Saturday, January 11, 2020

RIDHIWANI AWATAKA WAZAZI KUPELEKA WATOTO WALIOFIKIA UMRI WA KWENDA SHULE.

Na Shushu Joel

MBUNGE wa jimbo la Chalinze Mh Ridhiwani Kikwete amewataka wazazi wote katika jimbo lake kuwapeleka watoto wote waliotimiza umri wa kwenda shule ili waanze masomo haraka iwezekanavyo.


Wito huo ameutoa alipokuwa akizungumza na baadhi ya wazazi katika moja ya vikao vyake dhidi ya wananchi wake.


Alisema kuwa elimu ni ufunguo wa maisha hivyo kila mzazi ni lazima ahakikishe mwanae anaenda kuanza shule.


Aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli imetusaidia kwa kiasi kikubwa wananchi wa chalinze kwa kutupatia misaada mbalimbali ya kielimu hivyo jukumu tulilonalo wazazi ni kujitokeza kwa wingi ili kuwaandikisha watoto wetu wenye umri wa kuanza masomo ya msingi katika shule mbalimbali zilizopo jimboni.


Aidha Kikwete aliongeza kuwa chalinze imejipanga kisawasawa kwa kushirikiana na wananchi wake kuhakikisha wanakuwa kinara wa miundombinu ya utoaji wa elimu kwa watoto ili kuongeza ufanisi wa elimu kwenye jimbo hilo.


"Elimu bure imesaidia kuwapunguzia changamoto wananchi wengi hapa nchini hivyo pongezi za pekee ziende kwa Rais Magufuli kwani awali jambo hili lilikuwa kero kwa wananchi lakini sasa hivi lipo shwari "Alisema Kikwete.


Naye Mohammed Mzimba mmoja wa wazazi amempongeza mbunge huyo kwa jinsi anavyojitoa kutoa hamasa ili kuandikisha watoto mashuleni.


Hivyo nae amewataka wazazi wenzake kuchangamka kuwapeleka watoto shule ili waweze kupata elimu yao itakayowasaidia siku za baadae.


Aidha aliongeza kuwa elimu ya msingi ndio chanzo cha kupata elimu ya juu na kuwataka wazazi wasitegemee kuwasimamia watoto wao kwenye elimu za juu huku wakiwa wamepuuza elimu ya msingi.


"Watoto wetu wakipata elimu  bora tokea msingi wakifika elimu za juu itakuwa rahisi kwao kuwa na utambuzi wa hali ya juu"Alisema Mzimba.


Aidha amempongeza Rais Magufuli kwa usimamizi wa fedha za elimu bure kwenye shule mbalimbali .
Sara Juma amesifu jinsi mbunge Kikwete anavyojitoa kwa wananchi kwa lengo la kuhamasisha wazazi kuandikisha watoto wao kuanza shule mapema.

No comments:

Post a Comment