Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene akitoa maelezo kwa waandishi
wa habari juu ya kutoeleweka vema Agizo la Rais Dkt. John Magufuli kuhusu zoezi
la usitishaji wa kuwaondoa Wafanyabiashara ndogo ndogo katikati ya miji na
kuwatafutia maeneo rafiki kufanyia biashara zao kushoto kwake ni Naibu Katibu
TAMISEMI (Afya) Dk. Zainab Chaula.
.............................................
Serikali imewaagiza Wakuu wa Mikoa,
Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatekeleza agizo la Rais
Dk.John Magufuli la kuwatafutia maeneo ya kufanyia biashara Wafanyabiashara
ndogo ndogo ‘wamachinga’ na si kuwaacha wafanye biashara zao kiholela.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), George
Simbachawene alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.
Amewataka wakuu hao kuwawekea
Wamachinga utaratibu wa kupangiwa maeneo ya shughuli zao yenye wateja wa
kutosha, miundombinu rafiki na washirikishwe katika michakato yote wakati wa
maandalizi ya maeneo hayo.
Amefafanua kuwa Rais Magufuli
alisitisha zoezi la kuwaondoa kiholela wamachinga kutoka katika maeneo
wanayofanyia biashara zao kwasasa hadi pale mamlaka husika zitakapoandaa maeneo
maalum kwa ajili yao.
“Maagizo ya Rais yameonesha namna
anavyowapenda na kuwathamini wamachinga na aliweka msisitizo wasiondolewe mpaka
pale yatakapotengwa maeneo mbadala,”amesema Simbachawene.
Amebainisha utaratibu wowote wa
kuwapangia maeneo mapya uzingatie ushirikishwaji ili kuondoa msuguano wakati wa
kuwahamisha na kwamba pale inapowezekana wapangiwe maeneo ya katikati ya mji
ikibidi kuteua mitaa mahsusi kwa utaratibu utakaowekwa ili wafanye biashara
zao.
Pamoja na maelezo hayo, Simbachawene
amesema Rais alisisitiza kwamba maagizo yake juu ya wamachinga hayana maana
kuwa kwasasa wamachinga wafanye biashara zao kwenye barabara za kupita magari
na watembea kwa miguu au kwenye hifadhi za barabara.
Amewasisitiza wakuu hao kujipanga
kutekeleza maagizo ya rais kwa ufasaha, weledi na umakini mkubwa ili kuwasaidia
wamachinga kufanya biashara zao na kujipatia kipato na kuzitaka mamlaka za
serikali kuheshimu shughuli zao.
Wakati huo huo, Simbachawene
amewaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa ya Rukwa na Arusha watafute shule ndani ya
mikoa yao na kuwapanga wanafunzi ambao wameondolewa shule za sekondari Makuyuni
na Milundikwa ambazo majengo yake yamerudishwa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).
Amesema serikali imelazimika
kuwaondoa wanafunzi 254 wa shule ya Makuyuni wa kidato cha kwanza hadi cha tatu
na katika shule ya Milundikwa wanafunzi 120 wa kidato cha tano na sita.
Pia amesema walimu na watumishi wasio
walimu ambao walikuwa wakifundisha katika shule hizo wapangiwe kwenye shule
watakazopelekwa wanafunzi hao.
Ametaka utekelezaji huo wa agizo hilo
ufanyike kabla shule hazijafunguliwa januari 2017 na lizingatie kutowavuruga
wanafunzi wa kidato cha sita ambao tayari wamesajiliwa kufanya mtihani wa Taifa
mwezi mei, 2017.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene akitoa Agizo juu ya
Shule za Sekondari za Makuyuni (Arusha) na Milundikwa (Rukwa) ambazo majengo
yake yalikuwa ni makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na baadae Halmashauri
zikapewa kuyatumia majengo hayo kama shule za Bweni na kwa sasa zinarejeshwa
tena mikononi mwa Jeshi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za Jeshi.
No comments:
Post a Comment