Waziri
wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango akielezea waandishi wa habari kuhusu
ukuaji wa uchumi wa nchi na mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya kiuchumi
alipozungumza na wanahabari katika wizara hiyo leo jioni soma taarifa kamili ya
waziri huyo hapa chini.
...................................
Nashukuru
kupata fursa ya kuzungumza nanyi leo kuhusu hali ya uchumi wa Taifa kwa
kipindi cha Julai – Desemba, 2016 na matarajio hadi Juni 2017. Nitajitahidi
kutumia lugha rahisi ili wananchi wa kawaida waweze kuelewa mambo ya msingi kuhusu
mwenendo wa uchumi wa nchi yetu.
Ustawi
wa Uchumi Unapimwaje?
Ustawi
wa uchumi wa Taifa unapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali. Kwa kifupi,
ustawi wa uchumi unapimwa kwa kuangalia kama shughuli mbalimbali za kiuchumi
zinaongezeka au zinapungua au kama zimedumaa.
Shughuli
muhimu zinazoangaliwa ni pamoja na uzalishaji wa chakula na mazao
mbalimbali ya kilimo, mifugo na uvuvi; uzalishaji wa bidhaa za viwandani na
migodini; ujenzi wa miundombinu; uwekezaji; mwenendo wa bei, biashara na
masoko; utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii ikiwa ni pamoja na elimu, afya,
maji, mawasiliano, usafiri na usafirishaji, utalii na huduma za kifedha; na
kiwango cha utekelezaji wa bajeti ya Serikali.
Aidha,
uchambuzi na tathmini ya hali ya uchumi wa Taifa inafanyika kwa kulinganisha
viashiria na malengo yaliyowekwa au kwa kuangalia vigezo vinavyokubalika
kimataifa au kwa kulinganisha na mwenendo wa viashiria vya kiuchumi katika nchi
nyingine. Vilevile, afya ya uchumi inapimwa kwa kutumia vigezo vya jumla, vya
kisekta na kimaeneo.
- VIASHIRIA MBALIMBALI VYA MWENENDO WA UCHUMI WA TAIFA
1.
Ukuaji wa
Pato la Taifa
Ukuaji
wa uchumi (kasi ya kuongezeka au kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa na huduma
katika nchi) ni mojawapo ya vitu vinavyotazamwa katika kutathmini afya ya
uchumi wa Taifa.
Kiashiria kinachotumika kupima ukuaji wa uchumi ni ukuaji wa
Pato la Taifa yaani thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa katika nchi
katika kipindi kinachorejewa ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Takwimu za
ukuaji uchumi zinaonesha kuwa uchumi wa Taifa umeendelea kukua na Tanzania
imebaki kuwa miongoni mwa nchi za bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara
ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa zaidi.
Mwenendo wa ukuaji wa uchumi
kwa baadhi ya nchi jirani na kisekta umeoneshwa katika jedwali la 1 na la 2.
Jedwali1:
Ukuaji wa Pato la Taifa Katika Baadhi ya Nchi za Kiafrika
NCHI
|
2015
|
2016
|
Burundi
|
-4.0
|
-0.5
|
Kenya
|
5.6
|
6.0
|
Rwanda
|
6.9
|
6.0
|
Tanzania
|
7.0
|
7.2
|
Uganda
|
4.8
|
4.9
|
Zambia
|
3.0
|
3.0
|
Malawi
|
2.9
|
2.7
|
Congo DRC
|
6.9
|
3.9
|
Afrika Kusini mwa Sahara
|
3.4
|
1.4
|
1.
Mfumuko wa
bei
Kiashiria
kingine cha jumla ni mfumuko wa bei ambao unapima mabadiliko ya bei za bidhaa
na huduma zinazotumiwa na kaya nchini.
Mfumuko wa bei ulipungua kutoka asilimia
6.5 Januari 2016 hadi asilimia 5.5 Juni 2016 na kupungua zaidi hadi asilimia
4.5 Septemba 2016 na baadaye kupanda kidogo mwezi Novemba na kufikia asilimia
4.8. Maana yake ni kuwa bei za bidhaa na huduma ziliongezeka kwa kasi ndogo
zaidi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Mwenendo
huu wa kushuka mfumuko ulichangiwa na kasi ndogo ya ongezeko la bei za chakula
nchini, kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia, utekelezaji
madhubuti wa sera za bajeti na fedha, na utulivu wa thamani ya Shilingi.
Kupanda kwa mfumuko wa Bei mwezi Novemba kulitokana na kupungua kwa upatikanaji
wa bidhaa za chakula (mbogamboga, unga wa mahindi na ngano) pamoja na
mkaa.
Mfumuko
wa bei katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki: Wastani wa mfumuko wa bei
uliendelea kubakia katika wigo wa tarakimu moja.
Hata hivyo, mwezi Novemba
2016, karibu nchi zote zilikuwa na ongezeko la mfumuko wa bei kutokana na
kuyumba kwa ugavi wa chakula katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia. Nchini Uganda, mfumuko wa bei
uliongezeka kufikia asilimia 4.6 Novemba 2016 ikilinganishwa na asilimia 4.1
Oktoba 2016. Aidha, mfumuko wa bei nchini Kenya ulipanda na kuwa asilimia 6.68
ikilinganishwa na asilimia 6.47 katika kipindi hicho.
Matarajio
kwa mwaka 2017 ni kubaki na mfumuko wa bei katika kiwango cha tarakimu moja.
Hata hivyo upungufu wa mavuno ya mazao ya chakula uliojitokeza kwa baadhi ya
nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika unaweza kusababisha shinikizo la mfumuko wa
bei katika siku za usoni.
1.
Thamani ya
shilingi
Thamani
ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Kimarekani imeendelea kuimarika.
Shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa kati shilingi 2,167 hadi 2,199 kwa dola moja
ya Marekani.
Hali
hii ilitokana na kuwa sera thabiti za uchumi pamoja na mwenendo mzuri wa urari
wa mapato ya fedha za kigeni hususan kutokana na mauzo ya bidhaa za viwandani,
utalii na huduma mbalimbali.
1.
Mwenendo
wa Sekta ya Kibenki
Tathmini
ya hali ya mabenki yetu inaonesha kuwa mabenki yetu ni imara na salama, yakiwa
na mitaji na ukwasi wa kutosha:
Kiwango
cha mitaji kikilinganishwa na mali iliyowekezwa (total capital to total risk
weighted assets and off-balance sheet exposures) kilikuwa asilimia 18.68 kikilinganishwa
na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha asilimia 12.0.
Hali
ya ukwasi hupimwa kwa kuangalia uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa
fedha taslimu na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi (liquid assets
to demand liabilities).
Uwiano huu ulikuwa asilimia 37.46 ukilinganishwa na
uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia 20.
Amana
za wateja katika mabenki zilipungua kidogo kutoka shilingi trilioni 20.73 mwezi
Desemba 2015 kufikia shilingi trilioni 20.57 mwezi Septemba 2016.
Miongoni mwa
sababu zilizochangia kupungua kwa amana kwenye mabenki ni pamoja na uamuzi wa
Serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi na mashirika ya umma kutoka
mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo amana za serikali kwenye
mabenki ya biashara ni asilimia 3 tu ya amana zote za mabenki.
Upatikanaji
wa huduma za kifedha kwa wananchi wasiofikiwa na mabenki umeendelea kuongezeka
kutokana na ubunifu wa mipango ya utoaji wa huduma za malipo ya rejareja
kupitia simu za mikononi, pamoja na huduma za uwakala wa mabenki (agent banking
services).
Benki
zilizopata msukosuko: Katika kipindi cha Julai – Septemba 2016, CRDB na TIB
Development Bank zilipata hasara.
Hasara ilisababishwa na tengo kwa ajili ya
mikopo chechefu (provision for loan losses). Aidha, Twiga Bancorp imewekwa
chini ya uangalizi wa BOT, jambo ambalo si geni. Crane Bank Ltd ya Uganda
imewekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya nchi hiyo Oktoba 2016 kama
ilivyokuwa Imperial Bank Kenya, Oktoba 2015.
Licha ya hali hiyo, benki nyingi
zikiwamo CRDB na TIB Development Bank, zimebaki kuwa na mitaji na ukwasi wa
kutosha kwa mujibu wa Sheria. Aidha ni vema kukumbuka kwamba jumla ya benki na
taasisi za fedha nchini kote ni 66 na zina matawi 783.
Hivyo, kwa benki tatu
(3) tu kupata msukosuko katika robo moja ya mwaka si sababu ya kuzua taharuki!
Mwenendo
wa mabenki katika nchi nyingine Afrika: Kupungua kwa mikopo kwa sekta binafsi
katika miezi ya hivi karibuni siyo kwa Tanzania pekee. kwa mfano kiwango cha
ukuaji cha ukuaji wa mikopo kwenda sekta binafsi katika nchi jirani ya Kenya
kilipungua kutoka asilimia 19.7 kati ya Julai na Oktoba 2015 hadi kufikia
asilimia 4.1 katika kipindi kama hicho katika mwaka huu 2016.
Aidha huko Uganda
mikopo kwa sekta binafsi ilipungua kutoka asilimia 25.2 mwezi September 2015
hadi asilimia -1 mwezi September 2016.
Pia mwenendo usioridhisha ulijitokeza
katika mikopo chechefu katika nchi hizo jirani na kusababisha baadhi ya mabenki
hususan Crane Bank ya Uganda na Imperial Bank ya Kenya, kuwekwa chini ya
uangalizi. Hali ni mbaya zaidi kwa nchi kama Nigeria na Ghana zinazouza mafuta.
Ujazi
wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 4.5 katika kipindi cha
mwaka ulioishia Oktoba 2016 (au ongezeko la shilingi bilioni 547.3)
ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 16.6 (au ongezeko la shilingi bilioni
3,084.6) kwa mwaka ulioishia Oktoba 2015.
Ukuaji mdogo unatokana na
usimamizi madhubuti wa matumizi sambamba na kupungua kwa fedha za misaada na
mikopo kutoka nje.
Kwa
upande wa mikopo kwa shughuli za biashara na za binafsi ilikuwa asilimia 39 ya
mikopo yote. Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa shilingi bilioni 1,550.5
hadi shilingi bilioni 16,654.4 katika mwaka unaoishia Oktoba 2016, sawa na
ukuaji wa asilimia 10.3 ikilinganishwa ongezeko la shilingi bilioni 2,977.6 au
ukuaji wa asilimia 24.6 katika kipindi kinachoishia Oktoba 2015. Katika kipindi
cha Julai – Oktoba 2016 mwenendo wa riba za amana na za mikopo umekuwa wa
kupanda na kushuka.
Wastani wa riba za amana ulikuwa asilimia 9.49 ukilinganisha
na wastani wa asilimia 9.08 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
Aidha,
wastani wa jumla wa riba za mikopo ulikuwa asilimia 15.85 ikilinganishwa na
asilimia 16.11 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
Mwenendo wa riba za mikopo
unategemea mambo mbalimbali kama vile, gharama ya fedha (cost of funds),
gharama za uendeshaji wa benki husika (bank’s operational cost), kiwango cha
faida (profit margin), mfumuko wa bei na vihatarishi vinavyotokana na sifa za
mkopaji (risk premium).
Viwango vya riba katika masoko ya fedha vimeendelea
kutegemea nguvu ya soko na hali ya ukwasi unaotokana na sera za fedha na
kibajeti.
1.
Sekta ya
Nje na Akiba ya Fedha za Kigeni
Hadi
kufikia Novemba 2016, nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na
uhamishaji mali nchi za nje (current account deficit) ilipungua kwa asilimia
52.5 na kufikia nakisi ya dola za Kimarekani milioni 1,904.2, kutoka nakisi ya
dola za Kimarekani milioni 4,008.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
Kupungua huko kulitokana na ongezeko la thamani ya madini hususan dhahabu,
bidhaa asilia, mapato yatokanayo na utalii, pamoja na kupungua kwa thamani ya
bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za mitaji, na bidhaa za
matumizi ya kawaida.
Katika kipindi hicho thamani ya bidhaa na huduma
zilizouzwa nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 6.4 na kufikia dola za
Kimarekani milioni 8,502.8 wakati thamani ya bidhaa na huduma toka nje
zilipungua kwa asilimia 15.4 na kufikia dola za Kimarekani milioni 9,846.0.
Hadi
mwezi November 2016, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Kimarekani
milioni 4,254.1 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya
nchi kwa takriban miezi 4.
Wakati huo huo, rasilimali za fedha za kigeni za
mabenki (gross foreign assets) zilikuwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni
777.0 Hivyo, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha.
Jedwali
2: Viashiria vya Ustawi wa Uchumi
ENEO
|
KIASHIRIA
|
JUL – SEPT 2015
|
OCT – DES 2015
|
JUL – SEPT 2016
|
OCT – DES 2016
|
2016
|
Ukuaji wa Uchumi
|
Ukuaji wa Pato la Taifa
|
6.3%
|
9.1%
|
6.2%
|
8.0%
|
7.2%
|
Sekta zenye mchango mkubwa ktk
Pato la Taifa
|
Kilimo (35.8%); Ujenzi (12.4%);
Biashara (9.7%)
|
Kilimo (28.3%); Ujenzi (11.0%);
Biashara (10.7%); Viwanda (6.3%)
|
Kilimo (24.7%); Ujenzi (14.6%);
Biashara (10.3%); Viwanda (7.3%); Madini (5.2%)
|
|||
Sekta zilizokua haraka
|
Ujenzi (17.6%); Usafirishaji &
Uhifadhi (10.6%); Mawasiliano (9.1%); Huduma za kifedha (8.4%); Madini (8.0%)
|
Madini (15.750; Ujenzi (13.8%);
Huduma za kifedha (12.6%); Mawasiliano (10.2%); Viwanda (9.5%)
|
Madini (19.9%); Mawasiliano (14.3%);
Usafirishaji (12.2%); Nishati (11.8%); Huduma za kifedha (8.7%);
|
|||
Sekta zilizokua polepole
|
Kilimo (2.7%);
|
Kilimo (0.3%)
|
||||
Bei, Biashara na Masoko
|
Mfumuko wa bei
|
5.3%
|
6.6%
|
Jul (5.1%)
Ago (4.9%)
Sep (4.5%
|
Okt (4.5%),
Nov (4.8%)
|
5.5%
|
Nakisi kwenye Biashara ya Nje (US$
Milioni)
|
||||||
Mwenendo wa Sekta ya Fedha
|
Akiba ya fedha za Kigeni (US$
milioni)
|
3,999.3
|
4,093.7
|
4,096.0
|
4,254.1
|
4,654.2
|
Kiwango cha Kubadilisha Fedha (Tshs;
1US$)
|
2,150.0
|
2,148.5
|
2,175.32
|
2,170.97
|
||
Uwiano wa mikopo na Amana za wateja
katika mabenki
|
77.16
|
78.88%
|
71.16%
|
|||
uwiano wa jumla ya
mitaji
na mali iliyowekezwa (Total capital/Total risk weighted assets)
|
Sept (18.68%)
|
19.4% (Des)
|
Sept (18.68%)
|
12%
|
||
uwiano wa raslimali inayoweza
kubadilishwa kirahisi kuwa fedha taslim na amana zinazohitajika katika muda
mfupi (Liquid assets/Demand liabilities)
|
Sept (37.46%)
|
Des (37.18%)
|
Sept (37.46%)
|
20%
|
||
Riba za Mikopo ya mwaka mmoja
|
Sept (14.4%)
|
Okkt (14.27%)
|
Sept (13.4%)
|
Okt (13.23%)
|
||
Riba za amana za mwaka mmoja
|
Sept (10.6%)
|
Okt (10.95%)
|
Sept (11.5%)
|
Okt (11.46%)
|
||
Amana za wateja
|
Sept (Tshs19.892 trillion)
|
Okt (Tshs19.995 trillion)
|
Sept (Tshs20.73 trillion)
|
Okt (Tshs20.98 trillion)
|
||
Mikopo chechefu
|
Sept (6.62)
|
Des (6.64)
|
Sept (8.26)
|
- MWENENDO WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI 2016/17
1.
Mwenendo
wa Mapato
Katika
mwaka wa fedha 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya na kutumia shilingi bilioni
29.539.6. Katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya mwaka 2016/17,
makusanyo ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni
7,018.7 sawa na asilimia 96.4 ya makadirio ya shilingi bilioni 7,281.2 katika
kipindi hicho.
1.
Mapato ya
kodi
Mapato
ya kodi yalifikia shilingi bilioni 5,674.7 ikiwa ni asilimia 96.6 ya lengo la
kukusanya shilingi bilioni 5,873.3 kwa kipindi hicho.
Aina za kodi zilizofanya
vizuri ni pamoja na kodi ya Ongezeko la thamani ndani, ushuru wa forodha na
ushuru wa bidhaa nje.
Hii ilitokana na usimamizi thabiti wa makusanyo kwenye
malimbikizo ya kodi, ukaguzi na uchunguzi wa marejesho ya kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT returns) na kodi ya mapato uliofanyika katika kipindi hicho,
kupanua wigo wa kodi kwa kusajili walipa kodi wapya, pamoja na utekelezaji wa
mikakati ya kuongeza makusanyo ya kodi.
1.
Mapato
yasiyotokana na kodi
Mapato
yasiyotokana na kodi yalifikia shilingi bilioni 1,133.4 sawa na asilimia 0.2
zaidi ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 1,130.6. Sababu za kuvuka lengo ni
kutokana na kuongezeka kwa mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na TRA
ikijumuisha kodi ya majengo pamoja na kufanya vizuri kwa Wizara na Mikoa
zinazokusanya maduhuli.
1.
Aina za
kodi ambazo hazikufikia lengo
Aidha,
aina za kodi ambazo hazikufikia lengo ni pamoja na ushuru wa bidhaa ndani, kodi
ya Ongezeko la Thamani (VAT) nje, kodi ya mapato na kodi nyingine
hasa ushuru wa stamp (stamp duty) na Departure fee.
Sababu
zilizopelekea kutokufikiwa kwa malengo la ukusanyaji wa mapato ya kodi:
1.
Kushuka
kwa mauzo ya bidhaa mbalimbali kama vile saruji, bia, vinywaji baridi na bidhaa
nyinginezo za jumla na rejareja kumesababisha makampuni mengi kutopata faida
ilivyotarajiwa na hivyo kupunguza wigo wa ukusanyaji wa kodi;
1.
Mabenki
makubwa yalifanya marekebisho ya makisio yao ya kulipa kodi kutokana na kushuka
kwa mapato ya riba;
1.
Kupungua
kwa uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia ambako kuliathiri kodi ya zuio
na kodi ya mapato;
1.
Ajira
kutoongeza kama ilivyotarajiwa baada ya kusitisha ajira mya ili kupisha zoezi
la kubaini watumishi hewa serikalini;
1.
Baadhi ya
kampuni kupunguza bei katika baadhi ya bidhaa kama vile bia ili kuongeza mauzo
yao;
1.
Kuongezeka
kwa malimbikizo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye sekta ya uzalishaji wa
umeme hususan IPTL na Symbion Power Ltd;
1.
Matumizi
hafifu ya mashine za kielektroniki (EFD);
1.
Kupunguza
kwa ulaji wa bidhaa zinazotozwa kodi na ushuru wa bidhaa husuan bia, vinywaji
vikali na vinywaji baridi;
1.
Matatizo
ya kifedha yaliyokumba kampuni za usafirishaji wa anga pamoja na kupungua kwa
idadi ya wasafiri hususan wa sekta ya umma (departure charges); na
1.
Kushuka
kwa uingizaji wa bidhaa kutoka nje.
Hatua
za kuimarisha ukusanyaji wa kodi ili kufikia malengo katika kipindi kilichobaki
cha mwaka 2016/17:
1.
Kupanua
wigo wa kodi kwa kuendelea kusajili na kuhakiki taarifa za walipakodi kwenye
mifumo ya kikodi ya TRA;
1.
Kuendelea
kushirikiana na Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi kwa kubadilishana
taarifa;
1.
Kuendelea
kusimamia na kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutolea
risiti (EFDs);
1.
Kudhibiti
udanganyifu katika ukadiriaji wa kodi kwa kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa
mara kwa walipakodi;
1.
Kuimarisha
ukaguzi wa kodi (tax audit);
1.
Kudhibiti
na kusimamia bidhaa zinazopitia hapa nchini kwenda nchi jirani (transit) kwa
kutumia mfumo wa kufuatilia mizigo (electronic cargo trackin system);
1.
Kuboresha
ukaguzi wa mizigo bandarini; na
1.
Kudhibiti
biashara ya magendo hususan katika Bahari ya Hindi, mipaka na njia zisizo rasmi
kati ya nchi yetu na nchi jirani.
1.
Misaada na
Mikopo Yenye Masharti Nafuu
Katika
mwaka 2016/17 Washirika wa Maendeleo waliahidi kuchangia bajeti ya Serikali kwa
kiasi cha shilingi bilioni 3,600.8, ambapo kati ya hizo, misaada ya Kibajeti ni
shilingi bilioni 483.0, Mifuko ya Kisekta ni shilingi bilioni 372.1 na miradi
ya Maendeleo ni shilingi bilioni 2,745.7.
Jumla ya misaada na mikopo nafuu
iliyotolewa kwa kipindi cha Julai hadi Novemba 2016 ni shilingi bilioni 603.9
sawa na asilimia 21.5 ya lengo la shilingi bilioni 2,806.3 katika kipindi
hicho.
Misaada:
Kati ya Julai hadi Novemba 30, 2016, misaada ya kiasi cha shilingi bilioni
287.5 ilitolewa, sawa na asilimia 28.4 ya lengo la shilingi bilioni 1,012.6 kwa
kipindi hicho. Kati ya kiasi hicho, misaada ya kibajeti (General Budget
Support) ni shilingi billioni 36.1 ambazo zote zimetolewa na EU tu; na
kiasi kilichopokelewa kwa ajili ya mifuko ya kisekta (Basket Funds) ni shilingi
bilioni 58.4, sawa na asilimia 61 ya lengo ya shilingi bilioni 95.5 kwa kipindi
hiki cha marejeo.
Aidha, misaada kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa
kipindi hicho ilifikia shilingi bilioni 193.1, ambayo ni asilimia 21 ya lengo
la shilingi bilioni 917.1 kilichotarajiwa kupokewa kwa kipindi hicho.
Mikopo
nafuu iliyopokelewa kutoka kwa washirika wa maendeleo kwa ajili ya miradi ya
maendeleo kati ya Julai hadi Novemba, 2016 ni shilingi bilioni 316.4. Kiasi
hiki ni sawa na asilimia 17.6 ya lengo la shilingi bilioni 1,793.7.
Aidha,
katika kipindi hicho, hakuna mikopo nafuu iliyopokelewa kwa ajili ya mifuko ya
kisekta na programu (GBS).
Sababu
za kutofikiwa malengo ya upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu ni pamoja na
masharti magumu yaliyowekwa na wahisani/wakopeshaji. Hata hivyo, Serikali
inatarajia kukamilisha majadiliano na AfDB kati ya mwezi Desemba 2016 hadi
Machi, 2017.
Aidha, majadiliano na Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya, bado
yanaendelea. Kuhusu fedha za miradi, jitihada zinafanyika katika sekta husika
kukamilisha taarifa za miradi zinazohitajika na wafadhili.
1.
Mikopo ya
ndani
Katika
kipindi cha Julai – Oktoba 2016, shilingi bilioni 1,367.2 zilikopwa katika soko
la ndani. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 1,305.7 zilikopwa kwa ajili ya
kulipia dhamana na hatifungani za Serikali zilizoiva na shilingi bilioni 61.5
zilikuwa ni malipo ya marejesho (repayment). Kiasi kilichokopwa katika
kipindi hiki ni sawa na asilimia 58 ya kiasi kilichopaswa kukopwa cha shilingi
bilioni 2,232.5.
1.
Mikopo ya
Kibiashara
Katika
mwaka 2016/17, Serikali ilipanga kukopa fedha kutoka kwenye vyanzo vya
kibiashara kiasi cha Dola
za Kimarekani milioni 936
sawa na shilingi bilioni 2,100.9 ili
kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo. Hata hivyo, hadi kufkia Novemba,
2016 Serikali haikukopa kutoka katika chanzo hiki kutokana na hali ya soko la
fedha la kimataifa kutokuwa nzuri hasa katika kipindi cha robo ya kwanza ya
mwaka 2016/17.
Hali
hii ilisababishwa na mdodoro wa kiuchumi katika bara la Ulaya na hivyo
kuongezeka kwa gharama za mikopo mipya na kuathiri upatikanaji wake. Mfano,
riba ilipanda kutoka wastani wa asilimia 6 hadi asilimia 9.
Kutokana na sababu
hiyo, Serikali iliahirisha kuendelea na mchakato wa kukopa kutoka kwenye masoko
hayo na badala yake ikajielekeza kukopa kutoka nchi nyingine (China, India,
Korea Kusini, Japan).
Aidha, gharama za ukopaji katika masoko ya ulaya imeanza
kuimarika na hivyo Serikali imeanza majadiliano na Benki ya Credit
Suissuie ya Uingereza ili tuweze kukopa dola za kimarekani
milioni 300.
Vilevile majadiliano na taasisi
nyingine za fedha kama Kuwait Fund,
Abu Dhabi Fund na OPEC yameendelea kwa ajili ya kugharamia miradi
mbalimbali.
1.
Mwenendo
wa Matumizi
Sera
za Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17, zililenga kusimamia nidhamu ya
matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na
miongozo mbalimbali.
Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba
mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye
miradi ya maendeleo.
Fedha
zilizotolewa Julai – Novemba, 2016
Katika
kipindi cha Julai – Novemba, 2016 jumla ya Shilingi bilioni 9,481.260
zilitolewa na Hazina kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
- Shilingi bilioni 7,295.455 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya Kawaida (ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri Shilingi 61.047)
- Mishahara ya Watumishi wa Serikali Shilingi 2,834.695,
- Deni la Taifa Shilingi bilioni 3,552.249
- Matumizi Mengineyo Shilingi bilioni 928.511
- Shilingi bilioni 2,185.805 kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo (ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri shilingi bilioni 91.571)
- Fedha za ndani Shilingi bilioni 1,749.047
- Fedha za nje Shilingi bilioni 436.758
1.
Maeneo ya
Msingi ambayo fedha zimeelekezwa
Matumizi
ya kawaida yaliyopewa kipaumbele zaidi katika utoaji wa fedha kwa kipindi cha
Julai – Novemba 2016 ni pamoja na:
- Uboreshaji wa huduma za afya katika ngazi zote ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba Shilingi bilioni 69.346;
- Mitihani ya darasa la nne na saba Shilingi bilioni 33.745;
- Mitihani ya kidato cha pili na nne Shilingi bilioni 31.051;
- Posho ya chakula kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama;
- Chakula cha wafungwa Shilingi bilioni 7.5;
- Mishahara ya watumishi wa Serikali;
- Elimu msingi bila malipo Shilingi bilioni 93.885 (kwa kutenga shilingi bilioni 18.777 kila mwezi);
- Malipo ya posho na stahili mbalimbali kwa maafisa katika balozi zetu nje shilingi bilioni 23.127;
- Ruzuku ya pembejeo shilingi bilioni 10.00;
- Ununuzi wa chakula cha Hifadhi ya Taifa shilingi biliioni 9.00.
- Deni la kuchapisha Vitabu vya Hati za Kusafiria Shilingi 2.569;
- Uendeshaji wa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, Mkutano wa Bunge, Posho ya Jimbo kwa Wabunge pamoja na shughuli za Mfuko wa Bunge Shilingi bilioni 31,137;
- Michango ya Taasisi na Jumuiya za Kimataifa Shilingi billion 8.833;
- Ruzuku ya Vyama vya Siasa Shilingi bilioni 7.168;
Aidha,
sehemu iliyosalia ya fedha za Matumizi ya Kawaida ilielekezwa kwenye shughuli
za kila siku za uendeshaji katika Mafungu mbalimbali.
Matumizi
ya Maendeleo yaliyopewa kipaumbele kwa kipindi cha miezi mitano ni pamoja na:
- Ununuzi wa ndege mbili za Serikali Shilingi bilioni 103.386 na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege 4 shilingi bilioni 91.533;
- Usambazaji wa umeme vijijini Shilingi bilioni 266.493;
- Ujenzi na ukarabati wa barabara Shilingi bilioni 335.931;
- Usambazaji wa maji vijijini na mijini Shilingi bilioni 65.2445;
- Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu Shilingi bilioni 210.758;
- Mfuko wa Reli Shilingi bilioni 42.404;
- Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma na Mwanza Shilingi bilioni 12.353;
- Ujenzi wa majengo ya utawala katika Wilaya mpya na Mamlaka za Serikali za Mitaa Shilingi bilioni 11.00;
- Ujenzi na ukarabati wa ofisi za Halmashauri Shilingi bilioni 30.10;
- Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo Tanzania bara Shilingi bilioni 9.0; na
- Uboreshaji wa miundombinu ya shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum Shilingi bilioni 2.5.
1.
Ulipaji wa
Madai mbalimbali
Katika
kipindi cha Julai – Novemba, 2016 madai yaliyohakikiwa ya jumla ya Shilingi
bilioni 318.556 yalilipwa, ambapo shilingi bilioni 183.714 ni kwa ajili ya
Wakandarasi na Wahandisi Washauri wa miradi ya barabara; Shilingi bilioni
42.951 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji; Shilingi bilioni 30.00 kwa ajili
ya mikataba ya ulinzi na usalama; Shilingi bilioni 25.00 kwa ajili ya miradi ya
umeme; Shilingi bilioni 15.439 kwa ajili ya wazabuni mbalimbali; shilingi
bilioni 10.00 kwa ajili ya madai ya watumishi; Shilingi bilioni 7.00 kwa ajili
ya matibabu nje ya nchi (Hospitali ya Apollo, India); Shilingi bilioni 3.150
kwa ajili ya Mtaalam Mwelekezi wa mipango miji ya jiji la Arusha na Mwanza; na
shilingi bilioni 1.302 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali ya
Serikali.
1.
Deni la
Taifa
Deni
la Taifa limeendelea kuongezeka na kufikia dola za Kimarekani milioni 21,087.9
mwishoni mwa mwezi October 2016, kutoka dola za Kimarekani milioni 19,861.1
mwezi Desemba 2015.
Deni
la nje liliongezeka kwa asilimia 3.4 na kufikia dola za Kimarekani milioni
16,407.6 mwezi October 2016 (sawa na asilimia 77.8 ya deni la taifa), kutoka
dola za Kimarekani milioni 15,863.9 mwezi Desemba 2015. Hii ilitokana na
kuongezeka kwa mikopo mipya pamoja na malimbikizo ya malipo ya madeni. Katika
deni hilo la nje, asilimia 83.0 ni deni la Serikali na taasisi za umma.
Deni
la ndani liliongezeka kufikia shilingi bilioni 10,089.3 mwishoni mwa mwezi
Octoba 2016 kutoka shilingi bilioni 8,597.0 mwezi Desemba 2015. Ongezeko hilo
lilitokana na Serikali kukopa kupitia dhamana na hati fungani kwa ajili ya kugharamia
bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, ikichangiwa pia na kupungua kwa misaada
na mikopo kutoka nje.
Deni
la Taifa ni himilivu: Pamoja na kuongezeka huko, deni la Taifa bado ni
himilivu. Uchambuzi wa Uhimilivu wa Deni uliofanyika mwezi Novemba 2016
unaonesha kuwa viashiria vya deni la nje na deni lote la umma viataendelea kuwa
chini ya ukomo wa uhimilivu katika kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda
mrefu. Uchambuzi unaonesha kuwa viashiria vyote vitaendelea kuwa chini ya ukomo
wa kimataifa hivyo deni la Taifa ni himilivu.
1.
Changamoto
Pamoja
na mafanikio hayo, changamoto kadhaa zilijitokeza zikiwemo:-
1.
Baadhi ya
wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutokuwa na mwamko wa matumizi ya
mashine za kielektroniki;
2.
Ukusanyaji
usioridhisha wa maduhuli ya Serikali;
3.
Kushindwa
au kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka
nje;
4.
Maombi ya
misamaha ya kodi; na
5.
Mahitaji
makubwa (yasiyowiana na hali halisi ya upatikanaji wa mapato) ya kuboresha
miundombinu hususan ya maji, reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara;
- MAENEO YANAYOLALAMIKIWA NA BAADHI YA MAGAZETI NA KWENYE MITANDAO
4.1
Kupungua kwa Ukwasi Kufuatia Uamuzi wa Serikali Kuzitaka Taasisi za Umma
Kufungua Akaunti za Mapato Benki Kuu
Uamuzi
wa Serikali kuzitaka taasisi za umma kufungua akaunti ya mapato Benki Kuu
utaendelea kubaki kama ulivyo. Kwa kifupi, fedha hizi za umma zilikuwa
zinatumika vibaya na Bodi za mashirika lakini pia zilitumika kuikopesha
Serikali fedha zake yenyewe kwa riba kubwa kupitia biashara ya dhamana na hati
fungani za Serikali. Kasoro hiyo iliondoa motisha kwa mabenki ya biashara
kupeleka huduma za kifedha vijijini na hata kukopesha sekta binafsi (crowding
out credit to the private sector).
Aidha,
ni vyema jamii ya Watanzania ikafahamu kwamba akaunti ambazo fedha za mashirika
zimehamishiwa Benki Kuu ni akaunti za kukusanya mapato tu. Akaunti za matumizi
bado ziko katika benki za biashara ili kuyawezesha mashirika kufanya malipo
kupitia akaunti hizo. Hivyo, bado benki za biashara ni kiungo muhimu kati ya
mashirika ya umma na watoa huduma kwa mashirika hayo. Hatua iliyochukuliwa na
Serikali inalenga kuzisukumu benki za biashara kuchukua hatua za ziada kupanua
huduma za kifedha hadi vijijini badala ya kujikita mijini zaidi kuhudumia
makampuni makubwa (corporate sector) na kufanya biashara katika soko la dhamana
na hati fungani za Serikali.
4.2
Mkikimkiki wa Ukusanyaji Kodi umekimbiza Wapangaji wa Majengo Marefu na
Kusababisha Biashara Nyingi Kufungwa
Taarifa
kutoka Mfuko wa Pensheni wa PPF zinaonesha kuwa kati ya majengo 15 inayomiliki
sehemu mbalimbali nchini, mtiririko wa wastani wa wapangaji uko kama ifuatavyo:
1.
Majengo
saba (7) yana wapangaji kwa asilimia 100 hadi kufikia Desemba 14, 2016;
2.
Jengo moja
(DICC – PPF Tower) kwa sasa halipangishwi bali linaendeshwa na PPF wenyewe kama
ukumbi wa mikutano;
3.
Jengo moja
(PPF Plaza – Arusha) ni jipya na idadi ya wapangaji imeshaanza kuongezeka
kutoka asilimia 34 mwezi Machi 2016 lilipofunguliwa hadi asilimia 39.1 Desemba
2016;
4.
PPF
Kijitonyama ina nyumba nne (4) na kati ya hizo, mbili tu zenye wapangaji. Hatua
za kutafuta wapangaji zinaendelea;
5.
PPF
Kaloleni Arusha ina nyumba 20 na mwenendo wa wapangaji ulikuwa ukipanda na
kushuka na katika kipindi kilichoishia Desemba 2016 umeongezeka kufikia
asilimia 75 kutoka asilimia 65 mwezi Juni 2016;
6.
Majengo
manne yaliyobaki (PPF Tower and Parking Arcade, PPF Plaza Mwanza, PPF House na
PPF Olerien Estate) idadi ya wapangaji ilipungua na kufikia wastani wa asilimia
78.5 kwa yote katika kipindi kilichoishia Desemba 2016 ikilinganishwa na
wastani wa asilimia 84.8 Juni 2016.
Aidha,
taarifa kutoka PSPF zinaonesha kuwa katika majengo manne (4) inayomiliki
imeweza kukodisha jumla ya futi za mraba 58,119.33 katika kipindi kilichoishia
Juni 2016 ikilinganishwa na futi za mraba 57,883.5 zilizokodishwa hadi Juni
2015, sawa na ongezeko la asilimia 0.4. Katika kipindi hicho kilichoishia Juni
2016, eneo lililokodishwa katika majengo ya Jubilee na PSPF Plaza lilipungua
kwa asilimia 4.7 na 2.7 kwa mtiririko huo wakati ambapo katika majengo ya HIP
na Ubungo Plaza kulikuwa na ongezeko la eneo lililopangishwa kwa asilimia 20.9
na 1.3 mtawalia.
Ni
dhahiri kuwa, kwa ujumla, kumekuwa na ongezeko la ushindani katika sekta ya
nyumba na majengo kufuatia kuongezeka kwa ujenzi unaofanywa na mashirika na
taasisi mbalimbali za umma na binafsi. Hali hii ilipelekea baadhi ya wamiliki
wa majengo hayo kubuni mbinu mbalimbali za kibiashara ikiwa ni pamoja na
kubadili matumizi ya majengo hayo na pia kuweka viwango vya kodi ya pango
vinavyoendana na hali halisi ya soko. Kwa kuzingatia takwimu za hapo juu ni
wazi kuwa madai kwamba mkikimkiki wa ukusanyaji kodi ndiyo umekimbiza wapangaji
hayana mashiko.
Madai
ya biashara nyingi kufungwa: Kwa upande wa madai ya biashara nyingi kufungwa
katika siku za karibuni, tumefuatilia na kwa kiasi fulani kuna ukweli.
Imebainika kwamba kasi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao imeongezeka kati
ya mwezi Agosti na Oktoba 2016. Mfano Ilala 1,076, Kinondoni 443, Temeke 222 na
Arusha 131. Aina ya biashara nyingi zilizofungwa ni katika sekta ya ujenzi na
biashara ya jumla na rejareja, na chache katika huduma za usafiri.
Hata
hivyo, sababu hasa zilizopelekea biashara hizo kufungwa hazijabainika kutokana
na ugumu wa kupata taarifa kutoka kwa wenye biashara zilizofungwa. Sababu za
mtu kufunga biashara yake zinaweza kuwa nyingi, ikiwemo, kushindwa kuingiza
bidhaa nchini bila kulipa kodi stahiki, kushindwa kulipa au kulipwa madeni,
kubadilisha aina ya biashara, kushindwa kusimamia biashara, gharama kubwa za
uendeshaji, wabia katika biashara kutoelewana au kutapeliana, kuibuka kwa
washindani wa kibiashara wenye nguvu au huduma bora zaidi n.k.
4.3
VAT Imekimbiza Watalii
Takwimu
rasmi kuhusu wageni walioingia nchini katika mwaka 2016 kwa ujumla zinaonyesha
kuwa idadi ya wageni imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2015 (Jedwali 4).
Hivyo madai kuwa watalii wameikimbia Tanzania kwa sababu ya VAT kwenye baadhi
ya huduma za utalii hayana msingi! Na kama nia ni kutolipa kodi na wakati
huohuo Serikali inadaiwa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utalii na
huduma nyingine kwa wananchi, hilo halikubaliki! Nawaalika wadau wa sekta ya
utalii waje wajenge hoja zenye mashiko wakati wa mapitio ya marekebisho ya kodi
kwa ajili ya bajeti ya 2017/18.
Jedwali
4a: Idadi ya Wageni walioingia Nchini 2015 – 2016
Mwezi
|
2015
|
2016
|
Badiliko %
|
Januari
|
98,710
|
99,763
|
1
|
Februari
|
88,939
|
91,519
|
3
|
March
|
77,841
|
93,096
|
20
|
Robo ya Kwanza
|
265,490
|
284,378
|
7
|
Aprili
|
67,447
|
76,679
|
14
|
Mei
|
81,538
|
76,155
|
-7
|
Juni
|
90,236
|
89,626
|
-1
|
Robo ya Pili
|
239,221
|
242,460
|
1
|
Julai
|
91,896
|
126,755
|
38
|
Agosti
|
142,885
|
121,321
|
-15
|
Septemba
|
100,829
|
121,279
|
20
|
Robo ya Tatu
|
335,610
|
369,355
|
10
|
Octoba
|
84,121
|
124,623
|
48
|
Jedwali
4b: Idadi ya Wageni waliongia nchini kupitia njia mbalimbali ;
Januari
– Septemba
KITUO
|
2015
|
2016
|
Badiliko %
|
JNIA
|
238,423
|
252,524
|
5.91
|
KIA
|
126,286
|
137,024
|
8.50
|
ZIA
|
109,738
|
139,284
|
26.92
|
Namanga
|
105,883
|
81,073
|
(23.43)
|
Kasumulo
|
9,871
|
12,006
|
21.63
|
Sirari
|
18,899
|
24,393
|
29.07
|
Zanz. Port
|
31,994
|
43,242
|
35.16
|
Kabanga
|
13,565
|
16,751
|
23.49
|
Manyovu
|
17,761
|
18,550
|
4.44
|
- MWELEKEO NA MATARAJIO HADI JUNI 2017
Kwa
kuzingatia mwenendo wa ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha Januari hadi September
2016, matarajio ni kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2016/17
unatarajiwa kufikia asilimia 7.2 kama ilivyokadiriwa awali.
Mfumuko
wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki kwenye tarakimu moja.
Thamani
ya shilingi inategemea kuendelea kuimarika kutokana na hatua zinazoendelea
kuchukuliwa na Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania.
Kwa
upande wa mapato, Serikali inakusudia kufanya yafuatayo hususan katika kuongeza
mapato ili kuweza kufikia lengo:
1.
Kusimamia
dhana ya kulipa kodi kwa hiari kupitia udhibiti wa matumizi ya
mfumo wa EFDs;
2.
Kuendelea
kuboresha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi hasa yale yanayotokana na michango
ya mashirika na wakala za Serikali;
3.
Kuendelea
na majadiliano baina ya serikali na wahisani ili kuhakikisha kwamba fedha za
misaada na mikopo zinapatikana kama ilivyopangwa;
4.
Kuendelea
kufanya uthamini wa mkupuo wa majengo ili kukusanya zaidi katika kodi ya
majengo;
5.
Kuendelea
kuboresha na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli; na
6.
Kuendelea
kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya
kielektroniki. Aidha, MDAs zinahimizwa kutumia mabenki katika kulipia maduhuli.
Aidha,
Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kusimamia matumizi kama
ifuatavyo:-
(i)
Kuendelea kusisitiza nidhamu katika utekelezaji wa bajeti
kama ilivyoidhinishwa kwa kuzingatia
Sheria ya Bajeti ya mwaka
2015;
(ii)
Kuendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa kuhakikisha
kuwa mgawo wa fedha utaendana na upatikanaji wa mapato;
(iii) Kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kama kupunguza
safari za nje zisizo na tija, matumizi
katika sherehe za kitaifa pamoja na
makongamano.
- HITIMISHO
Ninapohitimisha
maelezo yangu naomba kusisitiza yafuatayo:
Kwanza:
napenda kuwahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali ya awamu ya Tano
inathamini sana mchango wa Wafanyabiashara katika Maendeleo ya nchi yetu.
Milango ya serikali ipo wazi kwa wale wote wenye hoja zenye maslahi kwa Taifa
letu. Wizara ya Fedha na Mipango imekwisha toa tangazo kwa Watanzania na wadau
wote wa kodi kuwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya kodi kwa ajili ya
uchambuzi na kufikiriwa kuingizwa katika mapendekezo ya mabadiliko ya kodi
katika bajeti ijayo. Ninawaomba wadau wote kuitumia vizuri fursa hiyo ili
tupate mapendekezo mazuri ya kuboresha mfumo wetu wa kodi na kutupatia mapato
zaidi ya kuendeleza nchi yetu.
Pili:
Napenda kutoa rai kwa Watanzania wenzangu kuhakikisha kuwa tunadai risiti za
EFD kila tunaponunua bidhaa au huduma kama Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyokwisha kuagiza. Yeyote
asiyetoa risiti na asiyedai risiti ajue anatenda kosa na anasaliti jitihada
zetu za kuijenga Tanzania mpya. Aidha, ningependa kusisitiza kwa wale wote
wenye mashine za EFD wazitumie ipasavyo kwa kila muamala wanaoufanya. Kuna
tabia ambayo imezuka ya kusingizia kuwa mashine imeharibika au kutoa risiti ya
EFD kwa mteja anayeidai tu. Wale wote wenye tabia hii wanahujumu maendeleo ya
nchi yetu na ninawataka waache mara moja! Nimewaagiza TRA kufanya kaguzi za
kushtukiza na kuwashughulikia ipasavyo wale wasiotaka kutii maelekezo ya
Serikali kwa mujibu wa sheria za nchi.
Napenda
nisisitize kuwa Tanzania mpya ambayo wote tunaitamani iko mikononi mwetu!
Lakini ili tufike huko lazima tufanye kazi kwelikweli – iwe ni kazi ya
kuajiriwa au kujiajiri katika kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara au huduma au
kumiliki viwanda (vidogo, vya kati na vikubwa)!! Aidha, lazima kila mmoja wetu
alipe kodi stahiki kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania yetu! Tuitikie wito wa
Rais wetu kwa vitendo ambaye amedhamiria kujenga Tanzania mpya ili
kuwaondoa Watanzania kwenye lindi la umaskini haraka. Kulipa kodi ndiyo njia ya
uhakika ya kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora zaidi (upatikanaji wa maji,
elimu, afya, umeme, barabara, ulinzi & usalama) kwa wananchi wake. Uamuzi
huu unahitaji kuachana na mazoea, kujitoa (sacrifice) na kufanya kazi kwa bidii,
nidhamu na uadilifu. Tunataka uchumi ambao wananchi wengi wananufaika nao,
uchumi ambao utajengwa kwa kufanya kazi siyo uchumi wa ujanja ujanja (mission
town), kukwepa kodi au wizi wa mali na fedha za umma.
Tatu:
Wanahabari kwa ujumla mnafanya kazi nzuri sana. Nawaomba mwendelee hivyo na
hasa nikiwasihi mtumie weledi na mjielekeze kuwajuza Watanzania kuhusu mifano
mizuri ya maendeleo hapa nchini na hata katika nchi nyingine lakini wakati huo
huo mtangulize maslahi ya Taifa letu kwanza. Hata hivyo, yapo magazeti fulani
ambayo consistently yanajielekeza kutoa taarifa za kupotosha na kuifanya jamii
ihamaki! Nawaomba: Epukeni kuwa vipaaza sauti vya nyimbo za watu wachache wenye
maslahi binafsi (wawe wanasiasa, wafanyabiashara, au wafanyakazi) waliozoea
“upigaji”! Punguzeni uandishi wa kuuza magazeti (sensationalism) na uchambuzi
wa mambo kijuujuu! Pimeni taarifa mnazoziandika ili msiwanufaishe
washindani wa nchi yetu kiuchumi (kibiashara au kiuwekezaji) au kuchafua sura
nzuri ya Tanzania!!
Nimalizie
kwa kuwahakikishia Watanzania wote kwamba madai ya baadhi ya magazeti
siku za karibuni kuwa uchumi wa Taifa una hali mbaya siyo ya kweli. Hata gazeti
moja la leo limeandika kuwa “Ripoti ya Uchumi Yashtua”!! Ukweli ni kuwa kama
Taifa tumeendelea kupiga hatua nzuri katika maeneo mengi ya uchumi japo yapo
maeneo machache ambayo yana changamoto, na Serikali inaendelea kuyafuatilia kwa
karibu ili kuyatafutia ufumbuzi. Afya ya uchumi wetu bado ni nzuri na
inatarajiwa itaendelea kuwa ya kuridhisha katika mwaka ujao 2017.
NAWATAKIA
WOTE HERI YA MWAKA MPYA 2017
UWE
KWELI MWAKA WA HAPA KAZI TU!!
ASANTENI
KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment