100 za kitanzania kutoka kwa
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Pink Ribbon Red Ribbon Bi.
Celina Schocken jijini Dar es salaam.
..........................
MIKOA na halmashauri nchini zimetakiwa kuweka tahadhari juu ya ugonjwa wa
kipindupindu kwa kuzingatia usafi binafsi na usafi wa mazingira hasa wakati wa
mvua za vuli na msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ili kuweza kuepuka ugonjwa
huo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na
Watoto Ummy Mwalimu wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa
ugonjwa wa kipindupindu kwa mwezi Novemba 2016 uliofanyika jijini Dar es
salaam.
“Mikoa na Halmashauri zote nchini ziwe katika hali ya tahadhari juu ya
ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia usafi binafsi na usafi wa mazingira hasa
wakati wa mvua za vuli na msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ili kuweza
kuepuka ugonjwa huo” alisema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Mikakati ya kudhibiti ugonjwa wa
Kipindupindu ishirikishe sekta mbalimbali za afya nchini bila kusahau jamii
husika na kuhakikisha kila Halmashauri inaunda na kuimarisha Kamati ya Afya ya
Kata.
Aidha Waziri Ummy ameiagiza Mikoa na Halmashauri zote nchini kutoa
taarifa ya wagonjwa wapya wa Kipindupindu ili jitihada za makusudi za kupambana
na ugonjwa huo zifanyike mapema ili kujenga taifa lisilo na magonjwa ya
mlipuko.
Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa takwimu zinaonesha katika mwezi
Novemba 2016 jumla ya mikoa sita ikiwemo Morogoro yenye wagonjwa 282, Dodoma 96
na vifo 2, Mara 31, Kigoma 30 na vifo 4, Arusha 11 na Dar Es Salaam 8 kutoka
wagonjwa 250 na vifo 4 kwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Kwa wakati huohuo Waziri Ummy amepokea vifaa vya matibabu ya mabadiliko
ya awali ya Saratani ya mlango wa kizazi vyenye thamani takribani milioni 100
za kitanzania kutoka Shirika la Kimataifa la Pink Ribbon Red Ribbon ili
kupambana na ugonjwa huo nchini.
Akikabidhi msaada huo Mtendaji Mkuu wa Shirikahilo Bi. Celina Schocken
amesema kuwa wametoa vifaa hivyo ili kuisaidia nchi kwa juhudi za kimakusudi
katika kupambana na ugonjwa wa saratani ili kuokoa maisha ya wanawake wa
Tanzania.
“Tumeamua kutoa vifaa hivi ili kuisaidia nchi kwa juhudi za kimakusudi
katika kupambana na ugonjwa wa saratani ili kuokoa maisha ya wanawake wa
Tanzania ”alisema Bi. Schocken.
No comments:
Post a Comment