Friday, December 16, 2016

AZAM FC YATAMBULISHA WACHEZAJI WAPYA CHAMAZI.

kikosi-aza
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo imetambulisha nyota wapya sita waliosajiliwa kwenye usajili wa dirisha dogo uliofungwa usiku wa kuamkia leo.

Zoezi hilo lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Azam FC walikuwemo kwenye zoezi hilo, wakongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu Abdul Mohamed, Meneja wa timu, Phillip Alando, Ofisa Habari, Jaffar Idd pamoja na Kocha Mkuu Zeben Hernandez.

Wachezaji wapya waliotambulishwa ni beki Yakubu Mohammed (Aduana Stars), kiungo mkabaji Stephan Kingue Mpondo (Coton Sports), mawinga Enock Atta Agyei (Medeama), Joseph Mahundi, washambuliaji Yahaya Mohammed (Aduana Stars) na Samuel Afful (Sekondi Hasaacas).

Akizungumza wakati akitambulisha nyota hao, Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, alisema kuwa Yakubu ameingia kuziba pengo la Pascal Wawa aliyeondoka baada ya kumaliza mkataba wake huku pia Mpondo akiongeza nguvu kwenye eneo la kiungo mkabaji baada ya kuondoka kwa wachezaji wawili Michael Bolou na Jean Mugiraneza.

Alisema kuwa wengine walioingia kwenye usajili huo ni washambuliaji Afful na Yahaya ambaye ni mzoefu, wakiziba pengo la Gonazo Ya Thomas na Francisco Zekumbawira walisitishiwa mikataba yao.

Hivyo orodha ya wachezaji wapya wa kigeni wa Azam FC inayotambulika hivi sasa, ni mabeki Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Yakubu, kiungo Mpondo, kiungo mshambuliaji Agyei, washambuliaji Yahaya, Afful.

Aidha Azam FC imewatoa kwa mkopo wachezaji wake saba wa kikosi cha vijana waliojiunga na timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), ambao ni Omary Wayne, Joshua Thawe (Friends Rangers), Rajab Odasi, Yohana Mkomola (Ashanti United), Abbas Kapombe, Godfrey Elias (Polisi Dar es Salaam) na Mohamed Sadalah (Mbeya Warriors).

Matarajio makubwa VPL, CAF
Kawemba pia alisema kuwa wanatarajia mabadiliko makubwa kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), katika kucheza mpira, kiwango, matokeo ya uwanjani kutokana na aina ya usajili uliofanywa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zeben Hernandez, kupitia mapendekeo aliyoyatoa kwa uongozi.

“Kwa sababu timu ni ya kwake na mapendekezo kayaweka mwenyewe na usajili kafanya mwenyewe na sasa yupo na ameuona mpira ulivyo hapa nchini,” alisema.

Katika hatua nyingine, bosi huyo alisisitiza kuwa bado malengo yao makubwa ni kutwaa ubingwa wa ligi hiyo na Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) pamoja na kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Zeben na matarajio makubwa
Naye Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, akizungumza kwa upande wake alisema kuwa jambo kubwa walilopanga kurejea nalo kwenye mzunguko wa pili ni kubadilisha mpira uliokuwa ukichezwa kwenye mzunguko wa kwanza pamoja na matokeo yaliyokuwa yakipatikana.

“Mimi na benchi langu la ufundi tunatambua ya kuwa Azam FC si timu ndogo ni timu kubwa, malengo ambayo yapo kwa upande wetu ni kubadilisha mpira uliokuwa ukichezwa raundi ya kwanza pamoja na kubadilisha matokeo yaliyokuwa yakipatikana raundi ya kwanza na ndio maana tumeleta wachezaji wa kuongeza nguvu.

“Kikubwa tutajitahidi kadiri iwezekanavyo kuweza kupata ushindi na ikiwezekana si tu kwenye ligi bali hata michuano mingine tunayoshiriki, jitihada tunazofanya kama benchi la ufundi tunaamini ya kuwa Azam FC itafika kwenye sehemu moja nzuri kuliko ambavyo watu wanafikiria,” alimalizia.

No comments:

Post a Comment