Wednesday, January 15, 2020

MKAZI KIDUGALO AUAWA NA TEMBO

Na Omary Mngindo, Chalinze,

MKAZI wa Kijiji cha Kidugalo, Kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo Pwani John Taimu, amepoteza maisha kwa kushambuliwa na Tembo akiwa msituni.

Taimu ambaye inadaiwa alikwenda katika moja ya msitu uliopo Midulu jirani na msitu wa Kambi ya Jeshi, mwili wake umeokotwa ndani ya msitu huo, hatua inayoelezwa imetokana na mkazi huyo kwenda huko kutafuta kuni.

Diwani wa Kata ya Bwilingu Lucas Lufunga alimweleza Mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kwamba, tukio hilo lililotokea january 13, 2020, mbali ya kuleta hofu kwa jamii, pia kifo hicho kimeacha simanzi kubwa kwa wanafamilia na wananchi wa maeneo hayo.

Amesema kuwa tangu Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli kuingia madarakani miaka minne iliyopita, imeweka mikakati madhubuti ya kudhibiti matukio ya mauaji ya Tembo, kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanyama hao, hivyo kuongeza hofu kwa wananchi.

"Kwanza tunaishukuru Serikali kwa udhibiti wa matukio ya mauwaji ya wanyama hususani Tembo, hii imeongeza wingi wa wanyama hao kuzaliana, hivyo kutembea mpaka kwenye makazi ya watu kisha kusababisha uharibifu wa mali na majeruhi wananchi," alisema Lufunga.

Aidha diwani huyo amewaasa wananchi kuwa makini wakiwa katika shughuli zinazowaingizia kipato, kwani hivi sasa wanyama hao ndani ya Halmashauri ya Chalinze wameripotiwa kuongezeka, hivyo kusababisha madhara ikiwemo uharibifu wa vyakula mashambaani.

"Marehemu Taimu alikwenda katika msitu huo kwa lengo la kutafuta kuni, lakini kwa bahati mbaya akakutana na Tembo, waliosababisha kifo chake, ambapo mawili wake ulikutwa kwenye msitu huo, leo muda huu wa saa 7 mchana tunazika (jana)," alisema Lufunga.

Aidha amewataka wananchi kujilinda kwenye maeneo yenye wanyama, huku akiiomba serikali kuendelea na utoaji wa elimu kwa ili kukabiliana na tatizo linaonekana kushamiri maeneo ya Matipwili, Mkange, Kiwangwa na sasa Matulii.

No comments:

Post a Comment