Sunday, January 19, 2020

MWENYEKITI WA KIJIJI ATUHUMIWA KUUZA ARDHI CHALINZE.

 Mwenyekiti wa kiji cha Tukamisasa, Kata ya Ubena Amani Msasu akijitetea kwenye Mkutano wa hadhara kuhusu tuhuma za yeye kuuza ardhi ekari 400, pembeni yake kushoto ni Afisa Tarafa, Tarafa ya Chalinze, Thomas Molel.
...............................................

Na Omary Mngindo, Chalinze

WAKAZI wa Kijiji cha Tukamisasa Kata ya Ubena Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani, wanamtuhumu Mwenyekiti wao Amani Msasu wakidai ameuza ardhi ekari 400.

Katika Mkutano Maalumu ulio ombwa na wananchi kwa lengo la kutoa tamko la kumkataa Mwenyekiti huyo, chini ya Afisa Tarafa, Tarafa ya Chalinze, Thomas Molel, wakazi hao walisema kuwa wakimtuhumu Msasu kuwa ameuza ardhi hiyo mali ya kijiji.

Shujaa Theophil wa kwanza kuzungumza ambapo alisema Msasu kabla ya nafasi hiyo alikuwa anauza ardhi, na kuwa alipochaguliwa akishirikiana na watu hao wamefanya mpango wa kuwauzia taasisi ya VICOBA ya Dar es Salaam ekari 400 mali ya wanakijiji.

"Hatuna imani na Mwenyekiti, ana mpango wa kuuza ardhi yetu eka 400 kwa kikundi cha VICOBA kinachotokea Dar es Salaam, mara mbili tumevamiwa na magari yakiwa na wanachama wamevalia sare wakisema wamekuja kuangalia ardhi yao," alisema Theophil.

Mkazi Fatuma Matitu alisema kuwa tuhuma hizo kwa Mwenyekiti hazina ukweli, na kwamba zinalenga kumchafua, huku akisema kuwa hiyo ardhi inayodaiwa imeuzwa iko salama.

Machaku Bunga aliuambia mkutano huo kuwa Msasu anapotoshwa na baadhi ya wakazi wanaomzunguka wakijihusisha na uuzwaji wa ardhi kijiiini hapo, na kwamba alishawahi kumwita kwa lengo la kutaka kumtaadhalisha juu ya hilo.

"Nilimuita Msasu kwa lengo la kutaka kumtaadharisha kuhusiana na watu waliomzunguuka ambao wanajulikana sana hapa kijijini kwa uuzaji wa ardhi za wananchi, lakini alinipuuza," alisema Machaku.


Nae mkazi Godian Mazoezi alisema kuwa wanakijiji hawana imani na Mwenyekiti huyo, kwani ameonesha hatokuwa na msaada kwa wananchi, na hiyo inatokana na dhamira yake ya kutaka kuuza ardhi hiyo mali ya wana-Tukamisasa.

Akitoa utetezi mbele ya Afisa Tarafa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, Msasu alisema kwamba yeye amewahi kuuza ekari 30 za ardhi kijijini hapo ambazo ni mali ya wanafamilia na si kwamba ameuza ekari 400 mali ya kijiji kama inavyodaiwa.

"Hata mimi kuna siku nikiwa hapa kijijini nimewaona wanachama wa SACCOS kutoka Dar es Salaam wakiungana na baadhi yao wakazi wa hapa Tukamisasa wakitaka waoneshwe ardhi ambayo wanadai kuinunua, nilishangazwa na hilo," alisema Msasu.

Akihitimisha mkutano huo, Afisa Tarafa, Tarafa ya Chalinze, Thomas Molel alianza kutoa elimu ya ardhi huku akisema kijiji kina mamlaka ya kuuza mwisho ekari 50 tu, na kwamba zaidi ya hapo wenye mamlaka ya kuidhinisha malipo ni ngazi ya wilaya.

"Kama ardhi ni mali ya familia lazima kuwepo na muhtasari wa wanafamilia wakikubaliana juu ya uuzwaji huo, kisha unafikishwa kwenye mkutano mkuu wa kijiji kwa kuridhia uuzwaji huo," alimalizia Molel.
  
Mkazi wa kijiji chicho cha Tukamisasa, Shujaa Theophil akizungumza katika mkutano huo. PICHA ZOTE NA OMARY MNGINDO.


No comments:

Post a Comment