Mkurugenzi
Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko
(katikati), akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es
Salaam leo, wakati akitoa taarifa kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa
ukimwi katika mkutano wa kujitambulisha kwao tangu ateuliwe na Rais
Dk.John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7 mwaka huu. Kutoka kushoto ni
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Muitikio ya Kitaifa, Dk.Hafidhi
Amri, Mkuu wa Kitengo cha Sheria Tacaids, Elizabeth Kaganda na Mkurugenzi wa
Habari na Ulaghibishi, Jumanne Issango.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti
Ukimwi Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko (kushoto), akisisitiza jambo
kwenye mkutano huo. Kulia ni Mkurugenzi wa Habari na Ulaghibishi, Jumanne
Issango.
...............................
MAAMBUKIZO
Mapya ya VVU na Ukimwi yameshuka nchini kwa zaidi ya asilimia 20 kati
ya mwaka 2010 na 2015 imefahamika.
Hayo
yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi
Tanzania (Tacaids) Dk.Leonard Maboko wakati akitoa taarifa kwa waandishi
wa habari katika mkutano wa kujitambulisha kwao tangu ateuliwe na Rais
Dk.John Magufuli kushika nafasi hiyo Julai 7 mwaka huu.
Alisema
maambukizo mapya ya VVU yaliyokadiriwa kuwa watu milioni 2.1 kwa mwaka
2015 Duniani kote wakati maambukizo mapya yameshuka kwa asilimia
50 miongoni mwa watoto duniani.
Alisema
watoto 290,000 wapya waliambukizwa mwaka 2010 na watoto
150,000 waliambukizwa mwaka 2015 ambapo maambukizo mapya kwa watu wazima
hayajashuka tangu 2010 duniani.
Katika
hatua nyingine Dk. Maboko alisema Tafiti zimeonesha kuwa wanawake
ndio waathirika wakubwa wa maambukizo ya VVU kwa upande wa Tanzania Bara ukilinganisha
na wanaume.
Alisema
maambukizo VVU kwa upande wa Tanzania Bara ni asilimia 5.3
wanawake wakionesha kuathirika zaidi kwa asilimia 6.2 ukilinganisha na
wanaume ambao ni asilimia 3.8.
“Katika
utafiti huo wa mwaka 2011 na 2012 ulionyesha kuwa Mkoa wa Njombe
ulikuwa na kiwango kikubwa cha maambukizo ukiwa na asilimia 14.8
ukifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mbeya kwa asilimia 9″ alisema
Dk.Maboko.
Dk.Maboko
alisema Mkoa wa Manyara ulikuwa na kiwango kidogo cha maambukizo ya asilimia
1.5 lakini takwimu za ndani ya mkoa huo eneo la Mirelani kwenye mgodi wa
Tanzanite maambukizo ya VVU yalikuwa ni asilimia 16 kiwango ambacho ni cha
juu ya Mkoa wa Njombe.
Dk. Maboko
aliwaomba wananchi kote walipo kutobweteka kwa mafanikio yaliyo ya mapambano
dhidhi ya VVU na ukimwi na kuwa yawe endelevu hata katika maeneo au mikoa
ambako kuna maambukizo kidogo ya VVU.
Alisema
kama nchi tunatakiwa kuweka nguvu nyingi kifedha na kimkakati katika maeneo na
makundi yenye kiwango kikubwa cha maambukizo ya VVU ikiwa ni pamoja na
kuimarisha utafiti na ukusanyaji wa takwimu za VVU na Ukimwi ili tuendelee
kubaini na kupanga mipango dhidi ya ugonjwa huo inayoongozwa na takwimu.
Aliongeza
kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu mapambano dhidi ya Ukimwi
(UNAIDS) limeweka malengo ya muda wa kati ya tisini tatu (90-90-90). 90 ya
kwanza ikimaanisha asilimia tisini ya watu wote wanaokisiwa kuwa na VVU kujua
hali zao na 90 ya pili ikimaanisha kuwa asilimia tisini ya waliobainika
kuwa na VVU kuanza kutumia dawa za kupunguza makali
ya VVU
(ARV) mara moja na 90 ya tatu ya walioanza dawa waweze kuwa na ufubazo endelevu
wa virusi vya ukimwi mwilini mwao.
Dk. Maboko
alitoa mwito kwa wananchi, Taasisi za kijamii, Serikali, watu binafsi na
makampuni ya kibiashara kuchangia mfuko wa udhamini wa masuala ya ukimwi (AIDS
TRUST FUND-ATF) ulioanzishwa na serikali ili kuondokana na utegemezi kwa
wafadhili.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment