Sunday, January 12, 2020

WAAJIRI WASIOLIPIA WAFANYAKAZI MIFUKO YA HIFADHI KUSHTAKIWA.

Happy Lazaro, Arusha.

Naibu waziri wa kazi, Vijana, Ajira na Ulemavu , Antony Mavunde ameiagiza Mifuko ya hifadhi ya jamii nchini kuwachukulia hatua kali ya kuwafikisha mahakamani waajiri wote wasiopeleka michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko hiyo na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyakazi pindi wanapoacha ama kuachishwa kazi.


Mavunde ametoa kauli hiyo jijini Arusha wakati alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa hoteli za Naura springs na Impala za jijini Arusha ambapo wafanyakazi hao walimweleza changamoto mbalimbali ikiwemo ya suala la michango ya mifuko ya Hifadhi ya jamii.


Naibu waziri amesema kuwa kumekuwepo na malalamiko mengi kwa baadhi ya waajiri nchini kutopeleka michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii jambo ambalo alionya ni kinyume cha sheria na kuitaka mifuko hiyo kuwakamata waajiri hao na kuwafikisha mahakamani.


Akiongelea changamoto za wafanyakazi katika hoteli hizo,Mavunde ameitaka menejimenti ya hoteli hiyo kuboresha utendaji wake wa kazi na kuhakikisha wanakuwa kitu kimoja na wafanyakazi wao kwani serikali inawahitaji wawekezaji wa mahoteli katika kuimarisha sekta ya utalii na ajira.


Naibu waziri amempongeza mkurugenzi wa hoteli hiyo,Randy Mrema kwa kukubali kumaliza changamoto ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi wake ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa hadi ifikapo Machi 31 mwaka huu. 


Kwa upande wake Mkurugenzi wa hoteli hizo Randy Mrema alimweleza Naibu waziri kuwa yupo tayari kumaliza changamoto za wafanyakazi wake na kuahidi pindi ifikapo Januari 31 mwaka huu atalipa mishahara ya miezi miwili na kwamba ifikapo Machi 31 mwaka huu atamaliza madai yote ya wafanyakazi hao.


Awali wafanyakazi hao walimweleza Naibu waziri kuhusu madai ya kutolipwa mishahara ya miezi sita pamoja na baadhi yao waliopunguzwa kazi hivi karibuni kutolipwa stahiki zao ikiwemo mishahara ya kuvunja mkataba.


Wamedai kuwa hali hiyo imewafanya waishi katika mazingira magumu na kushindwa kumudu maisha ikiwemo kuwasomesha wao ,kodi za pango pamoja na mahitaji mengine ya kujikimu.


Hata hivyo wameahidi kuendelea na kazi bila kuwa na kinyongo huku wakisubiri ahadi ya mwajiri wao ya kuwalipa mishahara katika kipindi cha miezi mitatu alichoahidi.

No comments:

Post a Comment