Tuesday, January 28, 2020

MNADA WA 11 WA KOROSHO GHAFI WAAHIRISHWA LINDI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI

CHAMA kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao kinachojumuisha wakulima wa Halmashauri ya Kilwa, Mtama na Manispaa ya Lindi Mkoani humo kimejikuta kikilazimika kusitisha kuendelea na mnada wake wa 11 wa mauzo ya korosho ghafi kwa kile kilichodaiwa kukosekana kwa watoa maamuzi.

Mnada huo ulifanyika katika chama cha msingi Tulieni Amcos Manispaa ya Lindi ambapo jumla ya tani 305 na kg 212 za korosho ghafi zilifikishwa kwenye mnada huo.

Kwa mujibu wa Kaimu meneja Mkuu wa chama hicho Mohamed Mchekenje alisema kuwa kati ya tani 305 na kg 212 , kg 5,720 za Daraja la kwanza na kg 6,074 Kutoka ghala la Buco Manispaa ya Lindi huku kg 10548 za daraja la kwanza na kg 282,870 za daraja la pili zikitoka katika ghala la Nangurukuru kilwa.

Wakati mnada huo unafanyika katika Manispaa ya Lindi, mnunuzi aliejitokeza kwa siku hiyo aliomba kununua korosho za Ghala la Nangurukuru tani 10 na kg 548 kwa bei ya shilingi 1,560 kwa korosho daraja la kwanza na tani 1 na kg 168 kwa shilingi 1,168 kwa korosho daraja la pili.

Baada ya majadiliano ya muda mrefu baina ya Mrajisi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Lindi Robert Nsunza, Afisa kutoka Bodi ya Korosho Ayub Mumi wajumbe wa bodi wakapendekeza mnada huo kuahirishwa mpaka pale watakapotangaza tena ili kuwapa fursa wanunuzi wengi kuja kununua korosho hizo pamoja na kuwapa fursa wakulima wa maeneo husika kutokea maamuzi ya kuuzwa kwa korosho zao.

"mnunuzi kuomba kununua korosho za kilwa wakati mnada unafanyika Manispaa haikuwa tatizo kwa wakulima wa hapa kutolea maamuzi endapo bei ingekuwa nzuri lakini kutokana na mazingira haya tumelazimika kusitisha mpaka pale tutakapopanga tena" alisema Mohamed Masudi makamu mwenyekiti.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Ndani wa Bodi ya Korosho Tanzania Ayub Mumi aliwashauri viongozi wa chama hicho kuandika barua na kuiwasilisha bodi ya korosho itakayoeleza sababu ya kuahirisha mnada huo pamoja na tarehe watakayoipendekeza kufanya mnada wa marudio.

"Kama mnakumbuka bodi ya korosho ilishatoa barua kwa vyama kikuu vyote kuwaeleza kuwa tarehe 26 ndio msimu wa korosho unafungwa rasm hivyo ni vyema muandike barua ili kuwajulisha hali halisi na wao wakafahamu kinachoendelea vinginevyo mnaweza kuendesha mnada ambao ni batili" alisisitiza Mumi

No comments:

Post a Comment