Sunday, January 19, 2020

TANI 60 ZA KOROSHO GHAFI ZAKOSA WANUNUZI LINDI.

Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao Mohamed Duka akifungua kikao cha mnada wa Korosho uliofanyika katika chama cha msingi Kiwalala AMCOS Halmashauri ya Mtama, PICHA NA HADIJA HASSAN.
..................................................


Na HADIJA HASSAN, LINDI.

ZAIDI ya Tani 60 za korosho ghafi kutoka chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao kinachojumuisha Wakulima wa Wilaya za Mtama, Kilwa na Manispaa ya Lindi Mkoani humo zilizopelekwa kwenye Mnada wa 10 wa chama hicho zimekosa wanunuzi.

Korosho hizo zilizokosa wanunuzi ni Korosho daraja la kwanza tani 4 na kg 318 na daraja la pili tani 6 na kg 74 kutoka ghala la Buko Lindi na Tani 50 daraja la pili kuoka ghala la Nangurukuru Kilwa.

Kwa mujibu wa Afisa ushirika wa Mkoa wa Lindi Richard Zengo alisema kuwa katika mnada wa 10 uliofanyika jana Januari 18, 2020 katika Chama cha Msingi cha Ushirika Kiwalala AMCOS halmashauri ya Mtama jumla ya tani 1057 na kg 761 zilifikishwa mnadani huku mnunuzi mmoja tu ndie aliyeomba kununua korosho hizo.

Zengo alisema katika mnada huo korosho Tani 150 na kg 827 Daraja la kwanza kutoka ghala la Mtama na Tani 378 na kg 827 za Ghala la Nangurukuru ziliuzwa kwa bei ya Shilingi 2015 na huku Daraja la pili tani 38 na kg 198 kutoka Ghala la mtama na tani 429 na kg 993 kwa bei ya shilingi 1560.

Awali Akiwasalimu wananchi wa Kilwalala Diwani wa kata hiyo kabla ya kutangazwa kwa bei hizo za korosho alitumia fursa hiyo kuwashauri wananchi hao kuridhia kuuza korosho hizo kwa bei iliyoko sokoni.


"Kwa kuwa mnunuzi aliyetufikia ni mmoja na bei tumezisikia Sisi hatuna namna niwasihi wakulima wenzangu kuipokea bei hii wajanja wanasema pesa haikataliwi hivyo katika mjadala wetu wote tukumbuke kuwa sisi ndio tuliopewa dhamana ya kuuza ama kuto kuuza korosho hizi hivyo sio vibaya kwa Kuzingatia hali ya maisha ya sasa sisi tukaitikia hiyo bei iliyopo kuuza korosho zetu" aliwasihi wananchi hao.

Hata hivyo ushauri wa Diwani huyo uliungwa mkono na wakulima waliohudhuria katika mnada huo kwa pamoja kuridhia kuuza korosho hizo kwa bei zilizopo sokoni.

Akifunga kikao hicho cha Mnada wa korosho Mwenekiti wa chama hicho Mohamed Duka aliwapongeza wakulima hao kwa maamuzi ya busara ya kuridhia kuuza korosho zao kwa bei iliyopo Sokoni.


No comments:

Post a Comment