Wednesday, January 29, 2020

SUBIRA MGALU AWAONYA WATAKAOUZA NGUZO ZA UMEME.



NA MWAMVUA MWINYI, KISARAWE.

NAIBU Waziri Wa Nishati ,Subira Mgalu ametoa tahadhali kwa vishoka na baadhi ya watumishi REA, ama shirika la umeme Tanesco kujiepusha na uuzaji wa miundombinu ya umeme na vifaa mbalimbali ikiwemo nguzo.


Ameeleza, endapo atabainika yeyote kujihusisha na vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria kwakuwa anarudisha nyuma juhudi za serikali na ni uhujumu uchumi.


Akihitimisha ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi wa Peri -Urban wilayani Kisarawe, Subira alisema, msimamo wa serikali nguzo haziuzwi, hata kama mtumishi upo REA ama TANESCO.


Aidha Subira ,alitoa rai kwa wananchi wasithubutu kulipia nguzo au kufanya makubaliano yoyote nje ya utaratibu wa serikali.


Akizungumzia suala la vishoka wanaofoji vitambulisho ,alisema serikali pia imeweka msimamo ,endapo kuna mazingira hayo wananchi watoe ushirikiano ili kuwabaini wahusika.


Aliomba vyombo vya usalama vya ngazi husika kuliona hilo ni moja ya majukumu yao kubaini vishoka wanaouza miundombinu mbalimbali na vifaa na kubaini mtumishi yeyote atakaehusika.


Pamoja na hayo,Naibu Waziri huyo alitaka maeneo ya taasisi za umma ikiwemo shule na viwanda kupewa kipaombele kufikishiwa umeme na kumtaka mkandarasi aendane na kasi inayoendana na muda aliopangiwa ili jamii iondokane na adha ya kukosa huduma ya nishati ya umeme.


Nae diwani wa kata ya Msimbu, Mama Lilomo alifafanua, kata yake imeguswa na  umeme eneo la Homboza lakini bado kuna changamoto ya ukosefu wa umeme katika vitongoji saba.


Kwa upande wake ,Mkuu wa shule ya sekondari Christon ,August Minja alieleza kwamba, mradi huo utakapokamilika na kufika shuleni hapo, itakuwa ni chachu ya kuinua taaluma,pia aliipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Rais John Magufuli kwa kuhakikisha umeme unafika pembezoni na miji na vijijini.

No comments:

Post a Comment