Saturday, January 11, 2020

WAKAZI WA ZINGA BAGAMOYO WALILIA AGIZO LA RAIS MAGUFULI

 Mke wa Rais Mstaafu wa serikali ya awamu ya nne ambae ni Mbunge wa kuteuliwa, Mama Salma Kikwete akizungumza na wana-Jumuia ya UWT wa Kata ya Zinga akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja.
 Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo mkoani Pwani Dkt. Shukuru Kawambwa akizungumza na wana-Jumuia ya UWT wa Kata ya Zinga akoambatana na Mke wa Rais Mstaafu wa serikali ya awamu ya nne Mama Salma Kikwete, ambae pia ni Mbunge wa kuteuliwa. Picha na Omary Mngindo


.........................................


Na Omary Mngindo, Bagamoyo.

WAKAZI wa Vijiji vinavyounda Kata ya Zinga wilayani ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wamesikitishwa kwa kitendo cha kupuuzwa agizo la Rais John Magufuli, la kuwataka wananchi wasiolipwa fidia katika mradi wa EPZ wapewe maeneo yao.


Kilio hicho kimetolewa na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi katani hapo Mukhisin Mintanga, mbele ya Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne Mama Salma Kikwete, akiwa katika ziara ya kuimarisha Jumuia ya Wanawake (UWT) wilayani humo.


Ziara ya Mama Salma iliyoanzia Jimbo la Chalinze na kumalizia Bagamoyo, akiwa Zinga amepokea changamoto kadhaa ikiwemo ya fidia, ambapo Mintanga alisema kuwa pamoja na Rais Magufuli kutoa kauli hiyo, lakini hakuna utekelezaji wake.


"Rais Magufuli alipokuja alitoa agizo kwamba, wananchi ambao hawajalipwa fidia kupisha mradi wa EPZ waruhusiwe kuendeleza maeneo yao, lakini wanapokwenda halmashaauri au ofisi za EPZ wanambiwa maeneo yamewekewa GN, mpaka itenguliwe na Waziri mwenye dhamana," alsema Mintanga.


Akizungumzia hilo, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa alimwambia Mama Salma kwamba, suala hilo alishaanza kulifanyikazi, lakini kwa bahati mbaya Waziri aliyekuwepo amebadilishwa Wizara.


"Mheshimiwa Mama Salma suala hili awali lilinichanganya, nikahoji hivi ni nani aliye juu ya Rais, sababu Rais Magufuli ameshaagiza kuwa waliokosa fidia wapewe maeneo yao lakini hakuna utekelezaji, ndipo nikaelezwa kuwa kuna hatua za kufuatiliwa wizarani kuhusiana na GN," alisema Dkt. Kawambwa.


Akizungumza na wanachi hao, Mama Salma alisema kwamba amelichukua hilo, na kuwa ataungana na Mbunge Kawambwa katika kulifanyia kazi, ili agizo lililotolewa na Rais liweze kutekelezwa mapema iwezekanavyo.


Aidha Mama Salma amewataka wakazi wilayani hapa kushiriki zoezi la uboreshwaji wa daftari la makazi, linalotaraji kuanza tarehe moja mwezi wa pili, litakalodumu kwa siku saba ili wasipoteze haki zao za msingi za kuchagua viongozi katika maeneo yao.


"Zoezi la uboreshaji wa daftari la makazi litaanza tarehe moja mwezi wa pili mwaka huu, niwaombe tuzitumie siku saba za zoezi hilo, kuboreshe taarifa zetu, mfano mtu ulikiwa unaishi Lindi sasa upo Bagamoyo unalazimika kufanya hivyo," alisema Mama Salma.

No comments:

Post a Comment