WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahimiza wakazi wa vijiji saba wilayani
Ruangwa waharakishe kufyatua matofali ili waanze ujenzi wa zahanati na yeye
atawachangia mabati.
Ametoa ahadi hizo leo (Jumatano, Desemba 28, 2016) wakati akizungumza na
wananchi wa vijiji vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi
na Chibula na viongozi wa wilaya ya Ruangwa, mkoa wa Lindi ambako anapita
kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo. Waziri Mkuu
yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
Amesema sera ya Serikali ni kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha
afya kwa kila kata na kwamba umefika wakati wa kuanza kutekeleza kaulimbiu ya
jimbo hilo inayosema “Ruangwa kwa maendeleo, inawezekana.”
Katika kuhimiza ujenzi wa zahanati hizo, amechangia mabati kati ya 50 na
150 kwa kila kijiji na akawahimiza wahakikishe wanakamilisha mapema ujenzi wa
maboma ili aweze kutimiza ahadi yake ya mabati.
Amesema katika awamu iliyopita, alikazania sana suala la elimu kwa
kusimamia ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa kwenye shule ambazo hazikuwa
na madarasa ya kutosha. Pia alisimamia ukarabati wa majengo chakavu katika
baadhi ya shule.
“Kuanzia awamu hii na miaka minne iliyobakia, mkakati wangu ni kusimamia
upatikanaji wa maji safi na suala la kuboresha sekta ya afya katika jimbo zima
nikishirikiana na uongozi wa Halmashauri yetu,” amesema.
Pia amemwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Japhet Simeo ahakikishe
anawasiliana na viongozi wa vijiji hivyo ili wapatiwe michoro ya ramani
zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.
Wakati huohuo, Mkurugenzi wa kampuni ya Umemejua ya Baraka Solar
Specialist, Bw. Ansi Mmasi amesema atajitolea kuweka mfumo wa umemejua wa watts
300 pamoja na nyaya zake kwenye zahanati inayotaka kujengwa kwenye kijiji cha
Namilema.
Alisema anaishukuru kwa kuwapa kazi makandarasi wazawa na akawataka
wakandarasi wenzake watumie vifaa bora na imara pindi wanapopewa kazi ya kutoa
huduma na taasisi mbalimbali ikiwemo halmashauri na idara za Serikali.
“Tujitahidi kufanya kazi hizi kwa weledi na tutumie vifaa bora na imara
ili watu wanaotarajia huduma zetu waweze kuridhika na kuendelea kuwa na umani
na wakandarasi wazawa kwamba tunaweza kufanya kazi nzuri na zenye ubora
unaotakiwa,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw.
Fakihi J. Bakili alisema atachangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa
zahanati hiyo ya kijiji cha Namilema.
Pia alichangia mifuko 100 kwenye zahanati
ya kijiji cha Manokwe na mifuko mingine 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya
kijiji cha Chikundi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, DESEMBA 28, 2016.
No comments:
Post a Comment