Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya Kimila Bibi Dafrosa Komba wakati
wa zoezi la kutoa hati kwa wakulima wadogo wa kijiji cha Litoa katika wilaya ya
Songea vijijini mkoani Ruvuma jana. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Songea
Pololeti Mgema.
......................................
Na Munir Shemweta, WANMM SONGEA.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekabidhi hati mia moja za Kimila kwa
wakulima wadogo wa kijiji cha Litoa kilichopo katika jimbo la Peramiho wilaya
ya Songea Vijijini mkoani Ruvuma na kuwataka wamiliki wake kuzitunza na
kuzitumia hati hizo kujiletea maendeleo.
Akizungumza wakati wa kuwakabidhi
hati hizo katika kijiji cha Litoa wilaya ya Songea vijijini akiwa kwenye
shughuli za kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi ya ujenzi ya
Shirika la Nyumba la Taifa katika mikoa ya kusini jana, Naibu Waziri Mabula
aliwataka wakulima waliokabidhiwa hati kutouza ardhi zao kwa nia ya kupata
fedha za haraka.
‘’Mmepiwa msikimbilie kuuza ardhi
bila kufuata taratibu kwa tamaa ya kupata fedha za haraka maana mkiuza mnaweza
kupunjwa fedha’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaandaa
mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji ili kuwa na salama za miliki za
ardhi zilizoainisha maeneo ya shule, soko, maeneo ya kuabudia, viwanja vya michezo
pamoja na maeneo ya uwekezaji.
Dkt Mabula alizitaka pia halmashauri
kuandaa maeneo ya uwekezaji sambamba na kuhaulisha maeneo ili kuwa rahisi kwa
Mwekezaji atakayekuja kuwekeza katika sekta mbalimbali na kusisitiza kuwa ili
kuwaendeleza wananchi kiuchumi ni lazima ardhi ipimwe na kufanyiwa mpango wa
matumizi bora ya ardhi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Songea Vijijini Pololeti Mgema aliupongeza Mtandao wa Vikundi vya Wakulima
Tanzania (MVIWATA) kwa juhudi kubwa iliyofanya kufanikisha wakulima wadogo
kupata hati miliki za kimila na kubainisha kuwa wilaya yake imejifunza bila
kushirikisha wadau zoezi la kuwapatia hati wakulima wadogo lingechukua muda
mrefu.
Naye Mratibu wa MVIWATA katika
mkoa wa Ruvuma Laila Haji alisema Asasi yake iliona umuhimu wa wakulima wadogo
kuwa na salama za miliki za mashamba yao na ndiyo maana ikafanya juhudi kwa
kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Songea ili kuwapatia hati wakulima wa
kijiji cha Litoa.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa
iliyopo kwa wakulima na wananchi kwa ujumla katika suala la hati miliki za
ardhi ni elimu ndogo kuhusiana na masuala hati za ardhi, mfumo dume kwa
wanawake kumiliki ardhi pamoja na migogoro ya wakulima na wafugaji.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alitembelea mradi wa
ujenzi wa Ofisi na nyumba za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) uliopo
Mpepo wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma.
Mradi huo pamoja na miradi mingine ya
ujenzi wa nyumba na ofisi za TFS katika maeneo mbalimbali nchini unajengwa na
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi akiangalia nondo zinazotumika kwenye ujenzi wa mradi wa nyumba na ofisi
za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaotekelezwa na Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) katika eneo la Mpepo wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma jana
wakati akikagua mradi huo. Kulia ni mhandisi wa Mradi kutoka NHC Omar
Chitawala
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi akifafanua jambo wakati akikagua mradi wa ujenzi wa nyumba na Ofisi za
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unaofanywa na Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) kwenye shamba la miti la Mpepo lililopo wilaya ya Nyasa mkoani
Ruvuma jana. Kushoto ni Meneja Mawasiliano wa NHC Muungano Saguya na aliyekunja
mikono ni Mhandisi wa Mradi kutoka Omar Chitawala.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi
waliokabidhiwa Hati za Kimila wakati wa zoezi la kutoa hati katika kijiji cha
Litoa wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni
Mkuu wa wilaya ya Songea Pololeti Mgema.
No comments:
Post a Comment