Friday, January 17, 2020

UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA LINDI WAELEKEA UKINGONI

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Wakati zoezi la uandikishaji wa dafatari la kudumu la wapiga kura likiwa linaelekea mwishoni katika mikoa ya Lindi na Mtwara, baadhi ya wananchi wa wilaya ya Kilwa mkoani Lindi wameelezea changamoto mbali mbali zinazolikabili zoezi hilo ikiwemo ya usumbufu wa baadhi ya mashine za BVR.

Wakizungmza na Bagamoyo kwanza Blog baadhi ya wananchi wa kilwa masoko, somanga, na Kinjumbi waliofika katika vituo vya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura wameeleza kuwapo na changamoto za baadhi ya mashine ambazo huwalazimu kusubiri kwa muda.

Nae Mohamed Linena Mkazi wa Kilwa Masoko alisema kuwa baada ya kufika katika kituo cha kujiandikisha wapiga Kura alilazimika kusubiri kwa masaa kadhaa katika kituo hicho kuendelea na zoezi hilo kutokana na mashine hizo kusumbua mpaka pale fundi wa (BVR) alipofika na kufanya marekebisho katika mashine hizo.

Nae mwandikishaji mkuu wa kituo cha ofisi ya Serikali ya Kijiji Somanga Kusini kata ya Somanga alisema kuwa licha ya ya changamoto hizo, zoezi hilo limeenda vizuri kwa siku zote isipokuwa siku ya nne ndio kulitokea changamoto kwenye mashine hiyo ya BVR hali iliyowalazimu kusimamisha kwa muda zoezi la uandikishaji.

Nae mwandikishaji Msaidizi wa kituo hicho cha Somanga kusini, Yusra Mtulya –alisema kuwa Inapotokea changamoto kama hiyo ya hitilafu ya mashine kwa muda mrefu huwalazimu wananchi wanaokwenda kujiandikisha kuwapeleka katika kituo cha jirani ili waweze kujiandikisha.

Kwa upande wake IT wa BVR Operate ambae alikataa kutaja Jina lake aliieleza Bagamoyo kwanza Blog kuwa maranyingi hitilafu zinazojitokeza katika mashine hizo za BVR zinatokana na kuhamishwa hamishwa kwa mashine hali inayopelekea baadhi ya waya kuchomoka au kukatika hiyo inatoka na aina ya usafiri unaotumika na hasa kwa hali ya bara bara ilivyo.

Nae Ofisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Ally Ligalawike alisema changamoto hiyo ya kusumbua kwa mashine za BVR unatokana na Jografia ya maeneo husika kwani yapo maeneo ambayo hayana umeme kabisa hali inayowalazimu wasimamizi wa maeneo hayo kuisafirisha mashine hiyo hadi maeneo jirani ambako umeme unapatikana ili waweze kuichaji kwa ajili ya matumizi ya siku inayofuata

" kutokana na hali ya Bara bara hasa katika kipindi hiki cha masika maeneo mengi magari yanashindwa kufika hiyo ulazimika kutumia usafiri wa baiskeli au pikipiki ili kutafuta umeme wa kuchaji mashine hizo kwa ajili ya matumizi ya siku inayofuata"

Alisema hali hiyo inafanya mashine zilete hitirafu mara kwa mara kwa baadhi ya maeneo yenye changamoto hiyo.

Hata hivyo Ligalawike aliesema kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo Halmashauri imetoa magari sita ambayo yatatumika kwa dharula katika tarafa sita za Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na mafundi (BVR Operate) kutoka tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC.

Kuhusu hali ya zoezi inavyokwenda alisema zoezi linaendelea vizuri kwani mpaka sasa tayari wameshaandikisha zaidi ya asilimia 70 ya lengo walilojiwekea kuandikisha wapiga Kura wa Wilaya hiyo.

Zoezi la uandikishaji katika dafrati la kudumu la wapiga kura katika mikoa ya Lindi na Mtwara lilianza januari 12 mwaka huu wa 2020, ambapo linategemewa kufikia tamati januari 18 likiwa na lengo la kuandikisha wananchi waliofikisha umri wa kupiga kura, kuboresha taarifa za baadhi ya waliowahi kujiandikisha pamoja na kurekebisha taarifa za wasio na sifa ikiwamo waliofariki.

No comments:

Post a Comment