Wednesday, January 15, 2020

DC KILWA AKERWA NA UCHELEWESHWAJI NAKALA ZA HUKUMU

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

MKUU wa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi Christopha Ngubiagai amesema ucheleweshwaji wa nakala za hukumu katika Mahakama ya Wilaya ya Kilwa ni Donda ndugu linalohitaji mwarobaini kwa baadhi ya wafungwa ambao wapo katika gereza la Wilaya hiyo Ngubiagai ameyasema hayo leo (jana) wakati akitoa salamu za Wilaya hiyo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania Profesor Ibrahimu Juma katika khafla fupi ya ufunguzi wa jengo jipya la Mahakama Wilayani hapo lenye thamani ya shilingi milioni 705.

Ngubiagai alisema usimamizi wa sheria na utoaji haki bado unakabiliwa na changamoto nyingi ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni kupungua kwa uadilifu kwa watumishi wachache wenye dhamana ya kusimamia sheria na kutoa haki.

Alisema wapo watumishi ambao wanadai rushwa, na wengine ambao wanatoa hukumu za upendeleo pamoja na kuchelewa kuandika hukumu na hata nakala za hukumu.

“Mfano katika gereza la Wilaya ya kilwa kuna jumla ya wafungwa 88 ambao wanatumikia vifungo vyao lakini hawajaweza kupatiwa nakala za hukumu zao” Ngubiagai alisema.

Ucheleweshwaji wa nakala hizo za hukumu zinawafanya wafungwa hao wanaoendelea kutumikia vifungo vyao kushindwa kuendelea na haki zingine ikiwemo ya kukata rufaa.

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya kanda Mtwara Paulo Ngwembe alisema kuwa kwa mujibu wa mwongozo na taratibu za Mahakama kuu zinataka nakala za hukumu pamoja na mienendo ya Mashauri zitolewe ndani ya siku 30 ambapo kwa Mtendaji yeyote wa Mahakama anaechelewesha kupatikana kwa vielelezo hivyo anahesabika anaihalifu mahaka.

“lakini sisi kama majaji na mahakimu katika kanda ya Mtwara tulikubaliana kwamba nakala za hukumu na mwenendo wa mashahuri zitolewe ndani ya siku (7), (14) mpaka 28 pale ambapo kutakuwa na hali isiyo ya kawaida hatukutaka kufikia ile iliyowekwa kwa mujibu wa uongozi wa mahakama kuu”

Kufuatia hali hiyo Jaji mkuu wa Tanzania Professor Ibrahimu Juma alitoa wito kwa watumishi watakao tumia jengo hilo kuwa wanapaswa kuliheshimu jengo hilo kama wanavyoyaheshimu majengo ya ibada na kwamba litumike kwa kazi tarajiwa ya kutoa haki pamoja na kutoa elimu ya sheria kwa umma.

Hata hivyo professor Ibrahimu aliongeza kuwa Mahakama inayoongozwa na professor Ibrahimu Juma haitakuwa na uvumilivu kwa mtumishi yeyote ambae anaharufu ya rushwa huku akieleza kuwa yeyote atakaebainika atashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria.

No comments:

Post a Comment