WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Bi.
Theresia Mahongo kuhakikisha kampuni zinazomilikiwa na madiwani na watumishi wa
halmashauri hiyo hazipewi zabuni zinazotolewa katika maeneo yao kwa
ajiliya kuepusha migongano ya kimaslahi.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Desemba 5, 2016) wakati akizungumza na
watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Karatu mkoani Arusha katika ukumbi bwalo
la Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Karatu akiwa katika ziara yake ya
kikazi mkoani hapa.
“Hauzuiliwi kufanya biashara ili mradi kampuni yako isifanye kazi katika
halmashauri ambayo wewe unaitumikia na una nguvu nayo ili kuepusha migongano ya
kimaslahi kwani miradi yote utajilundikia,” amesema.
Pia amewataka Wakuu wa Idara katika halmashauri hiyo walisaidie Baraza la
Madiwani katika kubaini vyanzo vipya vya mapato kwa lengo la kuongeza mapato ya
halmashauri yao.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amewataka watumishi wa halmashauri wa umma
kujitathmini na kujiridhisha kama wanafuata misingi ya utumishi katika
utendaji kazi wao wa kila siku. Amewasisitiza wawatumikie wananchi kwa
uadilifu na uaminifu mkubwa.
“Hatuhitaji kuwa na mtumishi mvivu, asiyewajibika, mwizi, mla rushwa na
asiyekuwa muadilifu mahali pa kazi.
Na atakayeona ameshindwa kutunza na kusimamia fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi atoe taarifa hatutaki watu kufanya kazi kwa mazoea,” amesema.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa ” watumishi wa umma lazima mbadilike na muwe
na nidhamu ya kazi. Muache malalamiko fanyeni kazi na msitafute sympathy
(huruma) kutoka kwa watu kwani Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ,” amesema.
Amesema katika baadhi ya ofisi za Serikali kuna ugonjwa wa watumishi
wanapoona wageni wamelifika kwa ajili ya kupatiwa huduma wanawapita bila ya
kuwasikiliza. ” sasa hatutaki watumishi wa namna hiyo, Jukumu lako ni
kumtumikia Mtanzania na tunataka kuona mabadiliko. Hatutaki kuona watu
wakizubaa maofisini,”.
Waziri Mkuu amesema Serikali ikikuta wananchi wanalalamika kutokana na
kutoridhishwa na huduma zitolewazo na watumishi wa umma itahakikisha
watumishi hao wanachukuliwa hatua. Serikali ni ya Watanzania wote hivyo lazima
wahudumiwe vizuri bila ya kujali uwezo wao kifedha wala itikadi zao za kidini
na kisiasa.
No comments:
Post a Comment