Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akifungua
mkutano wa wa wadau wa kujadili mpango wa kuhamasisha matumizi ya Gesi Asilia
nchini, uliofanyika Jijini DSM.
......................................
Na Zuena Msuya, DSM
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu,
amesema tayari Serikali imekamilisha mpango wa awali wa kusambaza gesi kwenye
Mikoa mitano ili kuhakikisha kuwa Tanzania inatumia rasilimali hiyo
inayochimbwa nchini katika kuimarisha uchumi wa viwanda.
Mgalu alisema hayo wakati
akifungua mkutano wa wadau wa kujadili mpango wa kuhamasisha matumizi ya Gesi
Asilia nchini, uliofanyika Jijini DSM, Januari 17,2020.
Mgalu alisisitiza kuwa mpango huo ni
matokeo ya utafiti wa miaka mitatu, uliofanywa na Serikali kwa ufadhili wa
Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA).
Aliitaja Mikoa hiyo kuwa ni
Arusha, Dodoma, Tanga, Kilimanjaro na Morogoro.
Aidha alieleza kuwa lengo la serikali
ni kuhakikisha mikoa yote Tanzania inapata nishati hiyo kwa matumizi
mbalimbali.
“Tanzania tumegundua gesi asili yenye
ujazo wa futi trilioni 57 hii sasa tunaitengenezea mkakati wa matumizi yake.
Kwa mijiibu wa takwimu zinaeleza kuwa
mpaka sasa gesi asilia inayochiimbwa chini inazalisha Megawati 892.72 sawa na
57 % ya Megawati zote zinazozalishwa.
Aliweka wazi kuwa Gesi Asilia
inatumika pia kwenye magari, tumeanza hapa Dar es Salaam ambapo magari
takribani 200 yanatumia gesi na miundombinu ya kusambaza gesi hiyo inaendelea
kuboreshwa ili kuwasogezea huduma watumiaji, na hii ndio maana hasa ya utafiti
huu.
“Gesi asilia inatusaidia pia kutunza
mazingira hasa kwenye kupikia ambapo mpaka sasa Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC), limesambaza miundombinu ya gesi ya kupikia majumbani katika
Mikoa ya Lindi, Mtwara, Dar es Salaam na Pwani,” alisisitiza Mgalu.
Kuhusu matumizi ya gesi viwandani
Mgalu alisema viwanda zaidi ya 50 vimeunganishwa na gesi asilia.
“Huu ni mradi mkubwa Sana utakuwa wa
muda mrefu pia hadi kufikia mwaka 2046 tangu kuanza kwa mradi huu mwaka 2017.
Kwa upande wake Kamishna wa
Petroli na Gesi wa Wizara ya Nishati , Adam Zuberi alisema Tanzania ipo kwenye
wakati sahihi hivyo jitihada za makusudi zinafanyika kufikisha gesi asilia
kwenye mikoa yote Tanzania.
“Tupo katika Muda muafaka wa utafiti
huu unaolenga kuhakikisha kwamba Mikoa yote nchini inapata na kutumia gesi
asilia kwa njia bora na sahihi,” alisema Zuberi.
Mshauri wa Taasisi ya Nishati na
Uchumi kutoka Japan, Kensuke Kanekinyo alisema awamu ya kwanza ya mradi huo
imetumia Dola Milioni mbili za Marekani kwa miaka mitatu.
Alisema gharama za mradi wote ni Dola
milioni 250 zitakazotumika kupeleka gesi mikoa yote ya Tanzania.
Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi akizungumza
na waandishi wa wabari wakati wa mkutano wa wadau wa kujadili mpango wa
kuhamasisha matumizi ya Gesi Asilia nchini, uliofanyika Jijini DSM
Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu( kulia) na
Kamishna wa Petroli na Gesi wa Wizara ya Nishati, Adam Zuberi wakifuatilia mada
zilizokuwa zikitolewa wakati wa mkutano wa wadau wa kujadili mpango wa
kuhamasisha matumizi ya Gesi Asilia nchini, uliofanyika Jijini DSM.
Naibu wa Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
(katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi kutosha Shirika
la Maendeleo la Japani ( JICA), Wakuu wa Taasisi ya Nishati na Uchumi kutoka
Japani, baaadhi ya Viongozi Wakuu wa Wizara na Taasisi zilizochini yake, baada
ya Naibu Waziri huyo kufungua mkutano wa wadau hao uliofanyika Jijini DSM.
No comments:
Post a Comment