Thursday, January 2, 2020

HOSPITALI MKURANGA YAPATIA X-RAY NA ULTRA SOUND

Pichani Waziri Suleiman Jafo mwenye suti akiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalla Ulega (Shati jeupe) Zaynab Matitu Vulu, Mkuu wa wilaya Philbeto Sanga na Mganga Mkuu wa wilaya wakishuhudia uzinduzi wa mashine ya X-ray kwenye hospitali ya Mkuranga. Picha na Omary Mngindo.
.........................................


Na Omary Mngindo, Mkuranga.

SERIKALI kupitia Wizara ya afya imeipatia hospitali ya wilaya ya Mkuranga mashine za X-ray na Ultra Sound, ikiwa ni uboreshaji wa huduma hiyo hospitalini hapo.

Hayo yamebainika kwenye uzinduzi wa vifaa hivyo, uliofanywa na Waziri wa TAMISEMI Suleiman Jafo, ambapo amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kupitia Waziri wa afya Ummy Mwalimu, kwa msaada huo.

Mbunge wa jimbo la mkuranga Abdallah Ulega ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ametoa shukrani mbele ya Waziri wa TAMISEMI Alhaj Suleiman Jafo, na mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Zaynab Vulu, kwenye hafla ya uzinduzi wa mashine hizo hospitalini hapo.

Ulega alisema kuwa hispitali hiyo inayobeba wagonjwa wengi kutoka wilaya mbalimbali na Mkoa wa Dar es Salaam, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya vifaa tiba ikiwemo mashine ya X-ray na Ultra Sound ambapo alimuomba Rais Magufuli juu ya hilo.

"Nilimweleza Waziri Ummy Mwalimu kuhusiana na azma ya kununua vifaa hivyo, kwamba tumetenga pesa kupitia halmashauri kwa ajili ya kununua vifaa hivyo, lakini Dada yangu Ummy akaniambia nizipeleke katika ujenzi wa madarasa, yeye atanipatia," alisema Ulega.

"Leo nina furaha kwa ndugu yangu Jafo kufika kwa tendo la uzinduzi wa mashine hizi ambazo tayari zimeshaanza kutoa huduma, tumeambiwa na Mganga Mkuu kuwa mgonjwa mmoja tu alipelekwa Muhimbili kwa ajili ya kipimo kikubwa zaidi," alisema Ulega.

Aliongeza kuwa mashine ya X-ray iliyofungwa ni sawa na ya Muhimbili, ambapo ukipiga picha hata ukienda miaka mingapi utaikuta, huku akimshukuru Rais Magufuli kwa upendo mkubwa alionao kwa wana-Mkuranga.

Akizungumza kabla ya Waziri Jafo, Mbunge wa Viti Maalumu mkoani hapa Zaynab Vulu aliishukuru serikali kwa juhudi za kuboresha upatikanaji wa huduma kwenye hospitali hiyo kongwe wilayani hapo.

"Hospitali yetu ya Mkuranga ni kongwe inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo vifaa hivi vilivyoletwa kutoka kwa Rais wetu Magufuli kupitia Waziri mwenye dhamana ya afya Ummy Mwalimu," alisema Vulu.

Akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Waziri Jafo alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kupambana na changamoto sugu zilizokuwa zinazowakabilia wananchi.

"Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli miradi mingi ya kimaendeleo inaendelea kufanyika, upande wa sekta ya afya zahanari zinajengwa na kuboreshwa sanjali na vituo vya afya na hospitali," alisema Jafo.

No comments:

Post a Comment