Na
Omary Mngindi, Kisarawe.
MBUNGE
wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynab Vulu, amewataka mafundi wanaojenga vyoo
kwenye shule mbalimbali mkoani hapa, kuweka kipaumbele maalumu katika vyumba
upande wa wasichana.
Vulu
ametoa rai hiyo katika Kijiji cha Kisangile Kata ya Marui wilaya ya Kisarawe
mkoani hapa, alipokwenda kuhamasishaji zoezi la uboreshaji wa daftari la
wapigakura, linalotarajiwa kuanza Februali Mosi mpaka saba mwaka huu, huku Mkoa
wa Pwani ikiwa ni moja ya mikoa itakayoanza zoezi hilo.
Akiwa
kijijini hapo, Vulu alichangia shilingi laki moja na elfu themanini ya
kununulia mifuko 10 ya saruji, itayokajengea matundu kumi ya vyoo kwenye shule
shikizi kijijini hapo, yenye vyumba vitano, vyoo matundu matatu, walimu wawili
na wanafunzi 380.
Alisema
kuwa katika ujenzi wa matundu kumi unaotarajiwa kuanza, ni vyema mafundi
wakazingatia mazingira ya wasichana, kulingana na hali wanayokabiliana nayo
katika kila kipindi, hivyo ni vizuri wakaweka chumba maalumu kwa ajili ya
kujisitiri.
"Sisi
kina Mama tuna muda maalumu tunaoutumikia, ambao hata katika vitabu vya dini
vimeandikwa, hivyo ni vyema kwa viongozi kukaa na mafundi, mkawapatia maelekezo
kuhusiana na ujenzi utakaozingatia mahitaji hayo," alisema Vulu.
Kwa
upande wake Abdallah Mapanya alisema kuwa shule hiyo yenye vyumba vitano, vinne
vimejengwa kwa nguvu za wananchi, huku halmashauri ya wilaya ya Kisarawe
ikijenga darasa moja linalotumiwa na wanafunzi wa shule ya awali.
"Masikitiko
yetu wana-Kijiji cha Kisangile ni hatua ya kutopatiwa kibari kwa shule hii pia
walimu, kwani hapa kama mlivyoona kuna mwalumu mmoja na mwingine wa pili
anajitolea tu, tumepeleka maombi yetu lakini hakuna taarifa zozote,"
alisema Mapanya.
Diwani
wa Kata hiyo Salehe Mfaume alisema kwamba shule yao ni shikizi, na kwamba
tayari wataalamu wa elimu kutoka halmashauri wameshafika, na kuwaambia wachimbe
shimo la matundu kumi ya vyoo kama ilivyo utaratibu wa serikali.
"Nimekutana
na wataalamu wanaohusika na elimu, nikawaelezea juhudi za wana-Kisangile,
wamefika wakatueleza tuchimbe shimo la vyoo lenye matundu kumi, zoezi ambalo
tayari limeshaanza," alisema Mfaume.
Akizungumzia
juhudi za wakazi wake kwenye suala la maendeleo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho
Ally Korongo alisema kuwa, wananchi wamejitolea katika ujenzi huo kwa kuchangia
michango ya hali na mali.
No comments:
Post a Comment