Wednesday, January 29, 2020

VULU ATAKA MICHEZO KUHAMASISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA.

Na Omary Mngindo, Kisarawe.  

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynabu Vulu, amewaonba viongozi wa Vijiji na Vitongohi mkoani hapa kuandaa mashindano madogo ya kuhamasisha zoezi la uboreshaji wa daftari la wapigakura.

Vulu ametoa rai hiyo akiwa katika Kijiji cha Kisangile Kata ya Marui wilaya ya Kisarawe mkoani hapa, alipoambatana na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wanawake wa UWT Sophia Gunia, ambapo amesema michezo ina nafasi kubwa ya kufikisha ujumbe kwa wananchi.

Alisema kuwa katika Mkoa wa Pwani kuanzia Februari Mosi mpaka saba mwaka huu kutakuwa na zoezi la uboreshaji wa daftari la wapigakura, litakalodumu kwa siku saba, hivyo kutokana na uchache wa siku amewaomba viongozi kuandaa mashindano hata ya kuwania sabuni.

"Kutokana na uchache wa siku za uboreshaji wa taarifa za wakazi kwenye daftari hilo, ningewaomba viongozi katika maeneo yao waandae mashindani madogo yatakayotumika kufikisha ujumbe kwa wananchi wetu, wajiandikishe ili wasipoteze sifa za kushiriki zoezi la kuchagua au kuchaguliwa," alisema Vulu.

Kwa upande wake Sophia amewataka wakazi wilayani hapa kutopuuzia zoezi hilo kwani ni la siku chache, hivyo wasipoteze nafasi hiyo muhimu kwa mustakbali wa nchi yetu, kwani ni fursa ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi za kisiasa.

"Tumekuwa na tabia ya kupuuzia maagizo yanayotolewa na serikali, tunao mfano mojawapo ni huu wa kitambulisho cha Taifa, zoezi hili lilitangazwa kwa muda mrefu lakini nananchi wamepuuzia lakini kwa sasa tunashuhudia wanavyohangaika," alisema Mwenyekiti huyo.

Nae diwani wa Kata ya Marui Selemani Mfaume amesema kuwa watafanya juhudi kubwa za kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu hiyo, ili isije ikajitokeza kama zoezi la kitambulisho cha Taifa.

"Ushauri wa mashindano nimeupokea nitakaa na viongozi wangu ngazi za vijiji kuandaa japo mashindano ya kuwania sabuni tutakayoyatumia kuwatangazia wananchi kuhusiana na uboreshaji wa daftari la wapigakura," alisema Mfaume.

No comments:

Post a Comment