Waziri wa Madini Doto Biteko kushoto
akimuelekeza jambo Mkuu wa jeshi la Polisi wa kituo cha Bugarama.
.................................
Na Tito Mselem, Kahama.
Waziri wa Madini Doto Biteko
amekifunga kiwanda bubu cha kuchenjua madini ya dhahabu kilichofunguliwa
kinyemela katika Kijiji cha Bunanga kata ya Bugarama Halmashauri ya Msalala
Wilayani Kahama.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na
Simoni Shule kipo katikati ya makazi ya watu ambapo kinahatarisha maisha ya
watu na kuharibu mazingira baada ya kutiririsha kemikali za sumu kwenye makazi
ya watu.
Waziri Biteko alisema, licha ya
serikali kuboresha Sekta ya Madini kwa wachimbaji na wafanyabiashara wadogo wa
madini nchini, imebainika kuwa wapo ambao wamekuwa wakifanya shughuli za
uchenjuaji wa madini ya dhahabu ikiwemo kuanzisha viwanda bubu kinyume na
taratibu na kuikosesha serikali mapato.
Hayo yalibainishwa Januari Mosi mwaka
2020 na Waziri Biteko baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika kijiji cha
Bunanga kata ya Bugarama Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama na kubaini
kiwanda bubu cha kuchenjua madini ya dhahabu kilichopo katikati ya makazi ya
watu.
“Kiwanda hiki kipo hapa katika nyumba
hii kwa kipindi cha zaidi ya miezi 7 kikiendelea kufanya kazi bila kufuata
Sheria na Taratibu zilizopo na kuipotezea Serikali mapato mengi, hivyo
tutachukua hatua kali za kisheria kwa mmiliki wa mtambo huu ili iwe fundisho
kwa wengine wenye tabia chafu kama hii,” alisema Biteko.
Aidha, Waziri Biteko aliwataka
viongozi wa vijiji na mitaa wilayani humo kuhakikisha wanawafichua
wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara haramu ya madini ambazo zinafanyika
katika makazi ya watu kinyume na Sheria na kuikosesha Serikali mapato.
“Niwaagize viongozi wote wa ngazi
zote Nchi nzima kuhakikisha mnasimamia na kuthibiti vitendo vya biashara haramu
ya madini ambavyo vinaendelea kufanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu katika
maeneo mbalimbali nchini, alisema Waziri Biteko.
Wakati huo huo, Waziri Biteko
aliliagiza jeshi la polisi la Halmashauri ya Msalala kumkamata na kumuhoji
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Bunanga Kajanja Kajanja na Mke wa mwenye nyumba
iliyobainika kuwa na mtambo wa kuchenjulia dhahabu unaomilikiwa na Simoni Shule
kuhusiana na
kuhusishwa na tukio hilo.
Katika ziara hiyo mifuko zaidi ya 44
ya kemikali zinazotumika kuchenjulia madini ya dhahabu (Kaboni) imekamatwa
katika kiwanda hicho inayodhaniwa kuwa na madini ya dhahabu, huku mashine hiyo
yenye uwezo wa kubeba kilo 500 za Kaboni ikiwa tayari imewekewa
mzigo kwaajili
ya kuanza kazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji
cha Bunanga Januari Luhamba, alisema, baada ya kugundua shughuli zinazofanywa
na kiwanda hicho katikati ya makazi ya watu, alitoa taarifa kwa mamlaka za
kisheria ikiwemo polisi kuhusiana na uwepo wa kiwanda hicho katika eneo
lake lakini hakuona hatua yoyote iliyochukuliwa kwa wahusika.
“Kiwanda hiki kipo katika nyumba hii
kwa muda mrefu sasa, kuna vijana wageni wengi wamekuja kufanya kazi ya
kuchenjua dhahabu katika kiwanda hiki, viongozi wote wa eneo hili wanajua
tumelalamika sana kuhusiana na kumwagwa ovyo kwa maji yenye kemikali kwenye
makazi yetu,”
alisema.Luhambo.
Maafisa wa Madini wa Wilaya ya Kahama
wakiweka sildi katika mlango wa kiwanda bubu cha kuchenjulia madini ya dhahabu.
Waziri wa Madini Doto Biteko kulia
akimuelekeza mwenyekiti wa Kijiji cha Bunanga January Luhamba sehemu ya
kusaini.
Waziri wa Madini Doto Biteko kushoto
akichungulia chumba kilichosimikwa mtambo wa kuchenjulia madini ya dhahabu,
kulia ni mwenyekiti wa Kijiji cha Bunanga Luhamba.
Baaadhi ya mifuko iliyojazwa kemikali
za kuchenjulia dhahabu. (kaboni)
Waziri wa Madini Doto Biteko kulia akiwa
amebeba furushi la kemikali za kuchenjulia madini ya dhahabu (kaboni) kushoto
ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Bunanga Kajanja Kajanja.
No comments:
Post a Comment