Friday, January 17, 2020

MWAKITINYA AWAPA SOMO UVCCM DODOMA

Na Omary Mngindo, Dodoma

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (MNEC-CCM) kundi la vijana Mussa Mwakitinya, amewataka vijana kuyasemea mazuri yanayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli.

Aidha MNEC huyo amewakumbusha wanafunzi hao wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Tanzania kilichopo Manispaa ya Dodoma, kutumia vyema masomo yao katika nyanja ya siasa ya Ujamaa, inayolenga kudumisha umoja, upendo na mshikamano katika nchi.

Mwakitinya ametoa kauli hiyo hivi karibuni akiwa mgeni rasmi kwenye Mkutano Mkuu wa Matawi mawili ya UVCCM, uliofanyika ndani ya Kata ya Ntyuka mbele ya Mwenyekiti Patrick Mathias, Katibu Aidan Kajivo na viongozi mbalimbali wa tawi la CBSL.

Mwakitinya alianza kwa salamu za Mwenyekiti wa CCM Taifa John Magufuli na Mwenyekiti wa UVCCM Kheri James, pia akipongeza kazi nzuri zinazotekelezwa na serikali, sanjali na Jumuiya hiyo kupata eneo la kujenga ofisi lililopo kata ya Ntyuka.

“Ndani ya chama na Serikali kuna macho yanakuangalia wakati mwenyewe usijue, niwakumbushe wana-CCM wenzangu tudumishe Umoja na mshikamano wetu katika kuelekea uchaguzi Mkuu, kwa kuhakikisha tunafuata misingi ya chama," alisema.

Aliongeza kuwa chama kinawahitaji watu wenye hulka kama za Dkt John Magufulli, na kwamba wawapime watu wanaokuja kuomba kura kwa kuangalia kama wanaendana na tabia ya Rais huyo.

"Tusiwape nafasi watu wanaopinga maendeleo na vibaraka wao katika kuelekea uchaguzi mkuu, vipo vyama vimepoteza mwelekeo, vinafanya siasa panapokuwepo na matukio, kutokee msiba, ajali, mafuriko na majanga mbalimbali, twendeni tukawapige mchana kweupee," alisema NEC huyo.


Aidha Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuwakilisha Vijana, ameviasa vyama vya siasa na baadhi ya wanasiasa, kuacha kuyapeleka masuala ya nchi kwa watu wa nje ya nchi, ambao hawahusiki na chochote cha nchi hii.

Kwa upande wake Katibu wa tawi la UDOM Mwinyi Halid alisema kuwa wao ni askari walio mstari wa mbele katika kukilinda Chama cha Mapinduzi (CCM0), pia wakiwa wasomi kazi yao ni kushauri na kupongeza panapofanyika mageuzi ya kiutendaji, yanayoleta athari chanya katika maisha ya watu.

No comments:

Post a Comment