Tuesday, January 28, 2020

VIJIJI 6 WILAYA YA KILWA VYAKUMBWA NA MAFURIKO.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Zaidi ya watu 4,500 katika vijiji sita vya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi wameathirika na mafuriko kufuatia hali ya mvua inayoendelea katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.

Bagamoyo Kwanza Blog imetembelea katika kijiji cha njinjo na kukuta baadhi ya wananchi wakiwa wamekaa juu ya mapaa ya nyumba, miti na vichuguu kwa zaidi ya siku mbili mfululizo kwa ajili ya kunusuru maisha yao huku hali zao zikionekana kudhoofika kwa kukosa chakula.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya kilwa Christopha Ngubiagai alisema vijiji vilivyoathirika na mvua hiyo ni pamoja na Njinjo, kisima Mkika, kipindimbi , Luatwe mitole, Kikole, Njinjo B na Nakiu ambavyo vinapitiwa na Mto matandu.

Ngubiagai alisema zoezi la uokoaji linaendelea ambapo mpaka siku ya jana january 27, watu 1000 tayari wameshaokolewa na kuwekwa katika shule ya msingi kipindimbi wa ajili ya kuwahifadhi.

"Hali hii inatokana na kuzidiwa kwa mto matandu ambao unapita katika vijiji hivyo kunakotokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambapo kingo za mto huo kwa sehemu kubwa zimeharibika na hatimae mchanga kuingia mtoni na kufanya kina hicho cha mto kuwa kifupi hali inayopelekea maji hayo kuenea katika makazi ya watu" alifafanua Ngubiagai.

Ngubiagai pia alitumia fursa hiyo kuomba Serikali kuongeza vifaa vya uokoaji kwa ajili ya kuwaokoa wananchi waliopo maeneo ambayo hayawezi kufikika kwa urahisi pamoja na kuongeza kasi ya uokoaji

"Kutokana na ufinyu wa vyombo vya uokoaji bado watu wengi kama unavyoona bado hawajafikiwa pamoja na boti tulizonazo bado tunahitaji kuwa na faiba bot, ikiwezekana tupatiwe na helicopter ya kusaidia ukoaji, ukiangalia maeneo mbali mbali ambayo yameathiriwa na mvua hiyo"

Nae mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa Mkoa huo , Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi akizungumza katika eneo la tukio alisema kwa sasa katika Mkoa huo hali sio nzuri hasa kwa Wilaya za Ruangwa, Liwale, Kilwa pamoja na Halmashauri ya Mtama.

Alisema kufuatia mvua hizo tayari watu sita wameripotiwa Kufa na maji yanayotokana na mvua hiyo huku akieleza kuwa huwenda idadi hiyo ya vifo ikaongezeka zaidi kutokana na hali ya mvua zinazoendelea kunyesha.

"Nimepokea taarifa kutoka kwa kamanda wa polisi Mkoa kuwepo kwa taarifa ya watu kufa maji, 2 kutoka Ruangwa, 2 mtama na 2 kutoka kilwa" Alisema Zambi.

Nae katibu tawala wa Mkoa wa Lindi Bi Rehema Madenge alisema kuwa tayari wameshafanya maandalizi ya chakula, dawa za dharula kwa ajili ya Magonjwa ya mlipuko endapo yatatokea kwa waathirika wa mafuriko hayo.

Hata hivyo Madenge alitoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo za Serikali kwa kuwasaidia wahanga hao wa mafuriko kwa kuwaletea vyakula pamoja na magodoro kwa ajili ya kulalia katika maeneo waliyo watengea wahanga hao.

No comments:

Post a Comment